Mwendo huu ungekuwa wa kuelekea vijijini "kuwajulia hali"
Mfumo wa vyama vingi unaoendelea kuwepo sasa nchini Tanzania ulirejeshwa mwaka 1992. Miaka 18 iliyopita. Na sasa wale waliozaliwa wakati mfumo huo wa siasa ukirejeshwa nchini, wanashiriki kwa mara ya kwanza kwenye mchakato mzima wa kupiga kura mwaka huu. Hii ni asilimia kubwa saana ya wananchi wanaotegemewa kupiga kura nchini.
Ninapoangalia mfumo wa upigaji na wapigaji kura nchini, nawaona katika makundi mawili. Kuna WAZEE ambao kwa bahati mbaya wanaamini kwenye "chama kilichotutunza" na VIJANA ambao wana nafasi kubwa ya kubadilishwa mitazamo yao kisiasa. Lakini ni nani wa kufanya hivyo? Na je! Anafanya?
Hapa ndipo linapokuja tatizo la upinzani na hapa ndipo watakapoanguka wakati wa uchaguzi ujao.
Vyama vya upinzani vimeonekana kuwa vyama vya kulalamika kuliko kuja na suluhisho la malalamo waliyonayo. Na hili lawafanya wazee kuwaona hawa kama wapenda madaraka na kwa vijana wanakosa la kulinganisha kwani kinachofanyika ni kulalamika bila kuwapa picha kamili ya nini kilikuwepo kabla ya kuja kwa mfumo wa vyama vya upinzani na nini watafanya kama watapewa dhamana ya kuongoza.
Wapinzani (kama ilivyo kwa chama tawala) hawajaonekana kuwa tayari KUJENGA MISINGI YA SULUHISHO kwa wananchi kwa kushirikiana na wale wa ngazi za chini kuanza kutatua matatizo yao. Kwa ufupi ni kama vile wanaongeza juhudi kumwagilia matawi badala ya mizizi. Ni watu wanaonekana kuwaza na kuota UBUNGE NA URAIS bila kuwa sehemu kubwa ya serikali za mitaa.
Waheshimiwa walio upinzani (kama ilivyo kwa watawala) hawaonekani kukabiliana na takwimu na upotoshaji (kama upo) unaoonekana kufanya na chama tawala na hawajibu hotuba za Rais atoazo kila mwezi. Kwa nchi zilizoendelea (ambao ndio wametukaririsha huu mfumo wa vyama vingi na kutufanya tuamini kuwa vyama vingi ndio demokrasia ya kweli), Rais anapotoa hotuba yake huwa kuna majibu toka upinzani. Iwe ni kumuunga mkono ama kueleza wasiwasi wao ama hata "kunyoosha takwimu" zinazoweza kuwa zimepindishwa na hotuba hiyo. Lakini wenzetu wa upinzani hawafanyi hivyo. Labda ni kwa kuwa hawapati muda TBC, lakini vipi kuhusu tovuti zao (kama wote wanazo) ama kutumia forums kama hizi ama kuwa na ukurasa kwenye You Tube ama Facebook na kuanza kuigusa jamii ambayo wanaweza? Vipi kuhusu viongozi wao wa mitaa na ngazi zote kuwaeleza wananchi wao juu ya usahihi wa kinachoelezwa?
Wanasubiri wakati wa kampeni za udiwani, ubunge na hata urais waanze kuorodhesha takwimu zisizo sahihi zilizotolewa na chama tawala..
Wapinzani wetu (kama watawala) hawang'ang'anii upatikanaji wa majibu ya matatizo ya wananchi hata pale yaonekanapo kuwadhuru wananchi na kupuuzwa. Mfano ni matokeo ya kidato cha nne. Kama asilimia 17 (Rejea SIKITIKO HILI)ndio wafaulu (daraja la I - III) na hakuna anayewajibika? Nililosikia ni "masikitiko" tuu toka kwa viongozi kisha ni "mwendo mudundo". Kama wao hawawajibiki na hawaoni haja ya kuwajibika, ni kwanini viongozi wa upinzani wasionekane kuwa na nia ya kuwawajibisha KWA MANUFAA YA TAIFA?
Ama sakata la maji taka toka viwandani na migodini ambayo yameathiri wananchi kwa sumu yake (rejea HAPA KWA KAKA CHACHA)
Wapinzani (kama watawala) hawasaki UWAJIBISHWAJI KATIKA CHANZO CHA TATIZO na kuielewesha jamii juu kwa umakini kuhusu kilichotokea na kwanini kimetokea. Mfano ni kesi za karibuni na hasa hii ya Familia ya Nguza. Miaka sita iliyopita wapo walioonekana kuwa na hatia, mwezi huu wameonekana hawana. Hakuna anayeonekana (na sitashangaa kama hakuna atakayejitokeza) kuibana serikali kujua na nani mwenye makosa na atawajibishwa vipi? Je ni kweli kuwa watoto wale wametendewa haki kwa hawa walioshukiwa kuwabaka (kama ni kweli walibaka) kuachiwa huru? Ama ni haki kwa vijana hawa wawili kukaa jela miaka 6 kwa kosa ambalo hawajatenda (kama kweli hawakutenda)? NA NI VIPI WATAFIDIWA KWA KUHARIBIWA TASWIRA YAO MBELE YA JAMII?
Na ni vipi kosa kubwa kama la kulawiti lifutwe kwa kuwa LILIKUWA LA KUTUNGA? Huyo muendesha mashtaka na mashahidi waliosema yale yaliyowafunga hawa TENA CHINI YA KIAPO watawajibishwa vipi? Na sasa kuna wangapi wanaoweza kuwa magerezani kwa kubambikiwa kesi kama hizi?
Ni maswali kama hayahaya kuhusu kesi ya kina Zombe ambao kama hawakutenda waliyoshitakiwa, basi ni nani alitenda?
Labda watetezi wa upinzani watasema "hawako wengi / hawana nguvu Bungeni" lakini hii ni kwa kuwa viongozi wenye uwezo wa kuongeza nguvu Bungeni wanawaza uRais pekee bila kuweka misingi katika udiwani, u-Meya, katibu kata na hata ubunge. Hivi tukiwa na Rais wa upinzani sasa tafanya kazi kwa kutekeleza sera na ilani za chama chake ama kwa ilani za CCM ambazo zitakuwa zinatekelezwa (kama zinatekelezwaga) katika ngazi ya majimbo na tarafa ambako wametawala? Juni 16 mwaka jana niliandika bandiko lenye kichwa Kama hauko juu ya juu, basi shuka chini uwe juu na katika bandiko hilo nikauliza "Kwani Mrema, Lipumba, Mbowe, na wengine wangekuwa wabunge unadhani Bunge lingekuwa na ladha gani? Si hata wale wabunge "wafyata mkia" wangepata ujasiri wa kusema yale watakiwayo kuwasemea wananchi?
Nililomaanisha na ninaloamaanisha: Ni kuwa wanasiasa wetu wanapenda juu (urais) ambako hawako juu (hawaaminiki na hakuna dalili za wao kupata karibuni), basi wangeshuka chini (ubunge) wawe juu (wawe wengi, wenye nguvu na uwezo wa kuibadili serikali kama haitendi sahihi) na hapo tungeweza kuibadili nchi."
Lakini hili halionekani kuwa wazo kwa wapinzani. Bado naamini kuwa wangeelekeza nguvu zao kwenye ngazi za chini na kushirikiana na wananchi kwa umakini, wangejenga IMANI wanayostahili na ambayo hawana na kisha kupewa dhamana.
Pia wapinzani (kama watawala) wanastahili kuwekeza kwenye kuyatambua MATATIZO HALISI YA WATANZANIA na kuwa SAUTI YENYE SULUHISHO LINALOWASHIRIKISHA WANANCHI. Nimeshuhudia ahadi za "nikichaguliwa nitafanya hivi na vile" na wanaposhindwa kuchaguliwa hawaonekani tena. Wanasiasa wetu (na hasa wapinzani) wamekuwa wakijitahidi kuwaaminisha wananchi kuwa wanaweza kuwa na suluhisho la matatizo pale wanapochaguliwa na si wakati mwingine. Pia wanajitahidi kuwaaminisha wananchi kuwa wao ndio wenye suluhisho badala ya kuwaonesha wananchi namna wanavyoweza kutumia rasilimiali walizonazo (wakiwemo wananchi wenyewe) kufanya mabadiliko makubwa ambayo watajivunia.
Nilipoandika Machi 11 kwenye post yenye kichwa NINGEKUWA WAO niliandika orodha ya mambo ambayo niliamini na bado naamini wanastahili kujiuliza wanapojiandaa kuelekea kwa wananchi kuomba kura.
(i)Kwanini watu wanaendelea kuumia na kuwa na uchumi m'baya huko vijijini licha ya kuwa na rasilimali zote?
(ii)Kwanini watu wanakosa upendo na imani kwa serikali?
(iii)Kwanini walio madarakani hawajui uhalisia wa matatizo yawakumbao wanakijiji ilhali wao ndio wawakilishi wao?
(iv) Kwanini licha ya sheria nyingi bado silaha zimetapakaa mitaani na zaendeleza mauaji na uporaji na kuteteresha usalama?
(v) Kwanini UKIMWI waendelea kusambaa na kuteketeza nguvukazi ya taifa licha ya mamilioni kumwagwa kusaidia kuutokomeza?
(vi) Kwanini thamani ya shilingi yazidi kushuka ilhali gharama za maisha zazidi kupanda bei lakini kwa wenye kipato cha chini?
(vii) Kwanini mauaji yanatendeka kwa wingi kama vile hakuna sheria? Kwanini watoto wa vijijini hapati elimu sawa na wale wa mijini?
(viii) Kwanini watu waendelee kubabimbikiziwa kesi wakati hawana hatia?
(ix) Kwanini tofauti ya maisha ya wenyenacho na wasionacho inazidi kuongezeka?
(x) Kwanini mauaji ya ndugu zetu albino yanazidi kuongezeka?
(xi) Ni nini kilichopo kati ya serikali kuu na wananchi ambacho kinazuia malengo na habari baina ya "vituo" hivi viwili vikubwa?
Kisha ni kupanga mikakati iliyo sahihi kujua namna ya kukabiliana na matatizo hayo na kwa kuwa na sera na ilani zinazoweza kuonesha njia halisi ya kutatua matatizo mengi ya wananchi walio wengi na ambao ndio wanataabika, sio tu kutaweza kuwapa nafasi ya kuingia IKULU, bali hata atakayeingia atajua kuwa kuna wenye mipango madhubuti ya kutatua matatizo ya watanzania na kama atazembea basi wananchi watakumbuka kuwa SULUHISHO LINALOSUBIRI NAFASI YA KUTATUA MATATIZO YAO.
Tatizo ni kuwa hakuna anayeonekana kuwa na suluhisho la matatizo na kama matatizo ndio kitu pekee ambacho watu wanakihitaji toka kwenu, basi hamtashinda uchaguzi wowote.
Na ni kutotafuta suluhu na ushirikishwaji wa wananchi katika kutatua matatizo yao kutakaowafanya muishie kuwa wagombea wasiopewa dhamana.
KWANI KAMA NINYI (WAPINZANI) NI KAMA WAO (WATAWALA) ILA MNAKOSA USHIRIKIANO NA UZOEFU, KUNA HAJA GANI YA "KUWAJARIBU" NINYI??????
Na ndio maana naamini HAYA NILIYOANDIKA HAPO JUU YATACHANGIA KUWAANGUSHA WAPINZANI KWENYE UCHAGUZI MKUU UJAO
Kumbuka tu kuwa huu ni mtazamo wangu, na natunza haki ya kukosea na kukosolewa. Labda namna nionavyo tatizo ndio tatizo
Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA
1 comment:
Mzee wa Changamoto,
Makala nzuri na yenye maeneo mengi sana ya msingi ambayo ningekuwa mwanasiasa,wa chama tawala au wa upinzani,ningeyazingatia.Zaidi nimependa ulipogusia matumizi ya social media katika kueneza ujumbe.Hili linabidi kuangaliwa sana!Atakayeanza nina uhakika atafanikiwa.
Post a Comment