Tuesday, May 11, 2010

Isaya Zephania Yunge......Kijana wa sasa, kwa Tanzania ya sasa

Destiny.
Nimekuwa nikisema kuwa MPAKA KESHO ITAKAPOHESABIKA KUWA LEO, BASI VIJANA HATUTAENDELEA. Maana kubwa ya sentensi yangu ni kuwa mambo ya msemo wa VIJANA NI TAIFA LA KESHO hauna maana.
Hauna maana kwangu kwa kuwa wazee wanaendelea kung'ang'ania madaraka mpaka vijana wanapoelekea kuuacha ujana na wakati huo ndipo tunapojikuta tumekosa la kufanya kwa kuwa tulikuwa tukisubiri hiyo KESHO ambayo haijawahi kufika na haitafika. Hakuna ubishi kuwa wazee wengi na hasa kwenye siasa za nyumbani na ambao ndio wanaoonekana kuhusika katika maamuzi mengi yahusuyo Taifa na Vijana wanategemea saana uzoefu na wanatueleza kuwa hatuna UZOEFU katika kushauri na kuamua, lakini wanasahau kuwa "The trouble with experience is that by the time you have it you are too old to take advantage of it. " — Jimmy Connors
Lakini kati ya watu wachache ambao wameonesha kuanza harakati za kuibadili dhana hiyo potofu na kuamua kujikita katika kuibadili jamii yetu akiwa na umri wa ujana ni Kaka mdogo ISAYA ZEPHANIA YUNGE. Ni kijana mdoog ambaye ameweza kuwa na mipango halisi ya kuibadili jamii yetu. Niliweza kuwasiliana naye kwa njia ya mahojiano ya maandishi na kisha kupanga kufanya mahojiano ya sauti na kuyarekodi kwa njia ya simu. Mipango yangu ilishindikana ila alikuwa mkarimu saana kunieleza kila nilichohitaji kujua kuhusu yeye kwa njia ya maandishi na nikaona nishirikiane nanyi katika kipengele hiki cha MWANANCHI MIMI ambacho ni maalum kwa wale waliokwenda "mwendo wa ziada" kuiokoa jamii.
Isaya alizaliwa 23/03/1990 katika kijiji cha Nyangunge, wilaya ya Magu, mkoani Mwanza akiwa ni mtoto wa kwanza katika kwa wazazi wake ambao walitengana akiwa na miezi michache tangu kuzaliwa. Akielezea anavyokumbuka maisha yake ya utotoni, anasema "nikiwa na umri mdogo mama yangu alilazimika kunipeleka kuishi na bibi yangu wilayani Magu ambapo Bibi alikuwa akijishughulisha na Siasa, Kilimo na Ufugaji hivyo kukua na kulelewa hapo na bibi yangu ambaye alinifunza kilimo cha mpunga na ufugaji wa ngombe, mbuzi na mondoo, nikiwa na umri wa miaka mitano tayari nilikuwa Mchungaji bora wa Mbuzi na Mhamiaji wa ndege katika mashamba ya Mpunga."
Harakati za Isaya katika kuikomboa jamii ziliznza mwaka 2005 ambapo alianza kufanya kazi za kujitolea katika shirika lisilo la kiserikali liitwalo KULEANA na akiwa hapo, walikuwa na kikundi cha watoto kilichoitwa SAUTI YA WATOTO,ambacho kiliwawezesha kupata mafunzo mbalimbali ya haki za watoto na wajibu wao na kupitia mafunzo hayo, waliweza kuelimisha jamii kwa njia ya redio, ambapo walikuwa na kipindi kila Jumamosi katika kituo cha Radio free Africa ya jijini Mwanza, kipindi ambacho kilikuwa kinafadhiliwa na UNICEF.
Hata hivyo, nia ya kujielimisha haikuishia hapo, kwani Isaya amenieleza kuwa "mwaka 2006 nilipata mafunzo ya uelimishaji rika juu ya masuala ya UKIMWI chini ya mradi ulioitwa Abstinence and Behaviour Change to Youth (ABY) uliokuwa unadhaminiwa na International Youth Foundation. Tangu hapo nimekuwa nikifanya kazi kama muelimishaji rika wa kujitolea mashuleni na katika jumuiya na kwa sasa natoa zaidi mafunzo hayo ya UKIMWI na stadi za maisha kwa Watoto wa mitaani , vile vile kupitia kipindi cha redio-katika redio iitwayo Passion FM nimeweza kutoa mafunzo hayo kwa hadhira kubwa zaidi juu ya masuala ya UKIMWI, stadi za maisha, na haki za watoto. "
Mwaka 2006, Kaka Isaya alichaguliwa na wajumbe wa baraza la watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo, ambalo liko chini ya usimamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Akiwa na washiriki wenzake wa Junior 8
Mwaka unaofuata (2007) alichaguliwa kuwakilisha Tanzania kama UNICEF-Youth Ambassador katika Mkutano wa Junior 8 ambao ni mkutano tangulizi wa vijana wa nchi za G8, katika mkutano huo uliokuwa na vijana 75 kutoka nchi za G8 na nchi zinazoendelea ambazo ni Brazil,China, Tanzania, Sierra Leone, Central Africa Republican, Ethiopia, India, Moldova, Algeria na Cameroon ambapo nchi hizi zilitoa vijana 10 ikiwa ni mmoja kila nchi. Anaendelea kunijuvya kuwa "nikiwa katika mkutano huu nilichaguliwa kuwa UNICEF-Africa Youth ambassador na nikahudhulia kikao cha G8 ambapo nilipata nafasi ya kuongea na kuwakilisha maoni yangu."
Akiwa na viongozi George Bush na Tony Blair katika mkutano wa G8
Mwaka 2007, Isaya alianzisha shirika lisilo la kiserikali liitwalo JUNIOR 9 FOUNDATION, ambalo linashughulika na watoto wa mitaani na waishio katika mazingira magumu. "Junior 9 Foundation inawasaidia kwa kuwapeleka shule watoto wa mitaani ili wapate elimu ya msingi na kutoa vifaa na mahitaji ya shule kwa watoto waliokatika mazingira magumu."
Kwa hakika niliguswa, nimeguswa na nimefurahishwa saana na HARAKATI za Kaka mdogo Isaya na nimeona ni vema kumleta hapa KUENZI juhudi zake za kuibadili jamii akiwa na umri muafaka.
Kwa sasa anasoma kidato cha tano TAQWA HIGH SCHOOL-Ghana Campus.
HEKO KAKA ISAYA NA MUNGU AKUJAALIE
Naomba nisindikize pongezi zangu kwa UJANA WA LEO wa Isaya na kibao hiki kiitwacho YOUTHS TODAY

6 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hakika ukijiamini utafanikiwa, nimesoma habari hii na nikajikuta machozi yananitoka yaani yale machozi ya furaha. Kwanza napenda kumpa pongezi zangu bibi Isaya kwa malezi alompa Isaya pia napenda kumpongeza sana Isaya kwa uvumilivu wako, kwa kijiamini. Maana kuna wengi wanaosema mimi nataka kula plau wakati hata ugali hajala. HONGERA SANA KAKANGU na nakuombea kwa mungu uwe na mafanikio na maisha mema.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nilikutana na huyu bwana mdogo miaka miwili iliyopita, kweli anajitahidi bwana

Christian Bwaya said...

Kijana mdogo kimwili lakini mkubwa kiakili kuliko wakubwa kimwili. Watu kama hawa bila hata msaada wa kiserikali wanafika-ga mbali.

Kwa hiyo, kwa kasi hii hata kama sera ya serikali ni angoje kesho, huyu bwana mkubwa kwake itakuwa ni mbele kwa mbele mpaka kieleweke.

Namtakia kila la heri. Atufunze kujisimamia katika ya kundi la wazee wenye hamu yakuhodhi kila kitu

Anonymous said...

Big up best

Unknown said...

Smart guy,god bless him for sure

Unknown said...

Smart guy,may god bless him kwakweli