Sunday, May 10, 2015

MV MAENDELEO YATIA NANGA SALAMA

Na Swahilivilla
Meli ya Mv Maendeleo imetia nanga salama katika bandari ya Unguja ikitokea kisiwani Pemba baada ya kukwama kwa muda wa masaa kadha katika eneo la bandari ya Mkoani.
 Mv Maendeleo ikiwa imetegesha katika katika eneo la bandari ya Mkoani Pemba.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka bandarini Unguja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazanzibari nchini Marekani (ZADIA) Bwana Omar Haji Ali, Afisa wa ngazi za juu katika MV Maendeleo alithibitsha kuwa meli hiyo imetia nanga ikiwa na abiria wote salama.
"Siwezi kuzungumza sana kwa sasa kwa vile bado tumo katika harakati za kushusha abiria", alisema afisa huyo na kuongeza kuwa atakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuongea baadaya mkutano na maofisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Zanzibar utakaofanyika mara tu baada ya kumaliza ushushaji wa abiria hao.
Mawasiliano ya Ndugu Omar Ali na maofisa wa ngazi za juu katika Serikali ya Zanzibar na MV Maendeleo, yankuja katika juhudi za kuwapatia taarifa za uhakika wanachama wa ZADIA na Wazanzibari kwa ujumla nchini Marekani, kufutia khofu na mtafaruku vilivyojitokeza miongoni mwa wanajumuiya hiyo baada ya habari za kukwama kwa meli hiyo kisiwani Pemba.
Bwana Ali amewataka wanajumiya hiyo kutokuwa na khofu yoyote juu ya ndugu na jamaa zao waliokuwa katika meli hiyo, kwani abiria wote wamefika salama salmini.
Meli ya Mv Maendeleo ilikwama baada ya kukosea njia wakati ikitoka katika banndari ya Mkoani kisiwani Pemba ikiwa na abiria zaidi ya 260. 
Bado haijajulikana rasmi ni hasara gani za kiuchumi zilizosababishwa na mkwamo huo wa abiria ambao baadhi yao walikuwa katika safari za kibiashara.
Taarifa zaidi baada ya mazungumzo na maofisa wa ngazi za juu wa MV maendeleo.

No comments: