Thursday, January 5, 2012

Tanzania Yangu.....Na mikakati thabiti ya "kuua kilicho chake"

Mwaka 2008, Tanzania ilitajwa kama nchi ya 78 katika nchi bora za kufanya biashara ulimwenguni. Kwa mujibu wa matandao wa Forbes unaojihusisha na habari za Mapato na Biashara, takwimu zilizotolewa mwaka huo zilionesha kuwa Tanzania ilikuwa imepanda nafasi 26 toka ile iliyokuwa nayo mwaka 2007 (ya 104) na kwa mwaka huo (2008) ilikuwa nafasi moja juu ya China iliyoshuka nafasi mbili toka mwaka uliopita.
Ripoti ya mwaka 2008 ilionesha kuwa ukuaji wa viwanda, madini hasa Dhahabu, mabadiliko ya mfumo wa kibenki na uwekezaji, michango ya wahisani pamoja na sera madhubuti za uchumi ni kati ya vigezo vilivyoiweka Tanzania katika nafasi hiyo. Lakini pia miundombinu chakavu imekuwa kikwazo katika uwekezaji na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.
Mwaka uliomalizika umeshuhudia Tanzania ikishika nafasi ya 108, ikiwa ni nafasi 6 chini ya ilivyokuwa mwaka 2010. Na kwa mwaka jana, wenzetu ambao tulikuwa juu yao kwa nafasi moja mwaka 2008, (namaanisha China) sasa wanashikilia nafasi ya 82.
Botswana ndiyo nchi bora zaidi kwa biashara barani Afrika (kwa mujibu wa mtandao wa Forbes) na inashikilia nafasi ya 55 duniani. Kwa upande wa Majirani zetu, Kenya ni ya 103, Uganda ni ya 105.
Bado yaonekana kuwa nchii yangu (inayosemekana kuwa katika asilimia 10 zenye uhitaji zaidi, ama wenyewe wanaita maskini) inategemea zaidi misaada ya nje ilhali inatumia asilimia nne (4%) ya eneo lote la nchi.
Miundombinu chakavu katika kukwamua uchumi inaonekana kuwa kikwazo kingine kinachoikwamisha nchi ambayo tayari inashikilia rekodi ya kupokea fungu kubwa zaidi kutoka Millennium Challenge Compact (MCC) lenye thamani ya dola milioni 698.
LAKINI NI NANI MCHAWI WA MAENDELEO YETU?
NAWAZA.......
Hivi kama serikali (ambayo naamini ina magari mengi sana) ingeweka ulazima wa magari yote kununua matairi kwenye viwanda vya ndani kama General Tyre, VINGEKUFA? Ama watasema matairi yaliyokuwa yakitengenezwa Arusha hayakukidhi ubora wa barabara na hali ya Tanzania?Hivi kama serikali ingeweka mkakati madhubuti na kuamua kutumia magari yanayotengenezwa na kiwanda cha jeshi cha NYUMBU katika idara na ofisi zake zooote nchini, tusingepunguza uagizaji wa magari? Ama watasema MAGARI YA NYUMBU HAYAKO KATIKA KIWANGO CHA TANZANIA ukilinganisha na magari yatokayo Marekani / Japan / China?
Hivi wabunge wetu na sare zote zinazofadhiliwa / kudhaminiwa na serikali zingekuwa ni kutoka viwanda vya ndani kama URAFIKI vingekufa?
Hivi serikali ingeamua kutumia (japo asilimia kubwa ya) saruji ya nyumbani, nondo za nyumbani na mafundi wa nyumbani kujenga "vikwangua anga" vyote vya nyumbani, ajira ingekuwa katika kiwangi ilichopo?
Ni wakati ambao naamini "wenye uerevu" wa mambo watajitokeza na kunyambua mambo haya yanayoelezwa na hawa "wataalam" wa uchumi wa dunia, ama wajitokeze kuwapinga na kujenga hoja za ki-uchumi wa Tanzania na / ama Afrika na kisha kutueleza ni kwanini tupo tulipo, na ni vipi tunaweza kusonga mbele zaidi (kama kuna uwezekano).
Lakini nawaza namna tunavyoweza kusonga mbele kiuchumi ikiwa HATUTHAMINI KILICHO CHETU?
Ni vipi tutaendeleza VAZI LA TAIFA iwapo mBunge asiyevaa SUTI haonekani kuvaa kiheshima ndani ya Bunge la Tanzania? Hata suti tunasikia kuwa wazivaazo wanazitoa nje ya nchi (kama WIKILEAKS ilikuwa sahihi).
Tutawezaje kuendeleza uzalishaji wa magari ya nyumbu ikiwa yale waliyotengeneza miaka hiyo hayajapata mteja na wala kupata nafasi ya kuonyeshwa na kunadiwa (zaidi ya siku ya maigizo ya uhuru)?
Ni vipi kiwanda kama General Tyre kingeshindana na viwanda vya nje iwapo maelfu ama malaki ya magari ya serikali yanatumia matairi yaliyoagizwa nje?

LAKINI HII NDIYO TANZANIA YANGU.....INAYOONYESHA MIKAKATI THABITI YA "KUUA KILICHO CHAKE"

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

1 comment:

Rachel Siwa said...

Mungu ibariki Tanzania,Mungu tubariki wa Tanzania.