Thursday, September 30, 2010

Majina haya ya wa-Haya....na haya majina kwa wa-Haya

Ni zaidi ya majina haya na wa-Haya
Nyumba ya asili ya waHaya
Photo credit: Zenjidar.co.uk
Sina hakika kama naweza kukueleza kwa ufasaha kwanini tuna majina. Lakini bado nayaona kama kiunganishi cha sisi tuliokuwa, sisi tuliopo na sisi tujao. Novemba 24, 2008 niliuliza Ni kweli majina yetu huathiri mustakabali wa maisha yetu? (bofya hapa ) na bado naendelea kuliwaza hilo. Lakini pia najua kuwa baadhi ya majina yetu huathiriwa ama kutokana na baadhi ya matukio ama kuonesha ama kutabiri kitu kutuhusu.
Nawajua ndugu zangu ambao majina yao huendana na msimu waliozaliwa. Wapo ambao majina hutokana na kitu ama tukio kubwa la siku waliyozaliwa (mfano rafiki yangu Sisiemu ambaye alizaliwa siku ya kuanzishwa kwa chama cha Mapinduzi ama VALENTINE aliyezaliwa Februari 14).
Nimepata kujiuliza haya baada ya kumaliza kuandika kazi ya shule ambayo ni RIPOTI ya habari, na aliyetakiwa kuisoma akaniomba kuandika "Ban-dee-oh" kumuwezesha kusoma. Kisha akasema jina langu ni gumu na ningehitaji "nick name". Nikamshangaa kwa kuwa yeye ana jina ambalo KWETU lingeitwa ambavyo asingeelewa. Jina lake ni FREDRICK ambalo utalisoma huko mbele tunavyolitamka "kwetu".
Lakini nikaishia kuwaza kwanini majina yanakuwa "MAGUMU" kwa wengine? Kwanini imuwie vigumu kusema Mubelwa lakini aseme Schwarzenegger
Ni kwanini aliye nyumbani ataweza kusema Nzunzulima ama Lutatinisibwa ama Ng'wanambiti ama Kitururu na hata Ngonyani na ashindwe kusema majina mengine?
Nikawaza majina ya kwetu, kama yangu na mengine kama ya Kakangu Lutatinisibwa, Lutabasibwa, Mkagendage, Kokuijuka, Mutalemwa na mengine mengi yawashindayo watu. Lakini nikageukia upande wa pili kuangalia majina ya "wazungu" yawashindayo wa-Haya wenzangu (hasa wakongwe).
Basi ukienda kwetu ukasikia baadhi ya majina, waweza dhani ni mapya ama ya kilugha kumbe sivyo.
FREDERICK.... Wewe waitamka hivyo wakati kwetu ni FIDILISHI
SYLVANUS uijuayo wewe, kwetu yaitwa SILIBWANDI.
SYLYVESTER unayoifahamu, kwetu ni SILIBWELI.
JUDITH kama ya "Komando" kwetu ni YUDESI.
Yapo mengi ya kuwaza na kuwazua kuhusu uitwaji wa majina
JE! Ni utashi wa waliotangulia ili kukufanya wewe uchukie majina ya wengine? YAWEZEKANA.
Kwani kuna lipi gumu la kumfanya mzungu ahangaike na Mubelwa na aweze Schwarzenegger?
Kuna ugumu gani katika Frederick kwa mhaya kuacha kujaribu kuliita sawa akaliita Fidilishi?
Labda ni yaleyale niliyofunzwa mwanzoni mwa miaka ya '90 nilipokuwa mikoa ya kusini kuhusu ndugu zetu wa ukanda wa Msumbiji ambao walijichora nyuso zao kuharibu thamani yao kwa WAKOLONI (ama madalali wao), NA INASEMEKANA ILIFANYA KAZI.
Labda na ndugu zangu hawakupenda watu wengi wachukue majina ya ki-magharibi wakaamua "kuyaharibu" na kama ndivyo basi walifanikiwa kwani naamini waHaya ni kati ya makabila machache yenye watu walio na majina yao ya asili.

Labda pia ni kampeni ya watu wa Magharibi kuhakikisha majina yetu hayaingii kwao.
Labda majina hayo ya ki-magharibi hayawapendezi wa-Haya..... na labda majina haya ya wa-Haya hayasomeki kizungu, lakini naamini NI ZAIDI YA MAJINA HAYA NA WA-HAYA.
Kwani kwenu kunalipi la hivi?
NAWAZA KWA SAUTI TUUU

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hakika leo umetoa wazo la kufirikiriisha. Ni kweli hapa duniani tu waajabu sana binnafsi napata sana taabu hapa na jina langu ni lazima nitaje kila herufi.
Haya kwetu ungonini kuna majina kama hayo ya asili mengi tu nikianza kuorodhesha hapa nitamaliza kurasa mia moja. Labda nitaje mawili matatu kwa mfano Magulukwenda, Ngondovahangi, nk. Ahsante sana kwa kunifikirisha kwa leo kuna kitu nimepata hapa,

emu-three said...

Labda, labda, labda...majina hayo yalitolewa kutegemeana na maana yake, kwahiyo wakatafsiri kwa lugha yao, labda, isiwe hivyo...
Kweli ni wazo kutafakari, kuwa haya majina ni kwanini lugha hii yaitwe hivi na hii yaitwe hivi...labda tutafute!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

wahaya ni watu wenye lugha yao na matamshi yao wasiopenda shida, kwa mfano kiingereza, kuna majina mengine kama bonface hutamkwa BENEFANSI, james JEMUSI, julian YULIYANA, nk,

ila sasa majina mengine na matamshi yake duhu
ngombe, ngambo nk nk