Tuesday, December 21, 2010

Mhe. Nyalandu na ubunifu wa kulalamikia "walalamikaji wasio wabunifu"

Photo Credit: Lazarosnyalandu.com
Mtandao wa gazeti la Mwananchi toleo la jumapili ya Desemba 12, uliweka habari iliyomkariri Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko Mheshimiwa Lazaro Nyalandu akisema "Watanzania wanaoishi nje ya nchi, wamekua walalamikaji tu kuhusu taratibu za uwekezaji, lakini hawachukui hatua."
Aliyasema haya alipokuwa akifanya mazungumzo na gazeti hilo baada ya kuzindua Kampuni ya Ndege ya Bold Air katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl JK Nyerere jijini Dar.
Kampuni hiyo inamilikiwa na Ndg John Ndunguru, mTanzania anayeishi Marekani.
Kisha Mhe. Naibu Waziri akaongeza kuwa “Kitendo cha kulalamika bila ya kuchukua hatua ni ishara kwamba wengi wao sio wabunifu. Nampongeza ndugu yangu John Nduguru, kwa kutumia fursa hiyo na kuanzisha kampuni hii,”
NAIBU WAZIRI ANAKOSOA ULALAMIKAJI NA UBUNIFU ilhali mwenyewe anakiri kuwa hali ya uwekezaji si njema na kuwa serikali ya awamu ya nne inapanga "kuwaandalia Watanzania mazingira bora ya uwekezaji kama ambavyo imekuwa ikifanya, ili kila Mtanzania aliyeko nje na mwenye uwezo wa kuwekeza, aje kufanya hivyo."
Baada ya kusoma makala haya na kuyatafakari (na kuombea fikra changanuzi) nimeishia kusikitishwa na UBUNIFU ALIONAO NAIBU WAZIRI KATIKA KULALAMIKIA WALALAMIKAJI.
LABDA KATIKA KUWEKANA SAWA NA MHESHIMIWA NAIBU WAZIRI.
KWANZA, binafsi nilitegemea Mhe Naibu Waziri "achukue hatua" (aliyosema sisi hatuchukui) kuwajibu na kuwaelimisha waTanzania "walalamikaji" walio nje ya nchi kupitia hizo blogu asomazo badala ya kwenda "kulalamika" kwenye gazeti. Ama angefanya vema zaidi kwa kuwa "mbunifu" na kuanzisha tovuti ama blogu ya Wizara yake itakayoeleza kwa ufasaha mambo mbalimbali kuhusiana na nafasi za uwekezaji zilizopo nchini.
PILI, tunatambua kuwa Tanzania kuna blogs nyiingi sana. Na kuna ambazo zipo makini kwenye kuandika matatizo mbalimbali na kisha kuona umuhimu wa kuweka suluhisho. Na hufanya hivyo.
Kisha zipo blogu za taswira ambazo huweka picha na "taarifa rejeo" ambazo zinabandikwa kama zilivyo na mara nyingi hakuna suluhisho linalotolewa. Kibaya zaidi ni kuwa wachangiaji wengi huwa ni "anonymous" ambao husema lolote watakalo hata kama haliifai jamii. NINAZIDI KUAMINI KUWA MHESHIMIWA WAZIRI ANASOMA HIZI. Na anadhani ndizo ziwakilishazo blogu za waTanzania. NA HILI LINASIKITISHA
Lakini MARADHI haya ya KUTOPENDA KUSOMA si ya sasa na ni kitu kibaya kuona kuwa yanamung'unya mpaka wanaotakiwa kutufanyia maamuzi yatakayojadili na kutabiri mustakabali wetu.
Naibu Waziri AMEDHIHIRISHA kuwa kwa mtazamo wake, kusaidia si kuelimisha, bali ni kutoa pesa. Yaani anaona sisi tunaoelimisha jamii ili iweze kujikomboa na kujitegemea TUNALALAMIKA NA HATUFANYI LA MAANA zaidi ya wale wanaotoa ajira za muda mfupi (na wakati mwingine za kudhalilisha). Labda wawekezaji ni wale wajao nyumbani wakafanya harusi za mamilioni na kualika vikundi vya ngoma kucheza na kuwalipa (japo kwa usiku mmoja).
Kama Naibu Waziri anasoma blogu za picha, maoni ya ma-anon na kudhani kila aandikaye "Mdau-US" ama "Mdau-UK" ni mtu aliye nje ya nchi, namshauri afanye uchunguzi kabla hajasema.
LAKINI HAKUNA LA KUSHANGAZA. Kwani analofanya Naibu Waziri ni kukwepa umuhimu wa utekelezaji wa majukumu yake. Wengi twajua kuwa kwa wanasiasa, mambo mengi hutafsiriwa tofauti. Kwa hiyo "kulalamika" anakokuzungumzia kwaweza kuwa kwa namna nyingi na kwa kuwa anataka kukimbia ukweli kuhusu mahitaji na suluhisho la matatizo linaloelezwa na wananchi, sitashangaa kusema nasi twalalamika.
MIFANO.
LAWAMA za wananchi mbele ya watawala wetu, ni ukweli wa uhitaji wa wananchi
Wananchi "wamelalamika"
juu ya uwezo wa mTanzania (anayestahili kuwa wa kawaida) kufanya harusi ya mamilioni ya pesa ilhali shule (za mahala atokako na anapoeleza kupajali) hazina hata madawati na zenye madawati hazina lolote la kuwafanya wanafunzi"watamani" kwenda, kuwepo ama hata kuifikiria shule. Mazingira ni hafifu na hatari.
Wananchi wamelalamika na hata blogu hii "imelalamika" na kuandika kuhusu huduma mbaya za afya hasa kwa kinamama na watoto
Wananchi wamelalamika na blogu hii "ikalalamika" kuhusu maji yenye sumu yanayomwagwa kwenye vyanzo vywa maji ya kunywa kama haya yaliyoonekana kutiririka katika Mto Mzinga huko Mbagala
Wananchi wamelalamika na blogu hii "ikalalamika" kuhusu hali mbaya ya uchumi Wananchi wamelalamika na blogu hii "ikalalamika" kuhusu mgao wa umeme
Wananchi wamelalamika na blogu hii "ikalalamika" kuhusu nyongeza ya mishahara ya wabunge Wananchi wamelalamika na blogu hii "ikalalamika" kuhusu wazee wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutolipwa pesa zao kwa miaka 33, ilhali bunge lilivunjwa Julai na mamilioni ya pesa yakawa kwenye akaunti Agosti. Labda mambo ambayo Mhe Naibu Waziri amesahau ni kuwa ALITAKIWA KUANZA KAZI KWA KUTUELEZA ATAFANYA NINI, VIPI, LINI NA MATOKEO YATAKUWA NINI. Huo ni kati ya UBUNIFU ambao tulitaraji toka kwake
Tulitaraji Mhe Naibu Waziri asiwe mbunifu katika kulalamikia walalamikaji wasio wabunifu, bali atueleze (kama Naibu Waziri wa Seriali ya Muungano)
-Ni vipi atafufua viwanda vinavyokufa nchini.
-Ni vipi bidhaa zinazozalishwa na VIWANDA VYA TANZANIA vitaweza kukidhi UBORA WA KIMATAIFA na kukabilianba na GHARAMA ZA UENDESHAJI iwapo gharama za umeme ndio hizo zinapaa kwa zaidi ya asilimia 10?
-Ni vipi atahakikisha uhakika wa "rasilimali" kwa viwanda na biashara za nyumbani?
-Ni vipi wale waishio karibu na viwanda vikubwa watanufaika na uwekezaji wa mabepari hao
-Ni vipi atahakikisha vibarua wa awali katika viwanda na biashara ni wale ambao wanaishi mazingira ya kuzunguka viwanda na Biashara hizo
-Ni vipi wanaoishi karibu na mazingira ya viwanda na biashara wataboreshewa makazi yao badala ya kumwagiwa sumu toka viwandani
-Ni vipi rasilimali muhimu kama maji adimu kwa wananchi hazitatumika kupoza mitambo ya viwanda na kuwafanya wananchi wakose maji

Licha ya yote, na tofauti na yeye, bado twaendelea kupongeza, kufarijika na kushawishika na mchakato wa Mhe Naibu Waziri katika kuboresha maisha ya wakaazi wa jimbo lake la Singida Kaskazini kwa kampeni yake aliyoanzisha ya OPERESHENI ONDOA TEMBE.

Photo Credit: Mpoki Bukuku.
Labda nimalizie kwa kukumbusha yale ambayo nilishaandika kwenye bandiko langu la UJINGA WA KUKIMBIA MIDAHALO, ambapo nilimnukuu Lucky Dube akisema "We are the soldiers for righteousness. And we are not sent here by the politicians you drink with. We' re sent by the poor. We' re sent by the suffering. We' re sent by the oppressed"
Ni ukweli huo ambao twauona na kuusimamia sasa. Ni ukweli huo tutakaoutumia kuwawajibisha waheshimiwa mliongia madarakani na naamini hakuna ubishi kuwa KWA KILA JEMA MTAKALOTENDA TUTAWAPONGEZA NA KWA KILA BAYA MTAKALOTENDA TUTAWAKOSOA. Nasema KUKOSOA na sio KULALAMIKA.
Na naamini kukosoa kwa kutoa sehemu ya suluhisho NI UBUNIFU

8 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Nyalandu ni mlevi wa kawaida na fisadi asiyeona kesho. Wengi wangetaka aeleze alipopata zaidi ya shilingi 60,000,000 alizotumia kwenye harusi mbali na nyingine nyingi alizotumia kukodisha helkopta aliyotumia kwenye kampeni za ubunge.
Nani hajui kuwa Nyalandu kafika hapo alipo akikufuru kutokana na kujikomba kwa Salma Kikwete na Ridhiwani? Hana tofauti na kina Salva Rweyemamu, Tambwe Hiza, Salum Msabaha na waramba viatu wengine wanaonona kwa kula makombo ya mafisadi.
Nyalandu anajulikana anavyobeba na Mohamed Dewji na mafisadi wengine wakiongozwa na baba yao anayejulikana. Hana lolote la maana zaidi ya kuja kuadhirika. Mie aliniudhi alivyotoa hitimisho la jumla kuwa tunaoishi ughaibuni ni walalamishi tu.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Nyalandu ni mlevi wa kawaida na fisadi asiyeona kesho. Wengi wangetaka aeleze alipopata zaidi ya shilingi 60,000,000 alizotumia kwenye harusi mbali na nyingine nyingi alizotumia kukodisha helkopta aliyotumia kwenye kampeni za ubunge.
Nani hajui kuwa Nyalandu kafika hapo alipo akikufuru kutokana na kujikomba kwa Salma Kikwete na Ridhiwani? Hana tofauti na kina Salva Rweyemamu, Tambwe Hiza, Salum Msabaha na waramba viatu wengine wanaonona kwa kula makombo ya mafisadi.
Nyalandu anajulikana anavyobeba na Mohamed Dewji na mafisadi wengine wakiongozwa na baba yao anayejulikana. Hana lolote la maana zaidi ya kuja kuadhirika. Mie aliniudhi alivyotoa hitimisho la jumla kuwa tunaoishi ughaibuni ni walalamishi tu.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Nyalandu ni mlevi wa kawaida na fisadi asiyeona kesho. Wengi wangetaka aeleze alipopata zaidi ya shilingi 60,000,000 alizotumia kwenye harusi mbali na nyingine nyingi alizotumia kukodisha helkopta aliyotumia kwenye kampeni za ubunge.
Nani hajui kuwa Nyalandu kafika hapo alipo akikufuru kutokana na kujikomba kwa Salma Kikwete na Ridhiwani? Hana tofauti na kina Salva Rweyemamu, Tambwe Hiza, Salum Msabaha na waramba viatu wengine wanaonona kwa kula makombo ya mafisadi.
Nyalandu anajulikana anavyobeba na Mohamed Dewji na mafisadi wengine wakiongozwa na baba yao anayejulikana. Hana lolote la maana zaidi ya kuja kuadhirika. Mie aliniudhi alivyotoa hitimisho la jumla kuwa tunaoishi ughaibuni ni walalamishi tu.

Unknown said...

Mimi napendekeza mheshimiwa Nyalandu kama unasoma hii blog basi jibu hizo shutuma za kaka NN Mhango kwani fununu tumezisikia muda mrefu sana...

emu-three said...

Mhh mwenye aone na mwenye masikio asikie, ...tuanzie wapi, aliuliza jamaa aliemaliza kubeba maboksi nje, kaja na kimtaji chake, anakuta shida ya umeme, barabara mbovu, leseni ya biashara kuipata shida, kukomboa mali yake bandarini ...alijuta, naa kubaki kuulizia nianzie wapi!

Yasinta Ngonyani said...

Mwisho mtu unashindwa cha kusema maana mmmm, Kaazi kwelikweli!!

Anonymous said...

kama kweli wanataka sisi watanzania tuwekeze basi watusikilize malalamiko yetu kisha tunaweza kuwekeza la sivyo,tunabakia kuwa watazamaji tu,kuna msemo unasemwa ukiona muhindi(gabacholi)anafurahia sehemu hiyo ujue hakuna kulipa kodi za kweli,naam kodi zinazolipwa ni za kifisadi na ndio maana leo ukitaka kushindana na wengine watakumaliza hata kabla ujaanza,rushwa,umimi,ukosefu wa haki za msingim,kabla jalalamikia watanzania walioko nje hao walioko ndani wanawasaidia vipi?mbona unapigia mbuzi gita wakati tuko mbali walio karibu unashindwa kuwasaidia?hawa ndio wale mawaziri au manaibu wanaoishia ktk mashindano ya umiss na kila kukicha hakuna jipya

BC said...

Hii bila shaka ni changamoto ya uhakika na ya aina yake kwa Mh.Nyalandu.Kama ni kweli anasoma blogs kama alivyokaririwa,basi ujumbe huu utakuwa umemfikia.

Najua hawezi kujitokeza kujibu.Viongozi wetu hawana utaratibu huo.Ni waheshimiwa sana kujibu hoja za wananchi.Ni hadithi ya watwana na watumwa.Yote tisa,ujumbe umefika.Contradiction ni ya wazi...mazingira yanayoandaliwa Vs mazingira yaliyo tayari!