Saturday, April 3, 2010

Yote waliyowaza "YALISAIDIA"

Kipengele cha WALIWAZA NINI kinakuja mapema wiki hii kupisha sherehe za Pasaka. Na pia hatutakuwa na mengi ya kutuwazisha.
Leo hii ningependa kuangalia MAWAZO ambayo kwa namna moja ama nyingine "yamesaidia" kupata usuluhishi wa jambo fulani. Iwe ni kuokoa maisha ama kurahisisha kupata suluhisho fulani. Yote juu ya yote, waliyowaza YALISAIDIA.

Nianze na wazo alilokuwa nalo Kaka Albert Paul (pichani juu)ambaye aliliweka kwenye blog yake ya MWANGAZA katika mfumo wa Chemsha Bongo. Aliuliza swali ambalo nilikosa jibu, kisha nikajaribu kuwatafsiria wafanyakazi wenzangu kazini kuona nao wangefanyaje lakini jibu langu na lao yakafanana. ALIWAZA NINI kuweka hii chemsha bongo? Ati ameuliza "Utachukua uamuzi gani pale mlinzi wako wa usiku anapokusimulia ndoto aliyoota usiku wa leo na anakutaka uahirishe safari yako kwani safari yako kulingana na ndoto yake inaonyesha basi utakalosafiria litapata ajali na watu wote watapoteza maisha? Fikiria kuwa umeahirisha safari na kweli ajali ikatokea,kwa maana kuwa ameokoa maisha yako. Utamfukuza kazi au utaendelea kuwa naye?"
Vyovyote iwavyo, alichowaza mlinzi kisha akakisema kilisaidia kumjulisha bosi wake kuwa wakati mwingine huwa "anapitiwa" na pia ni kupitiwa huko kulikookoa maisha ya "bosi" wakeAssociated Press Image
Na sasa tumzungumzie Albert Bailey (pichani juu) ambaye wiki hii naye ameushangaza ulimwengu kwa alichowaza baada ya kupiga simu kwenye benki kuwapa taarifa kuwa atakuja kupora kiasi cha pesa hivyo wamuandalie pesa hizo kwa kuziweka kwenye mfuko (naamini ili kuharakisha uporaji). Na baada ya dakika kumi, alikuja "kuchukua pesa alizoweka miadi" lakini kwa bahati mbaya waliompokea sio wahudumu na pesa, bali akapokelewa na askari wakiwa na pingu. ALIWAZA NINI? Lakini wazo lake lilisaidia kurahisisha kazi kwa polisi, kupunguza makimbizano na hata kuokoa maisha (kama angefanya uporaji kwa kutumia silaha).


Soma habari kamili HAPA
Lakini si Bailey pekee ambaye aliisaidia Polisi kumkamata kwa urahisi, ALEN NGUYEN (pichani juu) aishiye Florida aliisaidia polisi kumnasa kwa urahisi baada ya kurejea kwenye duka aliloiba tiketi za bahati nasibu na kutaka ku-cash tiketi moja iliyokuwa impatie dola 50. Nguyen mwenye miaka 22, alituhumiwa kuiba tiketi zenye thamani ya dola 70 na kisha kurejea kwenye duka hilohilo aliloiba ku-cash tiketi yake. ALIWAZA NINI???
Soma habari yake kamili HAPA

Huyu alinikumbusha ile habari ya binti aliyeenda BAR kupata huduma lakini alipoombwa kitambulisho na mhudumu, akatoa kitambulisho cha mhudumu ambacho kilikuwa kimeibiwa. Jikumbushe HAPA

***"Waliwaza nini ni kipengele cha kuelimishana tukifurahia. Hiki kitakuwa kikikuletea habari za kweli na kushangaza kuhusu watu ambao wamefanya yale ambayo unaweza kujiuliza kuwa WALIWAZA NINI? wakati wanatenda haya.
Kitakuwa na habari fupifupi kutoka ulimwenguni kote. Kwa habari zaidi kuhusu kipengele hiki
BOFYA HAPA"***

3 comments:

Fadhy Mtanga said...

Hawa watu sijui hata waliwaza nini? Lakini mawazo yao yamesaidia sana.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ile ya mlinz mimi siikubalii kwani aamini halali usiku, labda alipanga mwenyewe hiyo ajali

harafu ni mlinzi gani atakwabia aivyolala na kuota???

hakuwaza huyo

Albert Kissima said...

Binadamu tuna namna tofauti za kuyachukulia mambo.Kuna mazingira ambayo mtu hulazimika ku-act tofauti na utaratibu unaokubalika na uliozoeleka lakini kwa manufaa sahihi na yakubalikayo ya wahusika. Chemsha bongo niliyoitoa inahitaji hisia za ndani za mtu zikiambatana na kiwango fulani cha "risk" ili kufikia muafaka. Anachosema kaka Mubelwa ni kweli kuwa, hatua ya mlinzi kumwambia bosi wake kuhusu ndoto ile,ilimsaidia bosi; kwanza kwa kumrefushia maisha na pili kutambua kuwa mlinzi wakati wa usiku huwa anauchapa usingizi tena hadi na "kuota ndoto". Pamoja na mlinzi kukiuka taratibu za kazi ambazo kwa upande mwingine zingeweza pia kuhatarisha maisha ya bosi na familia yake na pengine hata kuleta madhara makubwa zaidi au sawa na ambayo yangetokea kwenye ajali, bosi aliukubali ushauri wa mlinzi. Je bosi akiwaza madhara yatokanayo na mlinzi wake kuuchapa usingizi wakati wa lindo na ni mara ngapi huwa anafanya hivi, na ni madhara gani yatokanayo na mlinzi kulala, mlinzi ataweza kusamehewa?
Si wote wenye uvumilivu wa kumsikiliza mwingine na kuyafanyia kazi yale aambiwayo hata kama yanagusa maisha yako kwa kiasi gani. Wapo ambao wangemtimua mlinzi hapo hapo na wala wasingefuata ushauri wake.

Nilichokuwa ninawaza ni namna gani watu wanavyoweza(wakati mwingine)kuchukua maamuzi sahihi kwa kujali pande zote bila kufuata utaratibu uliopo,bali kwa kutumia utaratibu wa muda lakini wenye tija kwa pande zote. Namna hii ya kuwaza inategea mtu na mtu na hutegea sana na hisia alizonazo mtu kwa mtu mwingine.



Dah! Huyu somo wangu na huyu yanki mwingine,mimi sijui waliwaza nini kwa kweli,nikijaribu kufikiria sipati ni nini hasa walitegemea,na naishia tu kujiuliza maswali:
walitaka umaarufu tu?
Walitaka kujulikana au ni nini?
Maisha ya uraiani yaliwashinda?
Pengine walitaka kuweka rekodi ya dunia?
Hakika maswali ni mengi na bado najiuliza "waliwaza nini".


Na nazidi kuwaza kaka Mubelwa naye "aliwaza nini" kwenye "WALIWAZA NINI" ya leo kwa kuhusisha majina yaanziayo na "A" na mawili yakifanana kabisa. Hahahaha! Just a joke.