Wednesday, October 20, 2010

Nani anayetafsiri hizi taswira sawasawa?

Tangu kuanza kwa kampeni za uRaisi na ubunge, tumeshuhudia “mchipuko” wa picha mbalimbali zikionesha wagombea wakiwa sehemu mbalimbali wakiwa wamezungukwa ama kuhutubia umati mkubwa wa watu toka itikadi, rika, hali, mitazamo na hata rika mbalimbali.
Lakini pia tumeshuhudia UANDISHI wa ajabu (ama tuseme wa kisasa maana u-sasa unatafsirika zaidi kama kupoteza uhalisia) ambapo hata WAANDISHI WAANDAMIZI wanalofanya ni kutujuvya juu ya …… afunika huku ama kule. Na hakika picha zaweza kuonesha kile anachodhani anasema japo swali la kujiuliza ni kuwa NI NANI ANAYETAFSIRI HIZO TASWIRA?
Katika darasa langu la PHOTOGRAPHY APPRECIATION, nimefunzwa kuwa TAFSIRI YA PICHA MOJA YAWEZA KUWA NA MAANA NYINGI KULINGANA NA UMAKINI WA MTAFSIRI.
Picha tuoneshwazo za wagombea wa Urais zaambatanishwa na vichwa vya kuvutia kama “Dr Slaa aiteka Moshi” ama “JK apokewa kwa shwangwe” na picha zenyewe zaambatana na umati mkubwa wa watu (jambo ambalo laweza endana na kicha husika). Lakini ni nani anayefanya uchunguzi kujua kuwa waliokwenda pale wamekwenda kwa sababu wanamuunga mkono?
Ni nani anayeangalia ama kuchunguza kama kiwapelekacho pale ni SERA na sio NAFASI YA KUMUONA MGOMBEA? Nadhani umeona aliyoandika Da Subi kuwa "Kwani tatizo ni wingi wa watu basi? Shida ni hii..."(irejee hapa) ambapo alidhihirisha kuwa hata wasanii wa bongo fleva huvuta umati kwenye bonanza sawia na huu umati tuuonao kwenye kampeni. UMEONA KINACHOFANANA? UMEJUA KWANINI KOTE "WANAJAA"?
“Maonesho” yote (ya Tigo, Voda, Zain, CCM, CHADEMA, CUF....) ni ya bure na watu hawa "humwagika" kushuhudia kile ambacho ni ADIMU kwao. Kwa maneno mengine ni kuwa HII NI NAFASI PEKEE YA KUMUONA MHESHIMIWA MTARAJIWA kwani wakishapata kura wanasahau kila kitu. Sasa niulize kwa yale niliyoona. Hivi Raisi kukaa chini na hohehahe kama sisi ni desturi yake ama ni jambo la mara moja katika miaka 5? Iweje leo akae chini ilhali alipokwenda kupanda mti (ambapo alijua kuwa anakwenda kupanda mti na angevaa mavazi yaendanayo na shughuli hiyo) aliwekewa mkeka na kutumia “koleo”?
Hawa waliomzunguka “mtarajiwa aliye tumaini lao” wana hali gani ya maisha? Wanamuona mara ngapi na ni nini hasa kilichowavutia? Tumaini? Yeye ni nani? Kwanini izungumzwe "alivyopokelewa kwa shangwe" badala ya kuuliza "wananchi na yeye walikuwa wapi mpaka makazi yaonekanayo nyuma yake yamefikia hatua hiyo"?
Tunapoangalia taswira zote hapo juu na zote za kampeni, tujiulize mambo kadhaa kabla hatujakubaliana na “vichwa” vya waandishi wafurukutwa.
1: Unaona nini?
2: Yahusu nini?
3: Yawakilisha / kuhusisha nini?
4: Nguvu ya kitamaduni yajengwaje humu?
5: Jamii husika yanufaika vipi?
6: Taswira ni sehemu ya tukio, ama suluhisho la nini?
7: Taswira yaakisi nini?
8: Taswira ni matokeo na nini?
9: Kwanini taswira imekuwa namna ilivyo?
10: Taswira iko ndani ya tamaduni gani?
11: Inamfundisha nipi mtoaji, na mpigwaji/ mhusika?
12: Waliopo pichani wana lipi la kujivunia?
13: Yaonesha nani akifaidi na nani akifaidiwa?
14: Yaonesha tatizo? Ni lipi na latatuliwaje?
15: Kuna kinachofunuliwa?
16: Inaathiri vipi maisha ya wahusika?
17: Inabadili mtazamo wa mpigaji na msomaji kuhusu nchi?

NAWAZA KWA SAUTI TUUU!!!!

PHOTO CREDITS: WAVUTI.COM, BONGO CELEBRITY, NGURUMO, KULIKONI UGHAIBUNI!

8 comments:

emu-three said...

Anayeweza kutafsiri hizi taswira sawasawa ni moyo wa mtu. Mimi nilimuuliza mmoja wa waliokuja kwenye kampeni akasema kilichomleta ni kusikiliza nyimbo za Komba, mwingine, sijawahi kumuona mkuu wa nchi, mwingine, mimi nimeona watu wamejaa nikaona nami nijiunge, mwingine, ...ilimradi kinachowapeleka wengi sio `mada husika' ndio maana wajuzi wa hawa watu wakagundua na kutembea na watumbuizaji...lakini yote yahitaji pesa, kama huna pesa, hawatakujua, hutaweza kufikisha ujumbe wako kwa watu wengi na mwisho wa siku watadai hawazijui sera zako....mwenye nacho anafanya nini vile!!!??

John Mwaipopo said...
This comment has been removed by the author.
Anonymous said...

nakubaliana kwa kiasi fulani na emu-three lakini nikirekebisha kidogo ni kuwa hapo anaongelea mgombea wa ccm. ili kuweka rekodi sawasawa kwa upande wa CHADEMA hakuna hata mmoja anayekwenda kuangalia waimbaji/wanenguaji (maana sio wasanii. Hawajui hata gitaa linashikwaje). kama umewahi kuhudhuria mikutano ya chadema wataweka audio za kikabila ama ule wimbo wa 'slaa anaweza' basi, tena kwenye spika hafifu mno. mziki huu hauvuti watu kwani husikika mita chache tu. hapa ni wakati wa kumsubilia amalize mikutano kwingine na aje. anakuwa bado hajafika lakini unakuwa watu 'nyomi'. spika anazohutubia huja nazo kwenye ile canter na tayari hukuta hiyo nyomi.

nyomi hutokea vipi. wakati ccm hutumia uwezo wao kutangaza huko na huko siku mbili au tatu kabla kuwa mgombea atakuja, CHADEMA hawatangazi kwa kuwa hawana uwezo huo. watu hupigiana simu ama kutumiana meseji wenyewe kwa wenyewe. hujisafirisha kwa babasi wao wenyewe kutoka mifukoni mwao. hawapandishwi katika mafuso ili kujaa.(nadhani mmesikia ajali ya fuso pemba ya watu waliokuwa wanatoka mkutano wa ccm). Hawavalishwi kanga, tisheti na kofia kama wanawake wa ccm wanavyovalishwa kanga za kumnadi mume wa mwenzao

ninachotaka kukazia ni kuwa, ingawa sababu kama kufuata mkumbo nk zinachukua nafasi yake, katika mikutano ya kampeni CHADEMA hakuna burudani ya bure. ni kazi kazi tu. wanafuata mkumbo ni watoto tu. tena wagombea wa upinzani wakifika eneo husika wala hawapeani mikono na mtu. huwachukua chini ya dakika 5 kuapanda jukwaani. hicho ndiocho kinachoendelea

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

duhu ni noma, jamaa anakimbiza,swali ni je, walioshikilia mpini watamkubalia???

John Mwaipopo said...

saa ya mabadiliko ni sasa

Albert Kissima said...

Nipo Singida kwa sasa na wiki iliyopita nilipata fursa ya kutembelea baadhi ya vijiji vya hapa Singida. Nilishangaa kuona bendera za CCM zikipepea juu ya baadhi ya nyumba aina ya tembe(kuanzia paa hadi chini ni udongo) za wanakijiji. Kwa kweli kwa kuzingatia hali duni ya maisha ya wanakijiji na uwepo wa bendera zile ulinifanya niwaze mambo kadhaa.

Je, ni ishara ya kuwa wananchi wale wana tumaini kubwa na CCM baada ya tathmini fulani waliyoipitia au ni ushabiki tu?

Je, kama walifanya tathmini ya kina, ilihusisha hali duni ya maisha waliyonayo na wakaishia kuona kuwa CCM ndio kimbilio lao la mwisho?
Je, kuna uwezekano bendera zipo tu kama urembo au ni wakereketwa au wanachama hai?
Niliwaza pia kama bado wapo kwenye zama za Mwalimu. Zama ambazo haikushangaza kuona watu pamoja na umasikini wao walijitolea kwa hali na mali katika kumuunga mkono Mwalimu Nyerere kwenye harakati halisi za kuleta maendeleo ya jamii nzima na taifa kwa kuchangia kile kidogo walicho nacho. Wananchi hawa ndio hao wanaoteseka kwa shida ya maji, nauli ya kutoka walipo hadi sehemu muhimu itakayoweza kuwapatia mahitaji yao muhimu(mjini) ni shilingi elfu nne, kiasi ambacho kingepungua sana kama barabara iwaunganishayo na mji ingekuwa katika kiwango kizuri, ndio wananchi waziangaliazo nyaya za umeme zikipita juu ya nyumba zao za tembe na kuelekezwa kwingine. Binafsi naona ingekuwa ni zama zile za Mwalimu ningewaelewa lkn si zama za serikali ya Kikwete.

Au wamesharidhika na hali halisi ya maisha yao na wanahisi wameshafika, au ni elimu ya uraia wameikosa(hili lawezekana kabisa) kiasi kwamba wameshindwa kuwa na uchambuzi sahihi utakaowawezesha kumchagua kiongozi sahihi (hili la kukosa elimu ya uraia kwa asilimia kubwa ya watanzania pengine ndilo linalopelekea umati mkubwa wa tu kwenye mikutano ya kisiasa isitofautiane na umati ule wa mabonanza ya bongo fleva).
Mwisho, ninawaza kama ni ushabiki au wanalo tumaini na chama au ni heshima ya chama, au labda ni nini?
Picha halisi kuipata ni vigumu lakini matokeo ya uchaguzi kama utakuwa huru na haki, utatupa jibu, kama tafsiri ya wingi wa watu kwenye kampeni za kisiasa hautofautiani na ule wa wingi wa watu kwenye mabonanza ya ubongo wa fleva, yani kama mikusanyiko ni ya kishabiki tu, itajulikana.

Lakini mpaka sasa tujiulize ni idadi gani ya watu ambao tayari wanahesabu kuikosa fursa ya kupiga kura kwa sababu ya kuwa mbali na sehemu walizojiandikishia kwa sababu ambazo ni nje ya uwezo wao na ambao ni miongoni mwa watu wanafanya mikutano ya kampeni kuonekana kufurika? Wanachuo wakiwa ni miongoni mwao? Je kuna suluhisho la hili?

haki itapatikana ukiwapo usimamazi wa kweli wa kura utakuwepo, nakujua nanikapiga, pia na mtangazaji matokeo pia awe mkweli vinginevyo yatajazwa majina ya chekechea kuongeza kura na mtangaza matokeo anaweza kufanya yaliotokea miaka ya nyuma kura za chama hiki kinapewa chama kingine