Thursday, November 4, 2010

AGENDA YA KWANZA YA UCHAGUZI WA 2015 IWE NI UCHAGUZI WA 2010

"A nation that forgets its past is doomed to repeat it." Sir Winston Churchill
Nilipobandika toleo langu la kwanza la kipengele cha "UCHAGUZI 2010" la Machi 11, 2009 nilipata barua pepe ikiniambia kuwa "uchaguzi ni mwakani wewe unaanza kuujadili sasa?". Naamini alilomaanisha mtuma ujumbe ni kuwa nilikuwa nimewahi mno kuanza kujadili mchakato mzima wa uchaguzi kwani bado kulikuwa na mwaka mmoja, miezi saba na siku 20 kabla ya "siku ya siku". Lakini sasa.... ni historia.
Uchaguzi mkuu wa Tanzania ndio umemalizika kwa wananchi "kutuma ujumbe" kwa wahusika kwa namna waliyoamini ni sahihi. Lakini wakati uchaguzi huo ukisubiri matokeo (ambayo naamini "yanawekwa sawa" kabla ya kutangazwa), naamini pia HUU NDIO WAKATI WA KUANZA RASMI MBIO ZA 2015 KWA WENYE NIA DHAHIRI NA HALISI YA KUIKOMBOA TANZANIA.
Ninasema mbio zianze kwani ni vema kwa wahusika kuanza kutengeneza mazingira mazuri ya uchaguzi kwa kujaribu kukosoa mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Na kama matokeo ya jumla kwa nchi kama Tanzania yanaweza kuchukua siku kadhaa "kuwekwa sawa" na kutangazwa, naamini KUBADILI MFUMO WA UCHAGUZI KUTAHITAJI MIAKA KADHAA.
Ni katika kuwaza namna ya KUBORESHA uchaguzi wa mwaka 2015, nikaona kukusanya haya machache ambayo nayaona kama ajenda / agenda ya kwanza katika kuelekea uchaguzi huo ili wakati ukifika tusirejee "kulia" kwa yale ambayo yalishatokea na tukayapuuza. Na ndio maana nilianza na hiyo nukuu ya Sir Churchill.
Sasa baadhi ya ajenda za CHANGAMOTOYETU kuelekea uchaguzi 2015 ni.....
1: MIDAHALO KWA WAGOMBEA URAIS NI LAZIMA.
Mwaka huu nilishangazwa, kusikitishwa na kukereka na namna ambavyo chama tawala kilionesha dharau kwa kugoma kufanya mdahalo. Sababu niliyoisikia ikitajwa ni kuwa wagombea watawafuata wananchi huko waliko. Huu ni upungufu wa elimu ya awali ya uraia.
Kuna haja kwa bunge kupitisha SHERIA ya midahalo (japo mitatu) kwa wagombea wote wa nafasi ya uraisi ili kuweza kuwapa uwanja wa kupambana. Mwaka huu tumeona walivyokuwa wakirushiana "ya nguoni" kwa kuwa tu hawakuweza kukabiliana ana kwa ana kupambanisha sera.
2: REJEO ZA AHADI ZA UCHAGUZI 2010
Sitashangaa kusikia kuwa ni asilimia chache ya waTanzania wanajua nani aliahidi nini wakati wa kampeni. Hili ni kwa kuwa siamini kama kila aliyejitokea na fulana ya chama huzika alikuwa amekwenda kusikiliza sera na si kingine. Baadhi ya wagombea wameonekana kwenye taswira wakiwa na umati wa kuridhisha japokuwa si hakika kuwa wote walioenda walisikia na kunukuu ahadi zilizotolewa. Kama hukubahatika kuziweka ktk kumbukumbu, ZISOME (za wagombea uraisi) HAPA
Kinachotakiwa ni kusubiri 2015 ili kujua zimetekelezwa vipi.
3: UCHAMBUZI WA AHADI ZINAZOTOLEWA.
Kwa bahati mbaya ni kuwa wengi wa "waandishi" wanawekeza kwenye kunukuu kilichosemwa na si kusaka uhalali wa kinachosemwa. Mfano, nilimsikia mgombea uRaisi kwa CCM akisema... ndani ya miaka 5 atahakikisha maji toka ziwa Victoria yanawafikia watu wa Tabora ilhali walio "mwaloni" katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara hawana maji ya kutosha toka ziwa hilohilo ambalo lipo mwendo mfupi zaidi ukilinganisha na mkoa wa Tabora. Watu wakapiga makofi, vigelegele na naamini kura zikahahakishwa...Hakuna aliyehoji wala kudadisi usahihi wa ahadi kama hiyo na kuwa kama atafanya hivyo kwa Tabora baada ya kumaliza Kagera Mwanza na Mara.
4: KAMPENI SI NYUSO ZA WATU PEKEE.
Helikopta zilikuwa kivutio kikubwa saana (na pengine ukiongeza fulana, kuwaona wasanii bure, kofia, kanga na kadhalika..) vyaweza kuwa sababu pekee ya watu kufurika mikutanoni. Lakini swali hapa ni kuwa ni kwanini wagombea wahimize kuona maisha ya wananchi mikutanoni? Nina hakika kuna mahali ambapo wagombea wa mwaka huu hawatarejea tena mpaka miaka 5 ijayo watakapoomba kura. Je! ni asilimia ngapi ya matatizo ya wananchi hudhihirika kwenye mikutano ya kampeni?
Kuna haja wagombea wakatafuta namna ya kuungana na kujihusisha na maisha halisi ya wananchi kwa kuwatembelea na kuona mazingira waishiyo hivyo usafiri usiwe wa kupaa na kutua pekee. Labda ndio maana wagombea hawajui hata kero za barabara za "wananchi wao".
5: TUME YA UCHAGUZI.
Hapa najua sina la kunena. Hii ya mwaka huu imenifurahisha zaidi maana licha ta TEKNOLOJIA kutumika katika chaguzi za miaka hii, licha ya kuwa tume hii ilikuwa ikitambua na kujiandaa kwa uchaguzi huu tangu mwaka 2005 (ulipoisha uliopita), licha ya wagombea kusema miundombinu imetengemaa zaidi, bado tume ya uchaguzi imekuwa kero zaidi ya maelezo.. Hili wengi walilizungumzia na hata mtandao wa Bongo Celebrity uliliongelea.
Kwa ujumla TUME YA UCHAGUZI TANZANIA INASTAHILI MAREKEBISHO.
6: ELIMU YA URAIA KWA WANANCHI
Kati ya mambo yaliyosikitisha katika uchaguzi uliomalizika ni idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura ukilinganisha na waliojiandikisha. Na pia kura zilizoharibika zimekuwa nyingi kiasi kwamba kama uharibifu huo ungezuiwa kwa elimu ya uraia kwa wapiga kura, labda matokeo yangekuwa tofauti na yalivyo. Mfano halisi ni nafasi ya Uraisi visiwani Zanzibar ambapo tofauti kati ya Rais Ali Mohamed Shein na aliyeshika nafasi ya pili, Seif Sharif Hammad ilikuwa ni kura 3471 ilhali zilizoharibika ni 6109. Kwa maana nyingine, kama theluthi mbili ya kura zilizoharibika zingeweza kuwa halali, kungekuwa na ushindi mpana ama wa tofauti zaidi.
Lakini yote juu ya yote, kusikia kitui kiliandikisha watu elfu ishirini na waliopiga kura ni elfu tatu hizi si habari za kupuuza hata kidogo.
Unahitajika uelimishaji kwa wapiga kura ili watumiapo muda wao (ambao wanatakiwa kuhimizwa kuutumia) kupiga kura, basi wahakikishe kuwa kura zao haziharibiki na uchaguzi wao unahesabika.

Uchaguzi 2015 ni "label" inayozungumzia namna nilivyoona uchaguzi wa 2010 na namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

2 comments:

chib said...

Safi sana Mzee wa Changamoto.
Kila siku tunasingizia tunajifunzaaaa, wakati tuna miaka 5 ya kujiandaa kabla ya uchaguzi. Tunapaswa kuanza sasa

emu-three said...

Miaka mitano kwani mingi, hebu kumbuka juzi tu tulikuwa ndani ya uchaguzi, sasa jana ndiyo imepita!
Tatizo kubwa ni kusahau. Hayo uliyonena kama yatafanyiwa kazi basi uchaguzi unaokuja tungepeta, lakini mmmh, akishaapishwa bwana mkubwa wengine wanaingia mashambani kulima, kutafuta riziki, ku...ku....ku, unasikia kukuruku kumekucha, uchaguzi ujao huu hapa!
Mimi nafikiri mtu ukishaahidi mbele ya kadamnasi ni `deni' na uslipolipa deni hata ukifa roho yako haitastarehe! Ndio maana kabla ya kuzikwa watu wanaulizwa, `je kuna anayemdai huyu marehemu'
Sasa kumbuka ahdi ulizotoa kwa watu ni madeni hayo, je ukifa nani atayalipa, au unasema `umewatia watu changa la macho ukapita..'
Ndugu yangu hilo ni deni, mapaka ulilipe na kulilipa ni kutimiza ahadi ulizoahidi!