Wednesday, January 5, 2011

Twaisema kwa kuwa ipo ama ipo kwa kuwa twaisema?

Mkurugenzi Mkuu mpya wa Taasisi ya Magonjwa ya Binadamu Dk Mwelecele Malecela.
Photo Credit:
Michuzi Blog
Jana nilikuwa narejea kusoma habari mbalimbali katika blogu na tovuti mbalimbali, kisha nikakutana na habari hii ya Mhe Rais Kikwete kumteua Dr Mwele Malecela kuwa mkuu wa NIMR.
Nilishaisoma hivyo haikuwa na utofauti na awali, lakini wakati nasoma nilikuwa na RAFIKI (namwita rafiki kwa kuwa sina uadui naye) ambaye alikuwa akilalamika kuwa "wenye vyeo wanaendelea kupeana vyeo zaidi". Nami nikabaki kimya nikitafakari kabla sijasema. Lakini kwa kuwa alikuwa akizungumza nami, nikaishia kumuuliza kinachomfanya aamini Dr Malecela hastahili cheo hicho, naye alikuwa na sababu nyingi za "kuhalalisha" aaminicho.
Hilo likaisha.
Nikakumbuka kuwa ni yeye ambaye tuliwahi kuwa na mazungumzo na akawa anazungumza namna ambavyo "wenye nacho ndio wanaoshinda bahati nasibu kubwa hapa nchini". Na ni wengi wanaamini hivyo kwani kuna aina ya kile kiaminiko kuwa ukweli katika hilo. Kwake yeye, msemo MWENYE NACHO HUONGEZEWA una maana zaidi ya nilivyodhani mimi. Nikakumbuka kuwa katika suala la watu kushinda bahati nasibu nilimuliza swali kuwa "hapo ulipo una dola ngapi?' naye akajibu kiasi alichonacho, kisha nikamuuliza kama anaweza kutumia kiaso hicho chote kununua tiketi ya bahati nasibu akanijibu "nimerogwa?" Nikamwambia kuwa "labda ndio maana watu wasio na kipato hawashindi kwani wenye nacho wanatumia pesa nyingi na pengine kwa miaka kadhaa bila kukata tamaa mpaka washinde ilhali wasio nacho wanapanga bajeti ya kila senti na ndio maana hawashiriki saana bahati nasibu. Na unavyozidi kushiriki ndivyo unavyojiongezea nafasi ya ushindi". TUKAELEWANA.
Lakini ninalowaza hapa ni kuwa... kwa mtazamo ama maongezi ya awali na ya karibuni yangu na "rafiki" yangu huyu, unadhani MWENYE NACHO HUONGEZEWA ama KWA KUTUMIA ALICHONACHO ANAYATAMBUA MAZINGIRA MAZURI YA KUONGEZEWA NA KUJITAYARISHA?
Ni kweli na haki kwa mhitaji kuendelea kujididimiza na kuonekana kukata tamaa kwa kuwa anaamini mwingine "amepata zaidi"?
Nikakumbuka aliyoandika Kakangu Shaaban Kaluse akieleza na kuuliza UMASKINI SAWA, LAKINI KWANINI TUWACHUKIE WALIOFANIKIWA? (mrejee hapa) ambapo alilielezea hili kwa ukubwa zaidi.
Lakini nikawaza mengi kuhusu kauli za RAFIKI huyu. Kauli kama "mwenye nacho huongezewa" ilhali natambua kuwa kuna zipinganazo nazo.
Kwani asemaye KAWIA UFIKE ndiye atakeyesema NGOJA NGOJA UTAKUTA MWANA SI WAKO?
Ama asemaye "haraka haraka haina baraka" unaamini ndiye atakayesema "ujanja kuwahi"?
Labda misemo imewekwa kukidhi kile tupangacho ama kudhania, lakini kuamini kuwa misemo fulani itadhihirisha ama kuhalalisha kile tusemacho, ndipo ninapowaza hapa.
Labda nami natakiwa kujiwazisha kama kusema "namna nionavyo tatizo ndilo tatizo" maana yaweza kuwa "funiko" la mawazo yangu.
Lakini nikirejea kwenye "chanzo" cha bandiko hili, yawezekana tunatumia misemo fulani ILIYOPO kujiridhisha kuwa HATUENDELEI KWA KUWA HATUKUWA AMA HATUNACHO, ilhali ipo misemo itupayo moyo kama MGAAGAA NA UPWA........
Ndipo hapa ninapokuja kuuliza kuwa misemo tuitumiayo ni katika kujitengenezea mazingira kwa kuwa ipo / ilikuwepo ama misemo hii ilikuwepo / ipo kwa kuwa twahitaji kuisema?
Dr Mwele (ambaye hatufahamiani na siamini kama anatambua kuwa kuna kiumbe kinachoitwa Mubelwa Bandio na ambaye "kukutana naye ni nisomapo maoni yake kwenye posts za marafiki zangu Facebook na nilipomsikia VOA kwenye kipindi cha Afya cha Da Mkamiti Kibayasi) amesoma na ameongoza taasisi kadhaa ikiwemo hiyo inayojishughulisha na mambo ya Matende, na pengine kutokana na "mazingira mazuri ya kuongezewa" aliyotayarishiwa, amekuwa katika nafasi nzuri ya kukwaa nafasi hiyo. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Desemba 31, 2010 imesema (na hapa nainukuu) "Dk. Malecela ambaye ni Mtafiti Kiongozi amekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa NIMR tangu Juni, 2009. Kabla ya kukaimu nafasi hiyo, Dk. Malecela alikuwa Mkurugenzi wa Uratibu na Kukuza Utafiti katika Taasisi hiyo.
Mkurugenzi huyo mpya ana Shahada ya juu ya Uzamivu ya Vimelea vya Magonjwa ya Binadamu katika fani ya Matende na Mabusha kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza na ameitumikia NIMR kwa miaka 23 sasa, tangu alipoajiriwa akiwa Mtafiti Mchanga katika Kituo cha Utafiti cha Amani.
Dk. Malecela pia amewahi kuwa Rais wa Mpango wa Kimataifa wa kutokomeza ugonjwa wa Matende na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Mpango huo."

Lakini hata kabla ya taarifa hii na uteuzi huu, niliwahi kumsoma Dr Mwele alipokuwa akieleza namna alivyotimiza ndoto zake kimasomo na kikazi alipozungumza na gazeti la Mwananchi ambapo alieleza namna ambavyo ALIWEKEZA JUHUDI ZA HALI YA JUU kuweza kufika hapo alipo (rejea HAPA)
Na kama maswali yangu yanaweza kuwa magumu kujibu juu ya NAMNA TUNAVYOWEZA KULAZIMISHA MISEMO KUTUFAA KWA KILE TUFIKIRIACHO, BASI (kabla hujaweka maoni) TEMBELEA UKURASA HUU WA KIBARAZA CHA AWALI CHA DA SUBI (hapa) USOME MISEMO NA METHALI ZA KIWETU KISHA UONE NI NGAPI ZAPINGANA, NA NI IPI KATI YA HIZO YAWEZA KUKUFAA KUTAFSIRI KILE USEMACHO
Labda wote hatuko sahihi kwa kuwa sote tuko sahihi
Lakini kutambua kuwa "mwaka mpya" wastahili kuanza kwa kuyafikiria mambo kwa mtazamo chanya na kutumia changamoto kujenga nafasi zetu......NI JAMBO JEMA

Naacha...Tuonane "NEXT IJAYO"

3 comments:

emu-three said...

Imekaa vyema hii mkuu, mwaka mpya kwa kutizama msimamo CHANYA, yawezekana hiyo, kwani hasi na hasi zinakuwa chanya au sio, lakini hasi na chanya inategemea ipi kubwa.
Ni wazo tu mkuu!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kachaguliwa kwa sababu ya sanamu au uwezo wake?

kwani wewe ni sawa ni ridhwani? hata kwako mwombeki siyo sawa na paulina au siyo?

Anonymous said...

Pamoja najina....huyu dada jamani kaifanyia kazi hiyo post...nakumbuka me niko shule ya msingi huyu dada anachakarika UDSM...pyuuu...hapa kwa kweli...waswahili tuongee tu...ila haki yake hiii...anastahili....kama yupo