Sunday, November 20, 2011

Labda hatuendelei kwa kuwa "wa kutuendelesha" hayuko kwenye "kiendelesheo" chetu

MAREJEO YA FEB. 3, 2011
Photo Credits:Jimmy Falon Blog
Natambuwa kuwa TUNA TAFSIRI TOFAUTI ya neno ama kitu MAENDELEO. Lakini haijalishi unatafsiri vipi, tutakubaliana kuwa SI KILA MABADILIKO NI MAENDELEO JAPO KILA MAENDELEO NI MABADILIKO.
Na kwa sehemu yoyote iliyo na maendeleo, utagundua kuwa ni wachache wafanyao maamuzi yanayoleta maendeleo hayo na ambao wakati mwingine wakati wafanyapo haya, hupuuzwa (kwa kuwa wengi wetu husita kubadilika). Kwa maana nyingine ni kuwa kwa maendeleo yoyote kufanyika, ni lazima wale wachache (ambao mara nyingi wamepewa ama kujipa dhamana) wanatakiwa kuwa makini katika kufanya maamuzi yao kwa manufaa ya nchi na wananchi.
Hawa (wafanya maamuzi) wanapokuwa na mtazamo mwingine, wanapokuwa wanawaza vingine, wanapojiweka katika ngazi ama hatua nyingine na wale wanaostahili kuwa nao, hawawezi kufanya maamuzi yawafaao kwa kuwa HAWANA MAHITAJI YAFANANANYO NAO. Kwa hiyo maendeleo kwao ni tofauti na maendeleo kwa wawaongozao.
Na ni hapo tunapokuja kuona mifano kadhaa.
1: Maendeleo yetu ni pamoja na KUTHAMINIWA.
Lakini tunaona namna ambavyo thamani ya mTanzania inavyokuwa kulingana na uajiri alionao, ama mahusiano kati yake na wakubwa mahala fulani. Hivi majuzi tumesikia habari ya WATOTO KUMI WALIOUKULIWA KWENYE SHIMO LA TAKATAKA huko Mwananyamala. Hiki kitendo kilitakiwa kupingwa na kufanyiwa uchunguzi wa hali ya juu. Hawa watoto hawakutendewa haki (hata kama walizaliwa wakiwa wafu) kwani kama viumbe na kama waTanzania, bado walikuwa na haki ya kupata HESHIMA ZOTE ZA MWISHO na kuzikwa kulingana na mila, desturi na imani za asili waliyorithi. Lakini hakuna aliyesikika akionekana kuwekeza ktika KUWAJIBISHA WATAKAOBAINIKA KUTENDA KITENDO HIKI CHA FEDHEHA.
Hawa walikuwa na bado ni waTanzania. Hazikuwa TAKWIMU. Hivi majuzi walipouawa watu Arizona tuliona Rais wa Marekani akienda kufariji.. Labda Rais wetu alikuwa "busy", lakini ni lini wanaotenda makosa kama haya wamewajibishwa?
Labda "waendeleshaji" wetu hawako kwenye "kiendelesheo" cha UTU NA THAMANI YA MTANZANIA kwani wangekuwa huko, wangemtafuta mhusika na kumuadhibu. HAWA WATOTO HAWAKUJIZIKA.
2: ADHA YA MIUNDOMBINU
Hakuna ubishi kwamba viongozi (ama niseme WATAWALA) hawatumii aina ya miundombinu tunayotumia sisi. Niliwahi kuandika kuhusu BARABARA ZETU (irejee hapa) , na mara kadhaa nimezungumzia suala la AJALI (rejea hapa). Haya yote licha ya kuwa yanachangia kuondoa nguvukazi ya jamii na kuzorotesha maendeleo ya nchi, WAHUSIKA HAWAJALI kwa kuwa wao si watu walio katika mfumo wetu wa maisha. Wakati sisi "tunalia" na foleni katikati ya jiji, wao wanafikiria kuanzisha huduma za helikopta za kukodi (as if zitamfaa aliye Mbagala ama Gongo la mboto ambaye ndiye mwenye uhitaji mkubwa wa kuondokana na foleni). Hawasafiri kwa barabara tupitazo sisi kwenda vijijini na ndio maana HAWAONI UCHUNGU NA ADHA YA UBOVU WAKE.
Siamini kama WANAPATA MGAO tunaosikia kila siku kwa ndugu zetu, na ndio maana hawana "LADHA HALISI" ya tatizo la kukatika kwa umeme. Hawatumii "line" za maji tutumiazo sisi, na ndio maana mabomba yao yakitoa maji masaa 24, hawajui kuwa kuna yanayomaliza miezi (kama sio miaka) bila kupitisha unyevu ndani mwake.
NI KWA KUWA HAWAKO KWENYE MIUNDOMBINU YETU, HAWAJUI ADHA ZETU.
3: ADHA YA HUDUMA ZA JAMII
Labda wangekuwa wanatibiwa atibiwako bibi yangu, ama kupata chakula apatapo mpwa wangu. Lada wangekuwa wanatambua adha hizi. Labda watoto wao wangesoma tuliposoma sisi wangethamini mazingira ya shule zetu, na labda wangekuwa wakikaa mahabusu wakaazo "wasingiziwa" wengine wangejua haki ya mtuhumiwa (kuwasi mkosaji mpaka atakapokutwa na hatia na mahakama)
Lakini kwa kuwa wao hupata dhamana hata kama kosa lao ni kubwa, kwa kuwa wao ksi zao huenda mwendo kasi, kwa kuwa wao hutibiwa nje, hufunga barabara waendapo vijijini, husafiri kwa ndege, husomesha nje ya chi, HAWAJUI MAHITAJI YETU KWA KUWA HAWAKO KATIKA NGAZI MOJA NASI.
Na haya ni machache ambayo yananifanya niingie katika sehemu hii ya tatu nikiwaza kuwa Labda hatuendelei kwa kuwa "wa kutuendelesha" hayupo kwenye "kiendelesheo" chetu
NAWAZA KWA SAUTI TU!!!!!!

No comments: