Tuesday, April 13, 2010

Dk. F. Mghanga AKUMBUKA ILIVYOKUWA TANZIA YA EDWARD MORINGE SOKOINE

Edward Moringe Sokoine (1938 - 1984)
Ni miaka ishirini na sita iliyopita. Siku ya Alhamisi, majira ya jioni kama saa kumi na moja. Anga la jiji la Dar es Salaam lilikuwa jeusi likihanikizwa na mawingu madogo madogo yaliyojikusanya kuashiria kamvua kalikokuwa kametawala siku hiyo. Hizi ni nyakati za masika katika sehemu kubwa ya nchi.

Ndo kwanza nimerudi toka shule, tayari nimeshajipakia ugali wangu wa njano (Yanga) na maharage ya Iringa.

Nipo mtaani nikicheza na wenzangu chandimu. Hatuna viatu, tupo pekupeku lakini hatujali kitu. Maisha yalikuwa mazuri bila kujua adha na masumbufu ambayo wazazi walikuwa wanayapitia ili kutufanya watoto wao tuweze kwenda chooni.

Nikiangalia pembeni, akina mama walikuwa wamekaa wakisukana na wengine walikuwa kwenye vibustani vyao wakipalilia matuta ya viazi vitamu. Hakika hatukujua lililokuwa limetokea masaa machache yaliyopita hapa nchini kwetu.

Lakini ghafla redio zikaanza kupiga wimbo wa taifa. Si aghalabu kusikia wimbo wa taifa mida kama ile tena kipindi kile kisichokuwa na sikukuu wala mgeni yeyote wa kitaifa. Haiyumkiniki kuna jambo kuu limetkea. Katika utoto wangu, ghafla nikaacha kucheza, akina mama waliokuwa wakisogoa nao wakapigwa na ubaridi wa ghafla. Katika mshawasha wangu wa kitoto nikaijongelea redio kutaka kujua kilichojiri jioni hiyo ya Alhamisi nyeusi. Dakika kadhaa zilipita kabla ya wimbo wa taifa kuisha.

Sauti iliyojaa huzuni ikasikika. Hata katika utoto wangu, naweza kusema kwa hakika kuwa sauti ile ilikuwa katika huzuni na majonzi na ilionesha ni ya mtu aliyekuwa katika kilio muda si mrefu uliopita. Naam, ilikuwa ni sauti ya hayati baba wa Taifa. Nayakumbuka maneno yake mpaka sasa. Hivi ndivyo alivyosema:

"Ndugu wananchi, leo mnamo majira ya saba mchana, ndugu yetu, mwenzetu, Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais, Edward Moringe Sokoine amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea huko Morogoro wakati akilejea Dar es Salaam kutoka Dodoma kwenye mkutano wa Bunge"

Naam, hiyo ndiyo sababu ya kupigwa kwa wimbo wa Taifa jioni ile. Utando mweusi ukatanda. Simanzi ikatawala. Vilio vikasikika, furaha ikatoweka. Giza la mawingu meusi likaongezea upotevu wa furaha. Nikausikia ukelele mkuu kutoka kwa mama mmoja aliyekuwa ameshika jembe akipalilia bustani yake "Mama wee mkombozi wetu amekufa, nani atatutetea sisi wanyonge?" Hakika ndivyo aliomboleza mama yule.

Huzuni kuu ikaniingia ghafla. Nikajiwazia "Sokoine kafa? Hapana, amekufa?" Nafsi ilikataa kuamini, akili ya utoto ikaniambia haiwezekani. Ghafla machozi yakaanza kunitiririka. Naam nililia. Nilimlilia mzalendo wa kweli. Wazazi walilia, wananchi walilia, hata Nyerere alilia tena hadharani, hakulia kiunafiki alilia kweli.

Watanzania wapenda haki tulilia, tulimlilia mpenda haki mwenzetu. Sokione mzalendo wa kweli. Mwana wa Kitanzania asilia, mtetezi wa kweli wa wanyonge, mchapakazi, mpigania mema ya nchi.

Naam, yawezekana kwa wengine ameshafutika lakini kwa wapenda haki, Sokoine atabaki kuwa kioo chetu daima. Huyu ndiye mtu aliyekuwa na sifa nilizozitaja wakati ule kwenye ile ndoto yangu ya "Namuona mtu huyu". Yawezekana alikuwa na kasoro zake kama mwanadamu na hata kiutendaji lakini daima nia yake njema kwa watu wake iliyafunika makosa yake hayo. Alipendwa na wanyonge na kuchukiwa na wezi, wabadhiifu wa mali ya umma na wahujumu uchumi (leo tunawaita mafisadi). Huyu ndiye aina ya mtu tuliyemuhitaji Tanzania ya leo.

Nimemkumbuka Sokoine, mtanzania mzalendo mwana mpenda nchi aliyenifanya nihisi msiba wake kuwa unanihusu kwa ukaribu mno. Naam, wajamaa kama kina Subi lazima watamkumbuka mtu huyu na kumuomboleza daima.Mungu alipenda kumchukua ingawa tuliona amemchukua mapema mno.

Pumzika kwa amani Baba Sokoine, mtanzania na mzalendo wa kweli.

Amina!
Dk. F. Mghanga, MD

SHUKRANI KWA DA SUBI KWA KUTUSHIRIKISHA HII
Mara zote nimekuwa nikimtambulisha Da Subi kama MUUGUZI MKUU WA BLOGU HII (kutokana na kushiriki kuirekebisha blogu hii ki-ufundi)
Kwa aliye na mashaka naombe asikilize UBUNIFU NA UTUNDU wa Da Subi katika audio clip zake
HAPA

1 comment:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kifo cha hyu bwanakina mushkeli mpaka kesho