Saturday, June 11, 2011

MAHOJIANO: NOVA KAMBOTA NA ASKOFU SYLVESTER GAMANYWA

Kutokana na ombi la wadau kutaka kufanya mahojiano na viongozi wa dini kubaini msimamo wao kuhusu matamshi ya rais Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa dini kujiepusha na biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo yamezua hali ya taharuki nchini , tovuti yako hii imefanya mahojiano na Askofu Sylvester Gamanywa wa huduma ya Wapo Mission kuhusiana na msimamo wake kwenye jambo hilo pamoja na maswala mengine kama ifuatavyo;
Nova Kambota.
Askofu Sylvester Gamanywa
1.Baba Askofu umewahi kunukuliwa ukisema “gharama ya kuilinda amani iliyopo ni ndogo kuliko gharama ya kuirudisha amani ikishapotea” je kimsingi una maana gani baba Askofu ?

JIBU
Maana yangu ilikuwa ni kuitahadharisha jamii itafakari kwa kina kuhusu matokeo ya kuvunjika kwa amani. Hakuna uamuzi usiokuwa na gharama. Uamuzi wa kuivunja amani una matokeo kinyume na kuwepo kwa amani yenyewe. Matokeo hayo kinyume ni pamoja na kupanda kwa gharama za maisha, kwa sababu uzalishaji pamoja na huduma za kijamii zinazotolewa wakati wa amani vitakoma, na jamii italazimika kujitafutia njia mbadala za kujikimu ambazo zitakuwa ni ngumu na aghali sana.
Hapo sizungumuzii suala la kuongezeka kwa majeruhi wa vita na machafuko ambayo wahusika pamoja na kuachishwa uzalishaji; lakini watahitaji tiba ambazo ama hazitakuwepo kabisa, au zikiwepo zitakuwa ni aghali hazinunuliki, matokeo yake ni wengi kupoteza maisha au kuwa na vilema vya maisha.
Si hayo peke yake, hata juhudi za kujaribu kuirejesha amani iliyotoweka nako kutagharimu zaidi. Maana itatuchukua muda mrefu zaidi kuirejesha. Isitoshe, wapo wengine ambao hawatakubali amani irejee kwa sababu tu wananufaika na mazingira ya vita na machafuko.
Sasa basi, kwa mwananchi wa kawaida ambaye mpaka hivi, katika mazingira ya utulivu bado maisha yake ni shida tupu; je! hali yake ya maisha itakuwaje pale ambapo gharama za maisha zitapanda ghafla na kudumu kwa muda usiojulikana wa kutokuwepo kwa amani? Nilitaka jamii ilitafakari hili.

2. Uhuru wa vyombo vya habari unaongeza uelewa miongoni mwa wananchi na pia unachochea tabia na mienendo ya wananchi kiasi kwamba kumeibuka hali ya vuta nikuvute baina ya viongozi na wananchi, je unaliongeleaje hili? Unadhani ni kweli kuna uhuru wa habari? Una manufaa gani?

JIBU
Kuna tofauti kati ya kuwa na “uhuru wa habari” na “matumizi sahihi ya uhuru wa habari”. Tukifanya tathmini kuanzi miaka 20 iliyopita, (kwa sisi tulioshuhudia mwanzo wa uhuru, azimio la Arusha mpaka Azimio la Zanzibar), hakuna wa kubisha kwamba Tanzania tunao uhuru wa habari. Hata kama uhuru wenyewe sio asilimia mia moja, lakini upo tena unaotushinda hata kule kuutumia ipasavyo.
Tatizo kubwa tena linaloelekea kuwa sugu ni dalili za kuwepo kwa “matumizi yasiyo sahihi ya uhuru wa habari”. Bila shaka, tatizo hili linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira mapya ya utandawazi, uchanga wa uwezo wa umilikaji wa vyombo vya habari pamoja na ukiukwaji wa maadili ya habari.
Kwa hiyo, kile kinachoonekana kuwa ni “hali ya vuta nikuvute baina ya viongozi na wananchi” hakikusababishwa na kuwepo kwa uhuru wa habari bali matumizi yasiyo sahihi ya uhuru wa habari.

3. Wewe kama mmoja wa wadau wa maadili kwenye taifa, je umelipokeaje swala la baadhi ya wabunge kutaka kupigana bungeni? Na una ushauri gani?

JIBU

Kwanza, bado tunapaswa kukumbuka kwamba demokrasia yetu bado ni changa. Pili, kwa mujibu wa taratibu za kuwapata viongozi wa kutuwakilisha katika ngazi za udiwani, ubunge hata urais, maadili kama maadili katika maana yake halisi bado si kigezo kinachopewa uzito unaostahili. Tafuta mwenyewe uone sifa za mtu kugombea nafasi ya uongozi katika ngazi husika, sifa ya maadili haimo.
Kwa hiyo, si ajabu kama kutajitokeza dalili za ukiukwaji wa maadili katika Nyanja za uongozi. Ni vema tukumbuke kwamba mlango wa kukiukwa kwa maadili umeachwa wazi tangu awali kwenye sifa za kuwapata viongozi katika ngazi husika. Hapa itabidi tusubili ujio wa katiba mpya pengine tutapata ufumbuzi wakati huo ukifika. Nikiwa na maana kwamba kigezo cha maadili kama mojawapo ya sifa ya kupata viongozi kitazingatiwa kikamilifu.

4.Rushwa umekuwa ni mwiba sasa kwa taifa letu licha ya kazi za TAKUKURU na sheria zilizopo, je nini nafasi ya viongozi wa dini katika kupambana na rushwa?

JIBU
Hili ni swali zito na muhimu. Siwezi kulijibu kwa haraka na kwa ufupi katika jukwaa lako. Linahitaji mjadala mzito, tena wa kuwahusisha kikamilifu viongozi wa dini. Nasema hivi kwa sababu rushwa sio tu kuwekewa TAKUKURU na sheria za nchi, lakini pia imeandikwa katika misahafu ya dini zetu.
Nafasi pekee ya viongozi wa dini, katika kupambana na rushwa, ni kurejea upya maagizo na sheria zilizomo katika misahafu ya dini husika. Kipaumbele kisiwe kukomea katika kukemea rushwa katika jamii, badala yake uzito mkubwa uelekezwe katika kurejesha maadili ya kiimani ambapo rushwa inatafsiriwa kuwa ni dhambi mbaya na hatari hivyo lazima iogopwe.
Kila mwamini aelimishwe bayana kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa dhambi ya rushwa ni Jehanamu ya moto. Pasipo mtu kuwa na hofu ya Mungu siku ya kiyama hakuna silaha itakayofaulu katika kudhibiti rushwa.

5. Kumekuwa na tuhuma za baadhi ya viongozi wa dini kutumiwa na wanasiasa nchini kufanikisha malengo yao, je wewe kwa upande wako limewahi kukukuta? Na je ni kweli lipo hili au ni uzushi tu?

JIBU
Mimi nami nimezisikia kama wewe. Kwa kumbukumbu zangu binafsi zijawahi “Kutumiwa na siwezi kutumiwa” na wanasiasa kwa malengo yao. Kila mahali popote niliposhirikiana na viongozi wa kisiasa chimbuko lake ni ubunifu wangu na ushawishi wangu kwao na kunipa fursa ya kutimiza malengo ya wito wangu kwa Mungu na kwa taifa. Siwezi kuwasemea wengine katika hili sababu sina ushahidi wala uthibitisho.

6. Matumizi ya mabavu dhidi ya wananchi hususani kutoka kwa vyombo vya usalama limekuwa ni tatizo siku za karibuni, je wewe kama kiongozi wa kiroho na mwananchi unaliongeleaje hili?

JIBU
Tatizo la msingi katika hili haliko kwenye vyombo vya usalama wala jamii. Tatizo liko kwenye mfumo uliopo wa mahusiano kati ya pande husika. Mfumo huu unaweza kurekebishwa vizuri pale ndoto za katiba mpya zitakapotimia.

7. Rais wa Jamhuri ya Muungano amewataka viongozi wa dini kujiepusha na biashara haramu ya madawa ya kulevya tena ameonya kuwa baadhi ya viongozi wa dini wanajihusisha na biashara hii haramu na baadhi ya viongozi wa dini wakaja juu wakimtaka athibitishe madai yake kwa kuwataja wahusika, je! wewe unalipokeaje hili?

JIBU
Hili nimelipokea kama bomu ambalo limelipukia kwenye kambi ya madhehebu ya dini. Hii ni kashfa nzito. Aliyeiweka hadharani ni mtu mzito, mkuu wa nchi mwenye vyombo vya dola. Wenzangu wamesema lakini mimi bado natafakari kwanza. Nasali kwa Mungu anipe ufunuo wa lipi niseme, niseme kwa nani na ili iweje.

8. Tiba ya Loliondo imekuwa ni moja kati ya mambo yaliyovuta hisia za viongozi wa dini huku baadhi wakipinga na wengine wakiunga mkono, je wewe kama mmoja wa viongozi wa dini unaliongeleaje hili? Na upi msimamo wako katika tiba ya Loliondo?

JIBU
Tangu habari hizi zianze kupewa uzito wa pekee na vyombo vya habari, kila nilipohojiwa jibu langu lilikuwa moja, “nafanya utafiti”. Kusema kweli mpaka sasa bado nafanya utafiti. Utafiti ninaoufanya ni kujua kwa hakika kwa kupitia maandiko matakatifu ya Biblia kama bado Mungu anatoa mafunuo na maagizo ya tiba kupitia dawa, vitambaa, maji ya Baraka, nk. Nikikamilisha utafiti wangu nitasema wakati huo. Msimamo wangu utajengwa kwenye taarifa ya utafiti ninaofanya hivi sasa.

9. Mihadhara ya kidini imekuwa sio tena sehemu ya kufundishana dini bali kukashfiana na pole pole uvumilivu wa kidini umeanza kutoweka, je unadhani kuna haja ya kupiga marufuku mihadhara ya kidini?

JIBU
Nani apige marufuku na kwa mamlaka ya nani? Je! Huu si ndio uhuru wa kuabudu na kueneza imani kwa mujibu wa haki za binadamu? Haya ni maswali yanayogongana akili mwangu lakini si majibu ya swali lako. Majibu ni kwamba, katiba mpya ndio ufumbuzi wa hii mitafaruku ya kidini ambayo inaonekana kuwa kero.
Unaweza kucheka kila ninapojibu kwa kutaja hoja ya “katiba mpya”. Lakini nina maana kamili katika kujibu hivi. Nami nimejiandaa kushiriki kikamilifu na uzito wangu utajikita katika nafasi ya “Haki na Uhuru wa kuabudu na kueneza dini; pamoja na mahusiano yanayotakiwa kuwepo “kikatiba” kati ya dini na serikali.

10. Mwisho kabisa baba kwenye changamoto lukuki kama maandamano ya CHADEMA, ugumu wa maisha, malumbani ya wanasiasa, migomo ya vyuo vikuu na ajali za barabarani za mara kwa mara zinazolikumba taifa letu nini mtazamo wako, maoni na ushauri wako kwa viongozi wa dini, serikali na jamii kwa jumla?

JIBU
Majibu yangu, mtazamo wangu, na ushauri wangu kwa viongozi wa dini, serikali na jamii kwa jumla ni kuwa na “katiba mpya”! Asante sana mhariri.


Nova Kambota ni mmiliki wa blogu ya NOVA TZDREAM ama LIBENEKE LA WANAMZUMBE na waweza kumtembelea kwa kubofya hapa

1 comment:

Goodman Manyanya Phiri said...

Siasa katika dini ndio sababu mimi siendi kanisani; na maiti yangu italiwa na funza jalalani ikibidi mpaka hapo nikiwapata viongozi wadhehebu au imani yenye kuitika "NAAM" au "HAPANA" na sio kutubabaisha sisi Waafrika katika hali ngumu tulionao leo ya kuletewa na wakoloni madawa ya kulevya watoto wetu kama sio kuletewa vijidudu vya ukimwi wakati wengine bado "wanamwomba Mungu" awaeleze eti kweli bomu limeripuka au la!



Naam, Mkuu! Kwa maoni yangu, Askofu huyu (kwa heshima lakini), anacheza mchezo wakisiasa pale anapoulizwa juu ya madai yake JK.


Kwanini adai yeye anamwuliza kwanza Mungu ampe jibu kwa swali kuhusu madawa ya kulevya kanisani? Kwani Mungu hakumpa yeye Baba Askofu akili kusudi atumie? Mbona Yesu alipoambiwa na Shetani aache mikate ya duniani bali atengeneze ya kwake kwa kutumia mawe, alikataa (ikiwa na maana kile Mungu aliekupa kama akili ukitumie na usikidharau nakwenda kumomba Mungu kingine kwa kudai wewe ni Mtakatifu au Mtoto Wake)?


Mimi naona Baba Askofu (tena kwa heshima kubwa) anaogopa tu akisema ukweli (na kuitika "Ndio, JK, wapo baadhi yetu!")atakosana na hao viongozi wadini wanaofikiriwa kuuza hayo madawa ya kulevya na huenda wakamdhuru. Sasa uoga na imani haviendi pamoja kamwe!


Baba Askofu pia anaogopa akidai "Hamna kitu kama kilivyosemwa na JK", wengi wafuasi wa dhehebu lake wataacha kuhudhuria kanisa kwani watamuona mwongo yeye mwenyewe, kwani yaliesemwa na JK ni kitu kinachojulikana kotekote Barani Afrika hasa ya Kusini, sio Tanzania tu!


Haya basi, Baba Askofu, endelea kumwomba Mungu akupe jibu. Lakini sisi tumekwisha kukuambia: watu hao kama alivyosema Mkuu Wanchi wapo kama kawa. Bomu unaedai wewe limeripuka kanisani ni moja tu: ile mantiki yako ya kudai hayo yote unayasikia mara ya kwanza leo kwa JK!