Wednesday, October 21, 2015

SERIKALI YA TANZANIA YATAKIWA KUDUMISHA AMANI WAKATI WA UCHAGUZI

NA MWANDISHI WETU WASHINGTON 
Serikali ya Tanzania imetakiwa kuhakikisha kuwa amani na usalama vinakuwepo wakati na baada ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Tanzania tarehe 25 mwezi huu.
Profesa Nicholas Boaz,
Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Mawasiliano na Sera katika Chuo Kikuu cha Maryland nchini Marekani, Profesa Nicholas Boaz katika mahojiano maalum na Swahilivilla.
Akizungumza na mwandishi wetu nyumbani kwake, Profesa Boaz ambaye amerejea nchini Marekani hivi karibuni baada ya ziara yake Tanzania, alisema kuwa nchini Tanzania kuna joto kali sana na vuguvugu la mabadiliko."Kuna joto kali sana la uchaguzi. Kwa kweli naona watu wengi wanaitikia wito wa kutaka mabadiliko", alisistiza profesa Boaz.
Alisema kuwa hali duni za wananchi katika nyanja mbalimbali za maisha baada ya miaka mingi ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na miaka kumi ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ndiyo iliyopelekea mwamko wa vuguvugu la kutaka mabadiliko. 
"Baada ya muda mrefu wa CCM kuwa madarakani, na miaka kumi ya Rais Kikwete, basi watu wamepata mwamko kuwa maisha na maendeleo yao yamekuwa duni.
 Kwa hivyo wanataka wapate mabadiliko ya kiongozi na kimtazamo juu ya namna ya kuweza kuwasaidia watu hasa katika maswala ya kazi, afya, mamno ya shule na mambo mengine mengi".
Aliyataja mambo hayo mengine kuwa ni swala la uhuru wa watu kujieleza na kuuliza juu ya kitu ambacho kinawakera.
Akijibu swali iwapo kweli wananchi wa Tanzania wamepata mwamko wa mabadiliko au wanaimba tu nyimbo za wanasiasa, Bwana Boaz alisema "Huwezi kuingia akilini mwa watu kuwajua nini wanakitaka. 
Lakini ukiona watu wanakusanyika wakasema wanataka mabadiliko, kuna kitu gani cha kuuliza zaidi ya hicho?" alidadisi msomi huyo na kuongea, "huu ni ushahidi kuwa watu wanataka mabadiliko ya kweli"
Aidha alisema kuwa wimbi hilo la mabadiliko linatokana na hali ya watu kukata tamaa na ahadi zinazotolewa na viongozi wa CCM wakati wakitafuta ridhaa ya wananchi kuingia madarakani na badala yake hali za maisha kuendelea kuwa duni.
Aliutolea mfano utawala wa Rais Kikwete ambaye aliingia madarakani akiwa na ari mpya, nguvu mpya na milo mitatu kwa siku, lakini baada ya miaka kumi ya utawala wake ukuwaji wa uchumi umebakia palepale.
"Kuna takwimu zinaonesha waziwazi, alipoingia Kikwete 2005 kuchukua madaraka aliukuta uchumi ukiwa ni asilimia 0.7, kwa miaka kumi, huo uchumi umebakia palepale, na watu hawapati hata nusu mlo", alifafanua msomi huyo na kusisitiza "Watu wameamka, hawadanganyiki tena na mambo ya zamani ya kubebwa tu na Chama. Watu sasa hivi wanangalia jinsi ya kuboresha maisha yao na kulinda mustakbali wa watoto wao"
Mtaalamu huyo aliendelea kufafanua kuwa kumekuweko na takwimu za kupotosha kuhusu ni chama gani kitashinda uchaguzi, hata hivyo alisema, "Mimi nikiwa kama Mhadhiri na mtaalamu wa Mawasiliano na Sera, huwa nayaangalia mambo yanavyokwenda kwa kutumia njia inayoitwa Observational Research Method"
Alifafanua ibara hiyo ya kitaalamu kwa kusema "Naangalia mikusanyiko ya watu anapokuwepo Lowassa na anapokuwepo Magufuli. Kwa hiyo, unaweza kutazama kwa hiyo tu bila hata takwimmu".
Kwa mujibu wa utaalamu huo, Profesa Boaz anahisi kuwa upepo mwanana unapulizia upande wa vyama vinavyojumuika chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Pia alidokeza kuwa takwimu zenyewe zinabashiria ushindi kwa UKAWA. "Kuna takwimu kutoka serikalini zinasema kuwa asilimia baina ya 60 hadi 74 ya wapigakura wote ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 40. Na katika hao kuna uwezekano mkubwa vijana kuipigia kura UKAWA kuliko CCM", alifafanua msomi huyo na kuongeza "Kwa hiyo ikiwa mambo yatakwenda vizuri bila ubabaishaji, basi kuna uwezekano mkubwa kwa UKAWA kuchukua nchi, lakini tarehe 25 mambo yatakuwa wazi"
Akijibu hoja kuhusu madai ya baadhi ya wadadisi wanaodai kuwa viongozi wa CCM waliokihama chama hicho na kujiunga na kambi ya upinzani wanatumiliwa na chama tawala kama vibaraka wa kudhofisha upinzani, Profesa Boaz aliimabia Swahilivilla "Watu wana uhuru wa kudadisi mambo au maoni, lakini watu wengine wanaweza kupotosha kitu ambacho kinaonekana kina ukweli"
Aliitupilia mbali joja hiyo kwa kusema "Hayo ni mambo ambayo watu wanayazusha na hayaingii hata akilini". Aliendelea kufafanua "Mimi nimetembelea sehemu mbalimbali Tanzania, mijini na vijijini, na unakuta kitu watu wanachokizungumzia ni mabadiliko"
Alisisitiza kuwa Watanzania wana kiu ya mabadiliko, na kwamba kati ya watu kumi wanaozungumza saba wanataka mabadiliko. "Unaweza kuwakuta watu kumi, labda wawili au watatu wanazungumzia CCM, lakini saba wanazungumzia mabadiliko na wanasema ni kwa nini wanataka mabadiliko"
Aidha aliusifu mwamko wa wapiga kura kwa kuthamini na kuzilinda shahada zao za kupigia kura kiasi cha kufikia kuziita "Vichinjio" na kuzionesha wakati wanapoulizwa mikutanoni.
Aliwatolea changamoto wale wote wanaobeza vuguvugu la mabadiliko kwa ksema "Tusubiri tuone hiyo tarehe 25 tuone mambo yatakuwaje, je kweli hayo mabadiliko yanayozungumzwa yatatokea? Nafikiri labda tutazame pale, lakini joto liko na watu wanataka mabadiliko"
Akijibu swali kuhusu malalamiko ya upinzani dhidi ya uadilifu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Profesa Boaz aliyapongeza mabadiliko yaliyofanywa na Tume hiyo likiwemo swala la matokeo yote ya uchaguzi kubandikwa vituoni tangu ya Udiwani hadi Uraisi, pamoja na vyama vyote kuruhusiwa kuwa na mawakala wao ndani ya vituo vya kupigia kura.
"Nafikiri hayo ni mambo ambayo yameleta faraja kuwa kuna uwazi, kwa sababu ukileta demokrasia vitu kama hivyo vinakuwa ni vya lazima, huwezi kufanya vitu kwa kujificha ficha"
Hata hivyo, alielezea wasiwasi wake juu ya kauli ya Tume ya uchaguzi kwamba wananchi wakishapiga kura hawaruhusiwi kukaa eneo la vituo vya kupigia kura umbali wa mita 200, akisistiza kuwa hiyo ni haki ya wananchi kikatiba. "Lakini katika katiba limo hilo, mwaka 2005 watu walikaa. 
Sasa hilo ni swali la NEC kulitatua. Kwa sababu ni haki na ndiyo njia ya uwazi kuona kweli kura zetu tumepiga, tunaziona"
Alielezea kuwa raia wa Tanzania ni watu wa amani na wasiopenda fujo, na kamwe hawawezi kuanzisha jufo, na kwamba iwapo fujo zitatokea, basi wa kubebeshwa lawama ni mamlaka husika.
"Kama kuna mtu ataanzisha fujo, basi ni askari wenyewe na serikali yenyewe ya Chama cha Mapinduzi, na mimi siamini kuwa ni watu wenyewe wataanzisha fujo", alisema Bwana Boaz kwa sauti ya kizalendo, na kudadisi "Kwani kuna ubaya gani, kuna kitisho gani, au CCM ina wasiwasi?"
Alifutilia mbali madai hayo ya uwezekanio wa kutokea fujo kwa kusema kuwa viongozi wa upinzani wamekuwa wakiwahimiza wafuasi wao kutunza amani na utulivu kwa kusema "viongozi wao hao wa vyama vya upinzani wamewaambia, mukimaliza kupiga kura kaeni kule pembeni, tulieni"
Aidha, alikariri lawama zake kwa vyombo vya ulinzi na usalama na rais Kikwete mwenyewe kwa kushindwa kuyakemea mambo hayo na kwenda kinyume na katiba. "Fujo Tanzania ikianza, kwa kweli itakuwa imeanzishwa na askari na yeye rais wa Jamhuri ya Tanzania ambaye alitakiwa hivyo vitu avikemee sana, na kwamba afuate hiyo katiba, hii ndiyo maana ya sheria" alitoa dukuduku lake na kuwa "Hili ndilo tatizo tulilonalo Tanzania, sheria zinakuwa hazifuatwi"
Halkadhalika Profesa Boaz alitoa nasaha kwa rais Kikwete kuwaheshimu wapiga kura ambao ndio waliomwingiza madarakani madala ya kutumia kauli za vitisho. "Yeye Kikwete muda wake umekwisha, mimi nadhani angekaa akatulia, aache tena haya mambo ya kusema Polisi watafanya mambo ambayo watu hawayataki"
Alielezea imani yake kuwa Tume ya uchaguzi itaweza kurekebisha kasoro zote kabla ya siku ya uchaguzi. "Kwa hiyo mimi naona tusubiri mpaka Jumamosi, watu watakuwa wamelitatua, kwa sababu watu ni haki yao kutazama", alisema Bwana Boaz na kuhoji "Kwani kuna ulazima wakake nyumbani?
Prosesa Boaz alimalizia kwa kutoa nasaha kwa Watanzania wote wenye haki ya kuoiga kura kujitokeza kwa wingi kupia kura na kumchagua mtu wanayemtaka kwa njia za amani bila woga ili kuendeleza sifa ya Tanzania kama nchi ya amani.
"Kwa hiyo mimi nahisi watu wakapige kura kwa amani wachague mtu wanayemtaka, na siyo kununuliwa na mtu yoyote au kufanya jambo jengine lolote"
itafaa kukumbusha kuwa kumekuweko na hali ya sintofahamu miongoni mwa wadau wa kisiasa nchini Tanzania kufuatia kauli iliyotolewa na NEC pamoja na Rais Jakaya Kikwete kwamba wananchi wakishapiga kura hawaruhusiwi kukaa eneo la vituo vya kupigia kura umbali wa mita 200.
Hali hiyo imepelekea imepelekea baadhi ya wanasiasa wa upinzani kufungua kesi mahakamni anaitaka mahakama itamke kama ni halali kwa Rais na Tume ya Uchaguzi (NEC) kuzuia wananchi kukaa kwa utulivu umbali huo ama la.

No comments: