Wednesday, March 2, 2011

Tanzania yangu..."Inayokazana" kuona ilhali imefumba macho

Katika wimbo wa Lady Jay Dee aliouita WANAUME KAMA MABINTI, mshirikishwa wa wimbo huo Hamis Mwinjuma ama MwanaFA aliimba ubeti akisema "nataka mwache kutazama, ninataka muone...sizuii msifanye mfanyayo, tunafikiri kwa ubongo sio kwa nyayo"
UANAUME WA KIKE kwa tafsiri niipatayo hapa ni ile hali ya kuwa Fulani lakini ukajitahidi kuwa tabia tofauti. Ama kuhitajika / kutegemewa kufanya jambo moja ukajikuta wafanya kinyume chake. Na mambo mengine yanayofanyika wala si ya kuhitaji akili saaaana, ni ya liyo wazi ambayo kama MwanaFA alivyoonyesha kisanii, kasema "..kufahamu hii ni 'simpo' zaidi ya kumyatia kiziwi...."
Leo hii naitazama Tanzania ambayo INAJARIBU KUPIGA HATUA ZA KIMAENDELEAO BILA KUWEKEZA KATIKA ELIMU. Niliwahi kusema mara kadhaa kwamba KAMA HILI LITAFANIKIWA, BASI TUTAKUWA KWENYE MAAJABU YA DUNIA.
Lakini pia kuna upande mwingine wa MAENDELEO ambao twaiona Tanzania yangu ikipanga kuendelea
Kwa kuwekeza katika NIDHAMU YA MATUMIZI ilhali hatuoni punguzo la matumizi haya na hata uwajibikishwaji kwa wale walioonekana kuwa chanzo cha matumizi mabaya ya fedha za serikali / umma. Hivi karibuni niliandika kuhusu HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS KIKWETE aliyoitoa wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya akieleza meengi yaliyotokea 2010 na yanayotaraji kutokea 2011. Na moja ya mambo aliyozungumzia ni pamoja na MATUMIZI na hapa nanukuu sehemu ya hotuba yake.
"Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa nidhamu ya matumizi bado hatujapiga hatua ya kunifanya nipoe moyo, ingawaje kuna mafanikio yanayoendelea kupatikana. Niliwakumbusha Mawaziri kuhusu kuwepo Kamati za Matumizi ya Fedha katika kila Wizara, Idara za Serikali na Halmashauri za Wilaya na Miji ambazo niliagiza ziundwe miaka mitatu iliyopita. Niliwakumbusha kuwa, wakuu wa taasisi hizo ndio wanaoongoza Kamati hizo na hivyo wao ndiyo wanaoongoza Kamati za Wizara zao. Nimewataka wahakikishe kuwa Kamati hizo zinatekeleza ipasavyo majukumu yake ili rasilimali za taifa zifanye kazi iliyokusudiwa. Halikadhalika, niliwataka wahakikishe kuwa Kamati za Idara na Mashirika chini ya Wizara zao zinafanya kazi kwa ukamilifu. ."

Lakini pia ninawaza namna ambavyo tunataka kuweka NIDHAMU katika MATUMIZI YA MALI ZA SERIKALI ilhali hata uwepo wa matumizi yanayohitaji nidhamu si halali. Niliwahi kuandika kuhusu WAKUU WA MIKOA ambao niliwatambulisha kama MZIGO KWA SERIKALI NA WANANCHI na pia CHANZO CHA KUDIDIMIA KWA MAENDELEO NCHINI MWETU (irejee hapa). Naamini kwa nchi ambayo inakusanya mapato machache kuliko matumizi, kabla haijafikiria namna ya kuyadhibiti, ingefikiria namna ya KUPUNGUZA MATUMIZI YASIYO YA LAZIMA.
Vyeo kama wakuu wa mikoa na hata wakuu wa wilaya bado (kwa mtazamo wangu) naamini ni upotevu wa hela kwani wale hawana wanalowatumikia wananchi, hakuna walilowaahidi wananchi na hawana hasara yoyote kwao kutojihusisha na wananchi kwani "REVIEW" yao inatokana na namna wanavyomtumikia Rais na sio wananchi.
Na kwanini tuwe na watu hawa kisha wakurugenzi wengi kusaidia utawala?
Ila ninashangaa nini? HII NI TANZANIA YANGU....ILIYO MAARUFU KWA KUENDEKEZA WINGI WA VINGI HATA KAMA VINGI HIVYO HAVINA UFANISI WALA TIJA KWA WENGI.
Ndiooooo...Mifano ipo.
Tazama idadi ya WIZARA NA WATAWALA kisha linganisha na ufanisi wake. Majengo makubwa ya wizara, wafanyakazi lukuki lakini makabrasha ya wastaafu yanachukua miaka miwili kuyapata (licha ya kwamba wamearifiwa kuwa muda wao wa kustaafu umefika)
Tazama idadi ya MAKAMPUNI / MASHIRIKA YANAYOLIPWA KWA "UZALISHAJI UMEME" (Tanesco, Richmond, Dowans, Songas) kisha linganisha na idadi ya watumiaji umeme na muda wanaokuwa na umeme.
Tazama idadi ya blogu na linganisha na maudhui ya kumsaidia ama kumkomboa mTanzania halisi kulingana na mahitaji yao.
Tazama idadi ya "SHULE ZA KATA" kisha linganisha na hicho kiitwacho ELIMU inayotoka hapo.
Tazama idadi ya AHADI ZA MHE. RAISI tangu mwaka 2005 kisha linganisha na utekelezwaji wake...
NINALOWAZA hapa ni kuwa, kwanini bado tunaamini kuwa tunaweza kupata maendeleo kwa kuendekeza na kuendeleza fikra na matendo ambayo ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipo?
Kwanini tuendelee kuamini kuwa WATAWALA waliosababisha uozo tulionao ndio watakaotukwamua toka hapa?
Kwanini tuendelee kuumbatia mfumo wa upeanaji madaraka ambao unapmpitisha mgombea kwenye njia zinazojeruhi utu na fikra zake kiasi kwamba anapofikia hatua ya kutawala anakuwa kama "walimu" wake waliomtangulia?
HUKU NDIKO "KUKAZANA KUONA ILHALI TUMEFUMBA MACHO".
Ni wakati wa kufumbua macho na kwa waliofumbua basi WAACHE KUTAZAMA BALI WAONE. Ni wakati ambao JAMII lazima ikwepe dhana za kizamani ambazo zimewafanya waweke tumaini kwa watu ambao wanatumia tumaini hilo kuwanyonya na kuwadidimza.
Ni wakati ambao sipendi kuona watu wakipigana, wala wakiuana, bali WAKIWAJIBISHANA NA KUTIMUANA. Na kuwa na HESHIMA KWA KATIBA na wakati ambao hata wale waliovunja katiba wasiitumie katiba hiyohiyo kujilinda.
NI WAKATI WA KUWAFUMBUA WATU MACHO ILI NAO WAAMKE (KAMA KWINGINE) NA KUWAWEZA KUONA.
Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

4 comments:

Christian Ishengoma said...

Habari yako mzeewa changamoto. Ahsante kwa kuanzisha blog hii inayotoa changamoto kwetu Watanzania,nadhani ingekuwa vizuri sana wananchi wangeweza kusoma ujumbe huu. Kila la kheri katika kuleta changamoto ambayo ni chachu ya mabadiliko chanya kwa nchi yetu.

emu-three said...

Kama aivyosema Chistian, kuwa kama Watanzania wengi wangelifanikiwa kupitia hapa kwenye hii blog wakapata haya mambo, ambayo ni changamoto,tungelifunguka macho , tukaona, kuliko kutembea kama vipofu ilihali macho tunayo

Unknown said...

Ni hivi kaka:

Imenifikirisha na kunifanya kuwaza jinsi KIPOFU ALIYEPEWA TOCHI AITUMIE WAKATI WA GIZA.

...nimeongeza wazo kifikra kwa kuendeleza Changamoto hii HAPA: http://mtayarishaji.blogspot.com/2011/03/kipofu-aliyepewa-tochi-aitumie-wakati.html

KWA MWENDO HUU IPO SIKU TUTAKAZANA ILIHALI TUMEFUMBUA MACHO!!

Godwin Habib Meghji said...

Sina uhakika ni watanzania wangapi wanasoma machapisho yako. Najua wengi wanapenda blog fulani za picha na habari za juu juu
Kazi nzuri endelea kuandika