Monday, September 6, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa....YALIYOPITA SI NDWELE

Mara ya kwanza kabisa kusikia habari za wimbo huu, ilikuwa ni kutoka kwa aliyekuwa Mwl Mkuu wa Shule ya Mazoezi Kigurunyembe Mwl Mihambo ambaye alikuja kuongea nasi wanafunzi tulipokuwa "mstarini".
Alitueleza faida za kusamehe na kisha akasema kuna urahisi wa kusamehe lakini si rahisi kusahau na ugumu wa kusahau ndio ambao husababisha ama kuleta akili na fikra za kulipiza kisasi. Kisha akauliza kama tumeshasikia wimbo mpya unaosema nimekusamehe lakini sitakusahau. Ndipo nilipopata HAMU ya kuusikia.
Na nilipousikia, sikuwahi kupoteza "pendo" na wimbo huu. Ndipo nilipounganisha sauti ya Eddie Sheggy na nyimbo zake za awali, gitaa la Hamza Kalala na kazi za awali (hao ndio nilibahatika kuwatambua kwa wakati huo) na kisha nikawa mpenzi mkubwa wa Washirika Tanzania Stars.
Lakini kuna UJUMBE wake kuwa japo hatuwezi sahau, haimaanishi kuwa tusisamehe. Nakumbuka post ya karibuni ya Kaka Matondo kuhusu Madaktari waliogombana ilhali mama mjamzito anasubiri upasuaji wao (iko hapa) na matokeo yake bandiko linasema "kutokana na kuchelewa kufanyiwa operesheni hiyo, mfuko wa uzazi wa mwanamke yule ilibidi uondolewe kabisa. Isitoshe mtoto alipata matatizo ya moyo na kuna uwezekano huenda amepata madhara ya kudumu ya ubongo kutokana na ukosefu wa hewa ya Oksijeni."
Ni nini unaloweza kufanya kwa watu waliokusababishia haya? Ni adhabu gani waweza kuwapa kutosheleza yaliyokukuta?
HAKUNA
Utakalopambana nalo ni juhudi za kuwasamehe ilhali unajua kuwa HUTASAHAU. Tunaishi na mambo kama haya kila siku na kwa namna na viwango tofauti. Iwe ni kwa watu wa nje ama wale "wandani" wetu. Na si mapya kwani yalionwa zamani.
Jikumbushe wimbo huu ulioteka mioyo ya wengi kutoka kwao Washirika Tanzania Stars Band wakisema YALIYOPITA SI NDWELE

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia siku za Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama kupitia mitandao rafiki HAPA na pia kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania HAPA

1 comment:

emu-three said...

Ni kweli kama dunia ingejenga `uono huo' wa kusameheana nafikiri tungekuwa katika `kisiwaa cha amani'
Ndio unaweza ukapata baya ambalo kulisamahe kunahitaji moyo, lakini `samehe tu' kwani kama binadamu unaweza ukatenda baya zaidi ya hilo kwa mwenzako naye akikumbuka kuwa ulimsamahe naye hatakawia kukusamehe!
Kweli nyimbo za kale zilikuwa na uumbe murua!