Monday, August 23, 2010

Za Kale vs Maisha ya sasa MASAFA MAREFU

Kwa mujibu wa Uncle Kitime, Tancut Almasi Orchestra, hapa wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma. Toka kushoto.. Ray Mlangwa, Bakari Buhero, Hashim Kasanga, Mohamed Shaweji, John Kitime, Kalala Mbwebwe, Kawelee mutimwana,Abdul Mngatwa, Kibambe Ramadhan, Zacharia daniel, Akuliake 'King Maluu' Salehe. Bahati mbaya Ray, Hashim, Kalala, Zacharia wameshatangulia mbele ya haki. Kuna utata kuhusu alipo Mohamed Shaweji.
Ni Jumatatu nyingine njema. Baada ya pilika za mwisho wa wiki, tunaianza wiki mpya ya kazi. Wengi wetu tumelazimishwa na maisha kusafiri toka mahala pamoja kwenda pengine. Na katika safari hizo, si nyakati zote tumeweza kusafiri na wale tuwapendao. Na wakati mwingine tunasafiri kwa muda mrefu na umbali mrefu.
Labda sasa hivi mambo ya mawasiliano si tatizo hasa kwa kuwa hii "teknolojia" inatuweka karibu. Twaongea na kuonaa kwenye mitandao ya kisasa na hili latufanya tuwe karibu ingali tuko mbali.
Lakini bado nawaza MAAGANO waliyokuwa wakiyafanya WAPENDANO pale wanapojua kuwa hawataonana kwa muda mrefu ujao. Nawaza na kufananisha na waaganavyo wanajeshi waendao vitani ambao wanakuwa na nafasi chache ya kuwasiliana kama tufanyavyo wengi tuishio URAIANI.
Nawaza ilivyokuwa na ilivyo kwa wale waaganao pale waendapo MASAFA MAREFU.
Sikiliza kibao hiki chao wana Tancut Almasi Orchestra walipoimba kibao hiki MASAFA MAREFU. Nilibahatika kumuomba UNCLE JOHN KITIME, mwamuziki mkongwe amilikiye Blogu ya WANAMUZIKI TANZANIA! na ambaye ameshiriki katika utunzi na nyimbo nyiingi ukiwemo huu na nilipomuomba maelezo ya wimbo huu, alinieleza kwa ufupi kuwa "Nyimbo hii ilirekodiwa katika awamu ya pili ya Tancut, Naiita awamu ya pili kwa kuwa Kawele alikuwa kishajiunga japo hakupiga chochota katika kazi hii. Ulitungwa na Kasaloo Kyanga akishirikiana na pacha wake Kyanga onga japo naona walikubaliana kuwa Kasaloo ndo mtunzi. Solo, Shaban Wanted, Rythm John Kitime, Second solo Ikunji Ramadhani, Bass Amani Ngenzi,Keyboards Abdul Salvador,Trumpets Ray Mlangwa na Buhero Bakari, Saxophone,Mafumu Bilali, na Abdul Mngatwa, Drums Kejeli Mfaume, waimbaji Kasaloo Kyanga, Kyanga Songa, Hashim Kasanga, Mohamed Shaweji. Kazi hii ilirekodiwa RTD."
ASANTE UNCLE KITIME KWA UELIMISHAJI WAKO USIOKOMA.
Sikiliza, burudika na elimika kwa kibao hiki, MASAFA MAREFU

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

2 comments:

Subi Nukta said...

Asante sana kwa burudani murua. Sikuwa nimeusikia wimbo huu, sasa ndiyo nausikiliza.

emu-three said...

Kweli ya kale dhahabu...kuna miziki ukiisikilza inakupeleka mahala fulani enzi hizo...jamani maisha