Sunday, August 12, 2012

TANZANIA YANGU....Ikimbizayo farasi kwa kobe.

Michuano ya Olimpiki imekamilika leo.
Na katika kukamilika kwake, Tanzania (kama ambavyo imefanya katika michuano 11 kati ya 12 iliyoshiriki) imeondoka bila medali. Maswali ni mengi kuhusu hili.
Wengi tunajiuliza kuhusu UMUHIMU WA KUSHIRIKI BILA MAANDALIZI YA KUTOSHA. Na pia idadi ya washiriki.
Nikumbushe nilichoandika Aug 25, 2008 baada ya kumalizika kwa michuano iliyopita.
"Michuano ya Olimpiki ndio imemalizika na pamoja na kupambwa na kupambika kwa sherehe za kufungua na kuhitimisha michuano hiyo, bado kuna maswali ambayo wapenda michezo wengi wanaendelea kujiuliza....
..... kuna ambao wanaendelea mbele zaidi kuangalia jinsi watu walivyoweza kuvunhja rekodi mbalimbali na kujiweka pamoja na kuziweka nchi zao kwenye ramani ya michezo.
Na hapo ndipo nami ninapogota, nikiangalia mafanikio ya nchi mbalimbali katika michezo mbalimbali nikarejesha mawazo hayohayo kwa nchi niipendayo na kuithamini TANZANIA, najikuta nakwazwa na maswali kadhaa.
Pengine michezo kama kuogelea itatugharimu saana maana waogeleaji wa kimataifa waliofanya vema wanawekeza gharama kubwa saana kwenye mchezo huo kuanzia chakula mpaka mazoezi. Lakini pia kuna sehemu nyingine ambazo naamini tungestahili kufanya vema kiasi.
Hivi ni kweli kwamba Tanzania hatuna wakimbiaji wazuri?
Na iweje kwa jamii kama ya Kenya ambayo tumepakana nayo na tunashabihiana kwa mambo mengi (hasa ukanda wa kaskazini upakanao nao) wanaweza kufanya vizuri katika michezo kama mbio ndefu nasi tushindwe?
Hivi ni kweli kuwa hatuna wapiganaji wenye vipaji vya kuweza kufanya vema kwenye michuano kama hii?
Vipi kuhusu walenga shabaha?
Sina takwimu lakini nakumbuka kuwa walikuwepo wenye vipaji katika nyanja nyingi za michezo (hasa mikoani nilikosomea) tena wengine wakifanya vema saaana hata katika michezo ya mashule kama Umisseta lakini wanapomaliza shule hakuna utaratibu mpango mahususi wa kuwaonesha njia kuelekea kwenye mafanikio na ndio maana wanaishia kuacha kushiriki michezo na kujiingiza kwenye kazi za kusukuma siku kama uvuvi, ukulima na muda mfupi baadae kwenye ujenzi wa familia.
Kwangu mimi nadhani kuna pengo kubwa kati ya serikali, jamii na michezo.
Kwa SERIKALI utoweka thamani halisi ya michezo na hata kutoitengenezea njia sahihi ya kuwawezesha wale wenye vipaji halisi waweze kujikita huko na kujiajiri kwa manufaa yao, familia zao na taifa kwa ujumla.
Pia JAMII lazima itambue kuwa namna nyingine ya kujiajiri katika michezo ni kupitia elimu."
Mwaka jana nilipata fursa ya kuhojiana na Ndg. Richard Kasesela kuhusu suala hili la Michezo na zaidi kuhusu Olimpiki na hili ndilo alilosema HAPA
Ninalowaza hapa ni kuwa,
=Iweje nchi kama Tanzania iwakilishwe na mchezaji mmoja (ndondi) kwenye michuano hii?
Ina maana ni yeye pekee aliyefuzu ama ni yeye pekee aliyeshiriki mchujo?
Ni kweli kuwa nchi nzima haina wachezaji (ama niseme WASHIRIKI) wanaotimiza kiwango?
Na ni nani anayewajibika na kuangalia uwiano wa wachezaji-WASHIRIKI na WATAWALA wao?
Iweje idadi ya viongozi izidi ile ya wachezaji-washiriki?
Na baada ya kurejea toka kwenye michuano hii, ni ripoti gani hutolewa na kuna mafanikio gani katika marejesho ya ripoti hizo?
Ukweli ni kwamba KINACHOTUHARIBIA NI MFUMO WETU WA KUTAWALA MICHEZO NCHINI.
Kama alivyosema Ndg. Kasesela kwenye clip ya hapo juu, MAREKANI HAINA WIZARA YA MICHEZO lakini mfumo wake unaruhusu michezo kukua na kuleta matunda kama tunayoona.
Ni kwenye shule, mitaani na hata kwenye uwakilishi kama huu wa kimataifa.
Hatujiandai, hatuwekezi na bado tunategemea kuwa tutafanya vema.
Na bado hata Mhe. Rais ANATOA BARAKA KWA TIMU AMBAYO HAIKUWA NA MAANDALIZI.
NI KWELI?
Lakini hii ndio
TANZANIA YANGU....inayoenda kuwania medali zinazohitaji maandalizi bila kujiandaa. 
TANZANIA YANGU....inayoharakisha kwa mwendo wa polepole. 
Tanzania yangu....Ikimbizayo farasi kwa kobe


Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA

Tuonane "Next Ijayo"

3 comments:

emuthree said...

Labda iundwe tume, kuchunguza, maana tume ndio ulaji wetu siku hizi,...
labda, ni ile hali ya mtoto wa kijijini hawezi kwenda Ulaya, kwani hajui kimombo!

Mimi siamini kuwa hata kukimbia hatuwezi,....lakini kunahitajika juhudi kama zile za `bongo search, ..' tukavitafute hivyo vipaji kijijini.

Wapo wakimbiaji kijijini, tatizo tunaangalia huku mjini tu,...kuna kule kuangaliana. chunguza utaligundua hilo,...

Na kuna mwingine kasema, kama hujui kimomb utaendaje Ulaya....! Haya kalagabaghwe!

Yasinta Ngonyani said...

Ndugu wa mimi umesema kweli hapa..na jingine nilionalo mimi ni ile kupeana moyo hatuna kabisa, badala yake mmoja akishindwa basi tunamcheka, unadhani atapataje moyo ywa kuendelea? pili hatuna mpango mzuri wa maandalizi. huu ni mtazamo wangu.

Israel Saria said...

Nimemsikia Richard Kasesela, Wafungwa wengi ni over 18! utaanzaje kumfundisha mwizi ambaye yuko jela kutumikia kifungo,mambo ya michezo ya kushindana huko jela ni michezo ya kujifurahisha, suluhisho la michezo Tanzania ni kuwa na viongozi wabunifu, na sio wa mazoea tu...viongozi hawana email, hawako kwenye twitter, hawako kwenye FB, hawaandiki yale wanayoaamini,ili tujue misimamo yao, hawana blogs na hata kuandika makala za utafiti juu ya michezo, yaani tuna watu wanaochukulia michezo kimchezo mchezo...ntarudi tena hapa--Israel saria