Tuesday, October 25, 2011

Kwa kuwa amekufa alivyokufa...........

Moammar Gadhafi akiwahutubia wale waliokuwa wakimuunga mkono mjini Tripoli Libya Machi 2, 2011.
Photo Credits: ABCNEWS.COM
Kama kuna jina moja (licha ya matamshi mengi) lililotawala vichwa vya habari katika siku za karibuni ni la kiongozi wa zamani wa nchi ya Libya, Moammar Gadhafi. Na kama ambavyo imeripotiwa kwa vichwa na maelezo tofauti, kiongozi huyu ameuawa na sasa nchi ya Libya yasemekana kuwa "huru".Utawala wa Gadhafi ulikuwa kati ya tawala kongwe zilizopo sasa (miaka 42) na anguko lake limeigawa dunia katika kilichotendea, kilivyotendeka na pengine kitakachofuata. Wapo wanaounga mkono yote matatu, wapo wanaounga mkono moja ama mawili kati ya hayo na wengine wapingao yote.
MAJIBU PEKEE YAKO KATIKA FUMBO MOJA TU....MUDA.
Ni muda pekee utakaoamua ama kuonyesha ama kudhihirisha kama kila kilichosemwa kuhusu Gadhaffi kilikuwa na ukweli.
Ni muda pekee utakaobainisha kuhusu Falsafa zake, imani yake alivyokuwa akiizungumzia, "uroho wake wa madaraka", "upendo" na / ama "ukatili" wake kwa nchi na wananchi wake, nia yake ama kauli za kuiunganisha Afrika na kadhalika.
Ni muda pekee utakaopima UONGO NA UKWELI wa propaganda za wamuungao mkono na wampingao.
Kwa muda wote wa "mlipuko" wa taarifa na habari za kifo chake, kumekuwa na machache ya kuangalia kijacho, na pengine mimi nawe tutembee pamoja kuangalia hili.....
Kwa kuwa amekufa alivyokufa, basi ameacha funzo kwa wengi kuwa YAWEZEKANA. Sina hakina ni wangapi wa wasomaji wangu waliamini kuwa ipo siku ambayo mtu kama Gadhafi atajificha kwenye "karavati" la maji machafu ili kujikinga ama kuulinda usalama na uhai wake? Lakini tumeona hivi karibuni. Na hakika kifo chake kimeongeza "chachu" ya "msako wa uhuru na demokrasia" katika nchi nyingine. Kwa hiyo kifo chake kimekuwa funzo kwa wengine kuwa wanaweza kuanguka, na wengine kuwa wanaweza kuangusha.
Mahala ambapo palitajwa kama maficvho ya mwisho ya Moamar Gadhafi
Kwa kuwa amekufa alivyokufa, wapo watakaopata ujasiri wa kuthubutu zaidi ya kuuangusha utawala. Wapo watakaopata ujasiri wa kukosoa kila kifanywacho na tawala zilizo madarakani kwa muda mrefu. Wapo watakaopata ujasiri wa kuamini kuwa MABADILIKO yako mikononi mwao na wanachohitaji ni nia na pengine "msaada mwema" wa kuwawezesha kufanikisha hilo.
Kwa kuwa amekufa alivyokufa, wapo wanaoona ama watakaoona ushujaa wake. Tayari baadhi ya watu mashuhuri duniani wameanza kupinga hadharani kifo cha Gadhafi na kuonya juu ya kitakachofuata. Kiongozi wa Nation of Islam, Louis Farrakhan amelaani mauaji hayo alipohojiwa na na mtangazaji wa kituo cha WVON-AM Chicago, Cliff Kelley na kusisitiza kuwa “Gadhafi died in honor, fighting for the Libya that he believed in.”
Mtumishi Louis Farakhan akizungumza kwenye kipindi cha redio siku ya jumanne Oktoba 25 ambapo alilaani mauaji ya Gadhafi..
Photo Credits: Chicagotribune.com
Kwa kuwa amekufa alivyokufa, wapo watakaotajirika tena kutoka nchi ambazo hazina mahusiano ya moja kwa moja na mwananchi wa Libya. Nazungumzia watunzi wa vitabu, filamu, waandishi wa historia ya Gadhafi, wachambuzi wa makala mbalimbali (ambao nao hulipwa pesa nono kwa hilo) na wengine wengi. Si tu kwa kuwa amekufa, lakini kwa kuwa amekufa kwa namna alivyokufa na kuanza KUPAMBANISHA historia na mustakabali wa waLibya na Libya kwa ujumla.
Kwa kuwa amekufa alivyokufa, wapo ambao kwa mara ya kwanza watatamani kusoma kitabu chake na kujua alikuwa na lipi jipya (kama lipo) linaloweza kuakisi fikra zake, falsafa zake, na pengine hata kunyambua alilokuwa akipanga kufanya iwapo wote wangeamini katika kitabu hicho cha kijani.
Miaka miwili iliyopita, Gadhafi alifanya mahojiano na Fareed Zacharia wa CNN, na alikuwa na HAYA ya kusema


Kwa kuwa amekufa alivyokufa, tayari kutakuwa na biashara halali na haramu kuhusu yeye, kifo chake na hata kitakachofuata. Tunajua alivyokuwa na misimamo (ambayo si yote ilikuwa mizuri akama ambavyo si yote ilikuwa mibaya), na naamini kuwa kati ya wale watakaofurahia kifo chake ni wale waliokuwa "wamewekewa kauzibe" hasa katika suala la rasilimani.
Kwa kuwa amekufa alivyokufa, wapo watakaoneemeka. Wale ambao watataka kuaminika kuwa NDIO WAKOMBOZI HASA WA NCHI. Wale ambao wanaamini kuwa wanastahili kuwa na madaraka kwa kuwa hakuna mwingine anayeweza KUIKOMBOA NA KUIJENGA LIBYA MPYA ZAIDI YAO. Kifo chake kimekuwa MTAJI wa wengi. Wanaoonyesha kuwa WALIDHAMIRIA NA KUWEZA na kuwa sasa ni wakati wa kutumia nafasi waliyoitengeneza "kusawazisha mambo".Lakini hili halitotokea bila wengine kutaabika. Haimaanishi kuwa wakati wa Gadhafi hakuna aliyetaabika, lakini kama lengo la kumuondoa lilikuwa kuondoa taabu ka ahizo, basi lengo hilo halitakuwa limetimia iwapo watu zaidi watandelea kutaabika. Na wazo la taabu hizi linakuja kutokana na ukweli kuwa (kwa mujibu wa vyomb nukuliwa vya habari vinavyomtangaza Gadhafi kama dikteta) vinaonyesha wazi kuwa hakuna aliyekuwa na madaraka zaidi yake. Kwa maana nyingine hakuna aliyekuwa na uzoefu wa utawala WA LIBYA zaii yake. Tuwaombee maana hili si dogo.
Kwa kuwa amekufa alivyokufa, wapo pia watakaodhihirisha UNAFIKI wao. Ambao wataunga mkono baada ya kuondoka na hata wanaoonekana kupinga kifo chake kwa sababu zisizo na maana.
Gadhafi HAJAFA SANA kuliko wengine anaoshutumiwa kuwaua, na japo yawezekana hajateseka kama wale wanaosemekana kuuliwa na majeshi yake, bado ukweli unabaki kuwa naye amekufa / ameuawa.
Na najua kuwa MENGI YATATOKEA sio tu kwa kuwa amekufa ama kuuawa, bali KWA KUWA AMEKUFA ALIVYOKUFA.
Na huu ni Mtazamo kwa namna nionavyo tatizo. Labda namna nionavyo tatizo ndio tatizo.

2 comments:

Unknown said...

Hapana chako na changu, hivi vyote ni shirika

Mimi wako wewe wangu, kipi cha kugawanyika?

Kuungana walimwengu, si neno lenye mwafaka,

Halipendezi kwa Mungu, pamoja na malaika

Kukwambia nenda zangu, sithubutu kutamka,

Na kadhalika mwenzangu, sidhani hilo wataka,

"Hutaki" lina uchungu, na kwangu ni kadhalika.

Dunia ina mizungu, nikwambiayo kumbuka.

Nakuachia swali.

Mzee wa Changamoto said...

Duh!!!!
Kaka Mcharia NAOMBA NIKUPE MJI utufumbulie hilooo swali. Maana nimewaza kwa sauti na kimyakimya sijaweza kuapata jibu.
Dadaa wajina wa Mwana (Dada Paulina). Umeweka zaidi ya bayana. nimeipenda hiyo. Tusubiri kuona itakavyokuwa.
"Mube yangu macho"......
BARAKA KWENU NYOTE