Tuesday, September 21, 2010

Kabla hatujapata Rais wa upinzani, ......YATOKANAYO

Jana "nilibandika" toleo langu kuhusu "nionavyo mimi" katika suala la Rais ajaye.
Kwa ujumla si rais tu, bali MABADILIKO YALIYO MUHIMU YANAYOHITAJIKA NCHINI KWETU. Na kama nilivyosema hiyo jana, "Najua kuwa MAENDELEO NI LAZIMA YAENDANE NA MABADILIKO lakini pia najua kuwa MABADILIKO SI LAZIMA YAMAANISHE MAENDELEO. Na hili ni kati ya yale ambayo ningependa wengi wayatambue na kuyajadili."
Na nilipata RAHA YA WEB LOG (ambalo ndilo hasa jina halisi na kamili la "blog") kwa watu kuweka umakini wa fikra zao kama ambavyo nilijaribu kuweka zangu. Na katika hili nilijifunza vitu.
Lakini nia hasa ya kuleta YATOKANAYO, ni kuendelea kufafanua kile ambacho nilikuwa na bado naamini kuwa chahitajika kufanyika ili kuwawezesha wapinzani kua viongozi wazuri kwa Tanzania yetu.
Kama alivyosema Kaka Fadhy, tunastahili MABADILIKO japokuwa "wengi tunayaogopa mabadiliko si kwa kuwa hatuyahitaji. La hasha. Ila kwa kuwa tunazijua vema gharama za mabadiliko. Mabadiliko yana gharama kubwa sana." Hapa nakubaliana naye kuwa mabadiliko hutisha mahala popote. Hata yale yanayotarajiwa kuwa mema huweka wasiwasi wa u-wema wake.
Lakini kwanini bado naamini twahitaji kuona UJENZI WA NGAZI ZA CHINI KABLA AWAJANG'ANG'ANIA JUU?
Blogu hii ilikuwa ya kwanza kabisa kuandika na kutenga kipengele cha UCHAGUZI 2010 abacho kilitundika post ya kwanza Machi 13, 2009. Hii ilikuwa katika kuamsha, kupanga na kuweka tayari jamii kuhusiana na NAFASI ZIJAZO ambazo nilijua fika kuwa zitagombea, na nakumbuka post ya kwanza niliiandika kuhusu VIONGOZI WA UPINZANI nikisema NINGEKUWA WAO (irejee hapa). Na hapo ilikuwa zaidi ya mwaka kabla ya kujua nani na nani watapenda ng'ang'ania nafasi mbalimbali. Na niliandika kuhusu umuhimu wa kujenga "msingi" wa utawala katika ngazi za chini.
Kisha mwezi wa pili mwaka huu, nikarejea kuandika bayana juu ya yale niliyokuwa na ambayo bado naamini YATAKAYOWAANGUSHA WAPINZANI WENYE UCHAGUZI MKUU (yarejee hapa pia).
Lakini juzi nilipoweka maoni kwenye HII POST YA KAKA KAMALA, ndugu yangu ANON alionekana kukerwa nayo lakini bado akaandika kwa heshima kupingana nami na Kaka Matondo. Aliandika "mubelwa you are singing the same song a friend of mine in Oregon is singing..." Naweza kuelewa ni kwanini mimi na rafiki w Oregon tunaimba wimbo mmoja. Ni kwa kuwa (binafsi) napenda kuona MABADILIKO KWA KUWA KUNA MSINGI WAKE NA SI KWA KUWA HATUMTAKI ALIYEPO. Na mimi binafsi naona siasa hizo za PINGA ALIYEPO BILA KUPANGA YA ATAKAYEKUWEPO ndiyo yatakayoivuruga Republican hapa Marekani ambao wameanza kujigawa kwa misimamo wakitaka kila mmoja awe mhafidhina hata kama analokubaliana nalo ama kuiunga serikali mkono ni la msingi. Ni kwa mantiki ya KUPINGA ALIYEPO, tunaona namna ambavyo mchakto wa TEA PARTY unaunda nguvu ya kupingana na Republican ndani ya Republican ili "kutuma ujumbe". NINALOTABIRI ni kuwa miaka 2 mbele, watajikuta wameweka watu ambao hawana ushirikiano na yeyote na hawana mipango yoyote makini na matokeo yake kuwafanya watu wakate tamaa nao kabisa katika CHAGUZI MKUU ZAIDI ambao wangefurahi kumng'oa madarakani Rais. Kwa maana nyingine, kwa kutojipanga vema, kumng'oa aliyepo kwa sera a kile utakachofanya, unakuwa unajitengenezea mazingira mazuri ya kung'olewa kwa kile ambacho hutafanya.
Kaka John Mwaipopo naye akaeleza kwa kina akisema "nyote mnaodhani tanzania bado kufanya mabadiliko your wish will be granted lakini haikatazi kuona kuwa kuna sehemu ya watanzania wanaotaka mabadiliko ya kweli, within or outside the vanguard party. atashinda mumtakaye lakini tuwaache watanzania waseme october 31. hata kama wanaotaka mabadiliko wataambulia robo, robo ni namba ya kujua watu wanataka nini?"
Nakubaliana kabisa na Kaka John, robo ya watakaoonekana kutaka mabadiliko watakuwa wmetuma ujumbe mwanana, lakini kama ndugu hawa baada ya uchaguzi hawatajisumbua kujenga vyama, kujenga kaya na ngazi nyingine zote, watavuma kisha waapotea kama ilivyokuwa kwa kina Masumbuka Lamwai na sasa Dr Slaa ambaye naye ametoka bungeni.
Nimaanishalo hapa ni kuwa, kama vita ama pilika zao ni kuing'oa CCM, basi wajue kuwa CCM wana vitu vingi vinavyowaunganisha na vitakavyowarejesha pamoja baada ya kushindwa, ilhali kwa wapinzani, kuing'oa CCM itakuwa ni KUTIMIZA NDOTO YAO ilhali si jukumu walilotumwa na wananchi.
Kwa hiyo wasibweteke hata pale watakaposhinda kwani kushinda ndio hatua ya mwanzo ya kufanya walilotumwa, na kama ama kabla hawajajenga msingi mzuri wa utekelezaji katika ngazi ya mpiga kura, basi nauona ushindi huo kama "ticking bomb" litakalokuja kuwalipukia wakiwa wamelikalia.

Na huu ni mtazamo wangu kwa namna nionavyo tatizo. Labda namna nionavyo tatizo ndilo tatizo.
Natunza haki ya kukosa na kukosolewa.


Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kaka Mubelwa huu ndiyo wakati ambao Watanzania karibia wote ndani na nje ya nchi tunacheza mdundiko wa aina moja. Siasa na uchaguzi mkuu.

Uchaguzi mkuu unaohusiana na ustaarabu wa vyama vingi.

Wiki iliyopita niliweka maoni kwa kaka Chib, nikamwambia kuwa chaguzi zilizopita nilipiga kura kwa ushabiki. Mwaka huu nitaitumia vema kura yangu.

Kwa nini nadhani nitaitumia vema kura yangu? Kwa sababu nataka kuwa sehemu ya mabadiliko ninayopenda kuyaona. Hapo ninakumbuka busara ya Mahatma Gandhi, you must be the changes you wish to see in the world.

Awali nikiwa bado mdogo sana wa shule ya msingi, nilijiuliza sana, kwa nini Mwalimu Nyerere alitaka tuingine ktk mfumo wa vyama vingi wakati asilimia 80 ya Watanzania hawakutaka? Baadaye nikaja kumsoma vema katika kitabu chake, Uongozi Wetu Na Hatma Ya Tanzania.

Mwalimu alisema, CCM imejisahau mno. Hivyo inaelekea kuwa chama cha kidikteta. Huu ni ukweli ukweli mtupu. Kiongozi wa juu wa chama anapofikia pahala akawaona wananchi wengine wote hawana fikra wala kumbukumbu nzuri, kiasi cha kuwakatalia hakutoa lugha fulani aliyowahi kuitoa hata miezi sita haijapita, unaona chembechembe za mawazo ya Mwalimu.

Hebu tuone na hili. Chama kinachoyajali maisha ya wananchi wake, kikapanga bajeti zaidi ya bilioni 50 kufanya kampeni za anasa huku zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wake wakiogelea kwenye bahari ya umasikini, tunapaswa tujiulize mara mbili. Nimekosea hapa, ninapaswa siyo tunapaswa.

Labda niseme na hili, uongozi uliokaa muda mrefu ukashindwa kujua namna ya kuzitumia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wote. Nchi iliyobarikiwa mito, maliasili na ukanda mkuuuuuubwa wa pwani, milima, vilima na nyanda zenye rutuba kiasi hakuna mmea usiokubali Tanzania. Wanyama weeeengi. Bado uongozi huo ukasema hatuwezi kuendelea bila misaada. Unapaswa kufanyiwa mabadiliko.

Tunashindwa kuitazama Rwanda kwa jicho la aibu. Waliokuwa vitani miongo mingi. Wasio na bandari. Ambao ukubwa wa nchi yao ni sawa tu na ukubwa wa wilaya ya Mbozi, leo hatuwafikii kiuchumi. Sisi tunakazana kununua fenicha Dubai, magari ya bei chafu Japan na safari za anasa ndani na nje ya nchi.

Kila siku nikisimama kwenye kituo cha daladala pale Benki, jijini Mbeya, huwa nayaona maandishi makubwa kwenye uwanja wa mpira wa Sokoine. Yanasema, NCHI MASIKINI HAZIWEZI KUENDELEA KWA KUTEGEMEA MISAADA KUTOKA NCHI ZA NJE-MWALIMU J.K. NYERERE.
Tatizo mie nahama sana kwenye mada, ngoja nirudi.

Mabadiliko. Lazima yaje tu. Niliandika jana http://fadhymtanga.blogspot.com/2010/09/wakati-ukifika-umefika-tu.html

Mwaka 1992 wakati vyama vingi vinaanza, mtu mmoja Zablon I. Manzi, aliandika kitabu, Tuyaelewe Mageuzi. Yule bwana ana akili sana. Alieleza jinsi nchi zote duniani hususani za Kisoshalisti zilivyokuwa zikiyapitia mageuzi. Akatoa rekodi pale. Kama tungekisoma kitabu kile vema, tungeanza kujiandaa mapema sana kuelewa, tutake tusitake, mabadiliko hayakwepeki.

Jana nilisema tatizo tunaziogopa gharama. Ni kweli.

Wanaoziogopa gharama wacha waziogope. Sisi tutapewa moyo na kauli ya Mwalimu Nyerere, aliyoitoa panapo Novemba 5, 1980 akipokea maandamano ya vijana Ikulu kumpongeza kuchaguliwa kwake kama rais. Aliwaambia maana ya demokrasia. Akasema demokrasia siyo tu ni sauti ya wengi kusikilizwa, bali pia sauti ya wachache kuonekana.

Kura yangu, haitojali kama itakuwa katika sehemu ya sauti ya wengi kusikilizwa, ama sauti ya wachache kuonekana. Angalau itakuwa katika fungu la wao wasemao kwa uwazi kabisa kuwa, tunahitaji mabadiliko.

John Mwaipopo said...

fadhy katika hili la mabadiliko nakuacha uwe msemaji wangu. umekubali?

kinachoturudisha nyuma watanzania ni woga ambao umepandikizwa vichwani mwetu kwa vizazi vingi. leo wafanyabiashara wanaogopa wakifanya mabadiliko biashara zao zitakwenda kombo. wakulima wanadhani watakosa mbolea (mwananchi leo, mbeya vijijini). walio nje ya nchi wanadhani kukitokea mabadiliko hawatakuwa watanzania tena. wakinamama wanadhani watageuka wakina baba, wakinababa wanadhani watageuka wakina mama.

mkiwa madereva wengi kwenye chombo kimoja akichoka huyu anampisha huyu.

wapinzaji sio kuwa hawajijenga vijijini. wapo wamejaa tele isipokuwa vyama vyao havina mihela. pengine mihela itumike kuona vyama viko vijijini. lakini mihela ndio tumeikataa miaka yote kuwa sio msingi wa maendeleo nchini. wanaotoa mihela, mikapelo, mitisheti na mikanga wanaitoa wapi?

vyama vya upinzani vitajijenga kwa hoja sio kwa halua na tende.

kupinga kwangu kusubiri mno kuliwahi kunighafirisha na baadhi ya wachangiaji pale kwa Koero. time is 'nau'. pengine neno 'upinzani' lina ukakasi katika kiswahili na hivyo tunapoongea 'upinzani' katika siasa tunabeba dhana ile ilea ya ukakazi. ndio maana baadhi ya wanaharakati wanataka tuviite vyama vya ushindani. upinzani sio uadui. ni muendeleza wa ushindani katika kuleta maisha bora iwezekanavyo kwa wananchi.

Anonymous said...

Wow all I can say is that you are a great writer! Where can I contact you if I want to hire you?

Mzee wa Changamoto said...

Thanx Anon.
I can be reached at changamoto@gmail.com
Blessings