Katika taarifa ya kuondoka kwa Kaka Issa Michuzi kuelekea kwenye mkutano wa Diaspora huko Uingereza nilisoma maelezo kuwa "Kwa mahesbu ya haraka haraka hivi sasa kuna blog zinazotumia lugha ya kiswahili zipatazo 200 ambapo pia blog takriban 10 zinaanzishwa kila siku, na kuifanya Tanzania kuw nchi zinazoendelea katika tasnia ya habari kwa njia ya mtandao."
Hii ilikuwa ni March 24 na kama takwimu hizi ni sahihi, basi tangu post hiyo iwekwe mpaka leo, kuna zaidi ya blog 270 (ukiacha zitakazoanzishwa leo) zitumiazo lugha ya Kiswahili zimeanzishwa. Hii ni takwimu ya kufurahisha (kama kuna jema litendekalo ama kutokea sababu ya blog hizi) na pia takwimu hizi zaweza kuwa BALAA kama tunapotosha jamii ya wasomaji wetu.
Ni lazima kurejea katika WAZO LA MWANZO KABISA lililosukuma kuanzisha blog.
Hakuna ubishi kuwa blogs zimekuwa CHOMBO TEGEMEZI (na pengine maarufu) cha habari kwa watu weengi nchini lakini swali ni kama twajua THAMANI YAKE.
Kuwa na idadi kubwa ya kitu ni jambo jema lakini wema huu huwa sahihi iwapo uwingi wa vitu hivyo waunganisha nguvu katika kutekeleza lengo hasa la kuwepo kwa kitu hicho. Na hakuna tofauti lijapo suala la uwepo na thamani za blog.
UMAARUFU.
Leo hii blog za kiswahili ni nyingi saana na pia umaarufu wa uwepo wa blog hizo wazidi ongezeka siku hadi siku. Ni umaarufu huu unaovutia wengi wazisomao kuamua nao kuanzisha zao.
Na hapa ndipo ninaposhabihianisha blogu zetu na muziki huu uitwao wa Bongo flava.
Huu muziki umekuwa maarufu japo umaarufu huo wabebwa zaidi na wasanii wachache (ukilinganisha na idadi nzima ya wasanii) ambao kwa hakika wanajitahidi kila kukicha kuhakikisha kuwa wanatimiza lengo lao katika kila albamu watoayo kwa kuifunza , kuiasa, kuikanya, kuionesha, kuiburudisha, kuifikirisha ama hata kuweka kumbukumbu ya mawazo yao CHANYA wanayoamini yanahitajika katika jamii na yaliyo sehemu ya suluhisho la matatizo ya jamii. Kwa kufanya hivi wanakuwa maarufu (bila jitihada za ziada). Kwa mimi nisomaye blogu nyingi kwa siku (pengine kuliko wengi wenu) nimeona hili likishabihiana na suala la blogu zetu. Wapo walio wema na waangaliao mambo kwa njia ya suluhisho na ukweli hata kama itamaanisha kuwa tofauti na wengine japo (kama ilivyo kwenye bongo flava, wapo ambao wanachojali ni idadi ya "washabiki" na hivyo kufanya kila wawezalo (hata kama ni potosho kwa jamii) kujipatia "watu"
PAPARA
Kwenye muziki wa bongo flava twaona "mbio za kuwa wa kwanza" kutoa wimbo fulani hata kama haujafanyiwa uhakiki vya kutosha na kupata kilicho sahihi. Hili lashabihiana na blogu zetu ambako watu (bila kuhusisha wasemacho na maudhui mama ya blogu yao), wanakimbizana kuandika habari nyingi (bahati mbaya nyingine si sahihi) na kujifurahisha kuwa na habari nyingi na pengine kuwa wa kwanza kutoa habari lakini haina wazo, fikra wala mtazamo wa mwandishi katika kutueleza kwanini "kabandika" alichobandika.
KUTOSHAURIKA.
Wenzetu wa Bongo Flava wanatambuana kwa watu kutosikiliza maoni ya wenzao na matokeo yake twaona wanavyoishiwa kimuziki na kuanza kuimba "madudu".
KUTOSHAURIKA.
Wenzetu wa Bongo Flava wanatambuana kwa watu kutosikiliza maoni ya wenzao na matokeo yake twaona wanavyoishiwa kimuziki na kuanza kuimba "madudu".
Nimeshaandika mara kadhaa kuwa BLOGU NI SHULE MAANA WAANDIKAO NDIO WAANDIKIWAO NA WAFUNZAO NDIO WAFUNZWAO na mara nyingi nimekuwa wazi kukiri kujifunza kutokana na maoni na ushauri mbalimbali niyupatao toka kwa wasomaji na bloggers wengine. Hili laonekana kuwa tofauti kwa baadhi ya wenzetu ambao hata waachiwapo ujumbe wa kuwaomba kusahihisha baadhi ya sehemu za taarifa zao kwa kuwa zapotosha, wanapuuzia na kuendelea kupotosha wasomaji.
KUWA KAMA FULANI.
Ni lazima tukiri kuwa wapo wasanii wenye kipaji na uwezo mwepesi wa kuandika nyimbo na kuimba. Ni kama vile 'walizaliwa wafanye hivi" ama yawezekana wamewezeshwa kwa urahisi ama yawezekana ni vyote kwa mkupuo. Tatizo laja kwa wale ambao labda wana kipaji lakini hawajawezeshwa ama wana kipaji na uwezo lakini si kwa kiwango sawa na wenzao lakini wanataka "kukimbizana" na waliowatangulia. Tatizo hili laja hata kwetu bloggers ambao wakati mwingine "nature" ya maisha yetu haitupi nafasi ya kusaka na kuchanganua habari nyingi kwa siku lakini twataka kukimbizana na wale walio katika tasnia ya habari ambao blog na maisha yao ya kazi ni vitu viendanavyo. Matokeo yake ndio twashuhudia COPY & PASTE zisizo kifani na ambazo wakati mwingine zatafsiriwa zisivyo ama "zanyonywa" kwa bloggers wa kiTanzania ambao asilia kubwa ya wasomaji wetu ni wale waliotoka kwao. Kwangu huu ni ucheshi na "uvivu wa fikra".
Jana nimepata taarifa toka Neowox kuwa mtu kutoka mji wa 3700 ametembelea blogu yangu tangu nijiandikishe kwao na hili lilinifanya niwaze NGUVU HALISI YA HABARI na namna ambavyo naweza kuwa msaada (kama ntaelimisha) ama naweza kuwa mmomonyoaji wa jamii (kama ntakuwa naotosha)
Labda kama ambavyo wasanii wa Bongo flava wameshauriwa kuwa na semina na makongamano ya mara kwa mara kuwatambulisha umuhimu wa kile wafanyacho na manufaa yake kwa jamii, pengine nasi twahitaji yetu kuhakikisha kuwa wale watuangaliao sisi an wanaotamani kuanzisha blogu zao hawafuati mkumbo ambao (pengine) haujui uelekeako. Tunapaswa kuwa makini na kujifunza (nasita kuita KUIGA) kutoka kwa wale ambao twaona kazi zao zikisaidia kuibadili jamii. Tuwe wepesi wa kuonesha kuwa twajifunza toka kwao na tuwafanye watambue kuwa wanasomwa na kutumika kama darasa ili waweze kuhakiki vema kazi zao huku nasi tukihakiki zetu kama wafanyavyo wao ili na wale waangaliao zetu wahakiki zao kama tufanyavyo na mwisho wa siku, BLOG ZOTE ZITAKUWA MAKINI
NA HUU NI MTAZAMO WANGU KWA NAMNA NIONAVYO TATIZO, LABDA NAMNA NIONAVYO TATIZO NDILO TATIZO
12 comments:
I couldn't agree more Mzee wa Changamoto.
Yep, wala hujakosea kaka. Kwa mtazamo wangu, katika mamia ya blog zetu, walio makini na kublog ni makumi tu. Wengine wapo ilimradi tu wapo. Wengine wapo kwa kuwa wana mambo ya msingi ya kuishirikisha jamii.
Ndo maisha hayo.
Naungana namtani wangu Fadhy ni kweli wapo waengi ambao wameanzisha blog kwa sababu fulani ana blog yaani kuiga tu. Na wapo wengine wana blog kwa maana ya kufunza na kujifunza. Kueneza habari kwa jamii yetu. Ni mada nzuri hii. Ahsante!!
Mzee wa Changamoto hapo umenena. Libeneke la kublogisha limevutia wengi lakini kamthemo ni kale kale tu kuwa wachache ndio wameitwa. Na walioitwa wana malengo madhubuti ambayo ni pamoja na kuelimisha, kukosoa na kuburudisha. Wengi wetu tunatafuta misuluhisho ya migogoro mingi iliyopo katika nafsi zetu na jamii kwa ujumla. Mawasiliano mazuri katika nyanja hizo hapo juu ni muhimu sana. Basi na tutumie mwanya huu kuisukuma jamii hii mbele. Swali la kizushi, je wawezaje kuwa blogger maridadi bila kupitia na kutoa mawazo kwenye blogs za wengine? Ni swali tu jamani!!!
Nimeipenda hii post yako. Bahati mbaya au nzuri nimeijua blog yako wiki tatu tu zilizopita!
Nimeipenda makala yako; nimekuja kupata "tuition" kwasababu libeneke letu ni changa mno (www.vijanafm.com). Tuna malengo yetu lakini tunaona jinsi ilivyokuwa ngumu kuyatimiza. Lakini ndio kujifunza.
Sisi hatuna hata viewers counter! Tunayoyaanika yatabaki kwenye mtandao tukishindwa kuendelea; ambayo sidhani itatokea karibuni.
Swali la Mrope:
Kwanza kabisa, kazi yako ni nzuri (nimeperuzi blog yako hivi punde). Kuhusu kuwa blogger mzuri ni kuwa "original" tu. Kwasababu, binafsi kama nataka kupata habari fulani najua pa kwenda. Sihitaji kwenda kwenye blogs za watu kwa lengo la kupata habari tu. Kama blogger anataka kuzungumzia matukio ya kila siku, basi angalau atoe kitu kama reflection au mawazo yake binafsi -- kutegemea analenga nini hasa.
Pia, kama Masangu alivyosema hapo juu, utafiti ni muhimu sana kabla ya kuandika. Jua kuwa kama blogger kuna uwezekano ukawa una-influence mawazo ya watu wengi. Kwahiyo sio jambo la busara kupotosha jamii.
Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha Vijana FM: www.vijanafm.blogspot.com.
Changamoto kwetu walengwa
Hii posti ni changamoto,kama ilivyo pia blog nayo ni changamoto kwa bloggers.
Wadau walionitangulia nao wametoa changamoto zao.
Mengi yamesemwa,nami ninayo ya kusisitizia.
Binafsi naona feedback ni muhimu sana.Kumbuka kwa blogger aonaye feedback siyo muhimu ndio huyo huyo asiyeona pia umuhimu wa yeye kurudisha feedback kwa comment(s) itakayokuwepo/zitakazokuwepo.
Feedback ni muhimu pia kwani mbali na kumpa mtu moyo,lakini itamfanya ajue ni kwa namna gani ataboresha na pia achukue uelekeo gani.
Bloggers kama ilivyo wasomaji,wanakabiliwa pia na changamoto mbalimbali kubwa zaidi likiwepo la kimtandao.Kwenye nchi zetu ambazo bado zinaendelea,mtandao bado ni tatizo kubwa tofauti na nchi za magharibi.Wapo wanaoblog katika mazingira magumu,ambao ni makini sana,lakini isiwe ni kikwazo,wajitahidi na watumie the only resources walizonazo.
Muhimu pia na la kuzingatia sana kwa bloggers, ni kurudisha feedback kwa waliochangia. Ni muhimu sana kwani hata mchangiaji nae,kwa kuchangia ni ishara kuwa anataka kujua zaidi,tofauti na aliyesoma na hakuchangia kitu.
Amani, Heshima na Upenbdo kwenu nyote.
Shukrani Kaka Jeff kwa kukubaliana na ujumbe huu. Najua wewe ni mtembeleaji mkuu wa blogu nyingi na unajionea mengi.
Kaka Fadhy na Dada Yasinta, NAKUBALIANA nanyi kuwa sote "tupo tupo" na walio na nia watasalia.
Kakangu Matondo. Umetoa mfano wa Kaka Simon nami nasema angalau huwa anapata maoni mawili matatu. Ninayemuona ana moyo usiopingika ni mtu ambaye anaandika kujaribu kuwanufaisha waTanzania wenzetu na bado wanachofanya ni kutomsoma na pia "kumponda". Namzungumzia Kaka Boniface Makulilo Jr. Wapo wengi namna hii na wengi wetu ni hawa waliotoa maoni hapa (nawe ukiwa mmoja wapo).
Kuna siku nilikuta maoni kwa Uncle Kitime ambapo mtu alikuja na hoja hiyohiyo kuwa "fanya hivi ili uwe kama Michuzi". Nikawaza kuwa ni wangapi watataka kumuiga Michuzi? Michuzi ni Michuzi na kazi yake njema anaifanya nasi "twajazia" yasiyo kwake.
Anyway..Kama ulivyosema,tuko kwenye MAPITO na sasa ni "Struggle for Existence and the Survival of the fittest"
Uncle Mrope nawe umenena. Kuhusu swali lako ni kuwa kufikiri kuwa unaweza kuwa blogger maridadi bila kupitia na kutoa mawazo kwenye blogs za wengine nadhani ni sawa na kuamini kuwa MAMAKO NDIYE MPISHI BORA ZAIDI DUNIANI ILHALI HUJALA KWINGINE KOKOTE. Looool!!!
Kaka Steve, shukrani saana kwa kuwa nasi. Karibu saana na tupo PAMOJAH.
Uncle Kitime, umenena kwa ufasaha kabisa kuwa ni CHANGAMOTO YETU SOTE. Uandikayo hayaishi muda (labda yatimizwe) na ndio nguvu ya ukombozi. Yaani kuandika kisicho-expire mpaka kitendewe kazi.
Kaka Albert wajua changamoto zako zilivyo. Asante kwa ushiriki na pole kwa mara kadhaa ambazo nimekosa muda wa kurejesha "mlishonyuma" (feedback) Hahahahaaaaaaaaa.
PamoJAH Kaka
Usihofu kaka ,pamoko saaaaaaaaaana,niliweka kamsisitizo tu kaka yangu mpendwa. Pamoja daima.
Naomba kukupongeza kwa uchambuzi huu makini.Pamoja na pongezi hizo,naomba uniruhusu kutofautiana nawe japo kidogo.Kwa mtizamo wangu (unaoweza kuwa si sahihi) lengo la kuanzisha blogu linabaki kuwa miliki ya bloga husika.Kwa mantiki hiyo,bloga anaendelea kuwa na haki na uhuru wa kuendeleza maudhui ya awali ya kuanzisha blogu yake kama ambavyo anavyokuwa na uhuru wa kubadilika kulingana na sababu mbalimbali (kwa mfano kwenda na wakati,kutanua hadhira,nk).Blogu si Biblia au Koran kwamba kubadili cbochote ni kukufuru.
Pia,tunaweza kuwa hatuwatendei haki bloga 'wanaoendeshwa na kusaka umaarufu,au 'wanaoiga'au 'wanaokurupuka',nk kwa vile kile tunachoita kusaka umaarufu,kuiga au kukurupuka kinaweza kabisa kuwa ni sehemu ya ubunifu wao.Na katika 'kuiga' huko inawezekana wanachofanya ni kufuata mkondo wa vinara wa fani.Tunashuhudia kwenye soka,kwa mfano,wanasoka chipukizi wanavyojitahidi 'kuiga' idols wao kama Beckham,Messi,nk.Kama 'kuiga' huko kunaweza kuzaa maendeleo basi nadhani ni jambo jema.Kumuiga mzee wa changamoto ili nami niweze kuitumikia jamii kiufanisi au haya nikidhi tu mapendezeo yangu si jambo baya (kwa mtizamo wangu).
Halafu,ninahofu kuwa bloga 'wageni'au'wachanga' wanaweza kutuona hatuwatendei haki 'kwa kuhukumu kazi zao'.Wanaweza kujiuliza tumepata wapi mamlaka ya kuunda vigezo vya ubora wa blogu (kwa kuzingatia mazingira yetu).
Sambamba na hilo ni swali nililowahi kujiuliza huko nyuma: tunablogu kwa ajili ya jamii au kwa ajili yetu?Jamii ni mkusanyiko wa watu wenye akili,upeo,ladha na matamanio tofauti,na kwa hali hiyo ni vigumu 'kuiridhisha' yote.Nafsi,kwa.upande.mwingine,ni moja.Ni mimi au wewe au yeye.U-moja huu unarahisisha kuridhika.Ni rahisi kuridhisha nafsi yangu kuliko ya mtu mwengine au kundi.Kwa.mtizamo wangu,alimradi bloga 'hachafui hali ya hewa' basi anaweza kufanya 'ile kitu roho yake inapenda' iwe ni kufuata nyayo ( 'kuiga') nguli wa fani au 'kuja kivyake'.
Binafsi sina tatizo na kukopi na kupasti alimradi huyo 'mkopaji' anaweka angalizo kuwa alichoweka hapo ni kwa mujibu wa au hisani ya flani.Hivi magazeti,radio na televisheni si ndio wanaongoza kwa kukopi habari?Na si kwamba kila mara wanafanya hivyo kwa kupenda bali habari zao nyingi hupatikana kutoka chanzo kimoja,hususan 'wire services'.Si ajabu kukutana na Habari kutoka Reuters au AFP ikiwa kama ilivyo kwenye magazeti,tv,redio na tovuti mbalimbali duniani.Sanasana itakuwa imeongezwa maneno mawili matatu au picha.Nafahamu kuwa neno linalotumika ni subscription lakini kimsingi ni copy and paste.
Tukumbuke kuwa si kila anayeanzisha blogu anataka kuelimisha,kuhabarisha,kuburudisha au kukosoa.Kwa vile kimsingi blogu ni mithili ya personal diary japo kwa mazowea tu inatarajiwa kuwa kama chombo cha habari basi kilicjomo humo kinategemea zaidi matakwa ya mmiliki kuliko sisi 'tunaoamua wenyewe kutembelea diary husika' (pengine diary si neno mwafaka lakini nadhani nimeeleweka).Kama kilichomo humo hakiendani na ladha,matarajio au matakwa yetu,tunaachana na diary hiyo.
Nimalizie kwa changamoto ndogo.Ukitafuta blogu zinazojihusisha na teknolojia ya android,kisha ukatembelea japo 20 tu,naamini utaafikiana nami kuwa exclusive content kwenye chapisho ina ugumu.
Post a Comment