Tuesday, September 16, 2008

JUNGU KUU


Mwaka 2005 nilipata bahati ya kusoma makala haya toka kwa Ndesanjo Macha hata kabla sijajua "uchawi" wake katika masuala ya Blogs. Bado ninasoma na kusoma na ninaona kuna changamoto nyingi za kufanyia kazi hasa katika jamii hii ambayo sio tu inasahau kwao, lakini hata yale machache ambayo yanajulikana yanapingwa na wanajamii wenyewe. Ametukumbusha juu ya uthamini wa tamaduni na desturi zetu na kunyambulisha namna tunavyodharau vile ambavyo kwa hakika ni kama vyetu.
Kama hukuwahi kusoma hii, soma yote uone CHANGAMOTO YETU kwa jamii yetu toka kwake NDESANJO MACHA

SOMA ANGA, MAWINGU, NYOTA KAMA VILE KITABU

Katika gumzo la wiki iliyopita niligusia kidogo busara na maarifa ambayo tumerithi toka kwa waliotutangulia. Nilikuwa nikiwataka vijana kubeba jukumu la kuongea na wazee wetu ili tusipoteze busara na maarifa hayo. Nikasema kuwa wakoloni walipokuja hawakuchimba kwa undani falsafa na tamaduni zetu. Na wale waliofanya hivyo, walishindwa kutuelewa kwa undani maana, kwanza walikuwa wanatudharau sana, na pili, walikuwa wakiamini kuwa tamaduni zao zilikuwa ni bora zaidi. Wao walikuwa wastaarabu na sisi tulikuwa ni washenzi.
Kwa kuwa waliamini kuwa tamaduni zao ni bora walitumia silaha mbili kuu za kufunga watu minyororo ya utumwa wa akili: elimu na dini. Wakatumia elimu na dini kutusahaulisha yote tuliyokuwa tumerithishwa. Historia yao ikawa ndio yetu. Utamaduni wao ukawa wetu, imani zao zikawa zetu. Watakatifu wao wakawa watakatifu wetu. Kumbukumbu zao zikawa kumbukumbu zetu. Urithi wao ukawa ndio wetu.
Wiki iliyopita niligusia pia hoja ya kuwa kuna mambo mengi ambayo walituletea wageni yanayofanana na mila na desturi zetu. Lakini pamoja na kufanana huko walidai kuwa tunayofanya sisi ni ushenzi na kinyume na mapenzi ya mungu. Niligusia suala la maji katika tamaduni za Kiafrika na katika dini ya kikristo. Maji yana nafasi ya pekee katika tamaduni zetu. Maji yanatumika katika tambiko na mambo mengine mengi ya jadi. Suala hili la maji, ukitafiti vyema, utagundua kuwa lina mantiki inayofanana dunia nzima. Wahindi, kwa mfano, wanaheshimu sana mto Ganges ambapo katika imani zao kwenda kuoga katika mto huo ni tendo muhimu sana la kidini na kiimani. Wakati wa sikukuu ya Maha Kumbh Mela, waumini wa imani za kihindu wanakwenda kuoga katika mto Ganges kwa ajili ya kujitakasa.
Waislamu kabla ya kwenda kuswali, lazima waguse maji. Wanatumia maji kuuandaa mwili tayari kukabiliana na Allah. Waumini wa imani ya Kitao (Tao: inatamkwa “dao”) wanaheshimu maji mno. Ukimtembelea muumini wa dini hii lazima akupe maji ya uvuguvugu unywe (sisi huwa tunampa mgeni soda). Wamasai nao, kwa mfano, wakitahiri watoto wanawapeleka kwenye maji baridi mapema alfajiri. Wiki iliyopita nilizungumzia maji kwenye ukristo nikasema kuwa wakristo “wanazaliwa mara ya pili” kwa maji. Nikaongelea na kitu kiitwacho “maji ya uzima,” na pia muujiza wa kwanza wa Yesu uliohusisha maji.
Miili yetu nayo asilimia kubwa ni maji, na dunia yetu vilevile sehemu kubwa ni maji. Mtoto anapokuwa tumboni kwa miezi tisa anakuwa ndani ya maji. Yesu alipokuwa akifundisha wanafunzi wake aliwasafisha miguu kwa maji na kuwataka wafanye hivyo wao kwa wao. Maeneo yanayopendwa sana na watu ni maeneo yaliyoko ufukweni (yaani karibu na maji). Mwisho wa wiki tunakwenda kupumzika ufukweni, wenye mali wanajenga nyumba zao ufukweni, hoteli kubwa za kitalii zinajengwa ufukweni.
Siri hii ya maji mababu zetu walitufundisha. Waliijua. Wengi tumesahau somo hili na mengine mengi ndio maana nikawashauri vijana wanaoniomba vitabu vya historia yetu waende kuongea na wazee. Wakajifunze wazee wetu waliyotufundisha, kwa mfano juu ya kuumbwa kwa dunia. Kuumbwa kwa dunia watu wengi wamekomea kwenye hadithi ya Adamu na Hawa. Kuna maelezo maelfu na maelfu duniani juu ya dunia ilivyoumbwa. Kila kundi la kitamaduni huku duniani lina maelezo na simulizi juu ya kuumbwa kwa dunia na viumbe vilivyomo duniani. Maelezo haya yote ni urithi wetu.
Je ni vipi busara za kale za waliotutangulia zinaweza kutupa majibu ya maswali yanayotusumbua leo? Kwanini tutafute maarifa haya ya kale toka kwa watu ambao hawakuwa na uwezo mkubwa wa kisayansi na kiteknolojia kama tulivyo hivi sasa? Kwanini tujifunze kwao wakati inaaminika kuwa dunia ya leo tumeendelea zaidi ya waliotutangulia? Kwani ni kitu gani walikuwa wanajua ambacho hatujui leo hii? Haya ni baadhi ya maswali ambayo tunaweza kujiuliza.
Hivi kukitokea ukame wa kutisha nchini Tanzania hivi sasa, Watanzania watafanya nini? Tutasikia viongozi wa dini wakihimiza waumini waende wakasali. Waislamu watakwenda msikitini na wakristo makanisani kumuomba mungu alete mvua. Kwa wale wanaosikiliza busara za mababu na mabibi zetu, kwenda makanisani na misikitini sio jibu. Kitendo hicho kinatufanya tudhani kuwa tumepata jibu la tatizo la ukame. Kumbe ukweli ni kuwa mvua hatupati za kutosha au kuna ukame kwa kuwa tumepoteza upendo wetu kwa mazingira yetu na sasa tunapata adhabu yake. Sala kuu ni kwenda kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji, na kuheshimu mazingira.
Unapoharibu mazingira yako, unapokuwa na imani ambayo imekazana kukwambia habari za unakokwenda baada ya kufa huku ukiwa hujui lolote kuhusu dunia unayoishi hivi sasa, dunia hiyo inakuadhibu kwa ukame na mambo mengine. Uharibifu wa mazingira ni sawa na kuishi katika ndoa isiyo na maelewano. Ndani ya nyumba yenye magomvi huwa hakuna furaha wala upendo. Binadamu nasi tuko katika ndoa kuu na mazingira yetu. Tumeoana na miti, mito, milima, bahari, wanyama, ndege, wadudu, n.k. Tukiharibu ndoa hii, hata tukisali kwa miaka elfu kumi, hata sala hizo zikiongozwa na maimamu wakuu kabisa, mashehe, maaskofu, mapapa, na makadinali, ukame hautatokomea. Ni mpaka pale tutakapotambua kuwa tumetia dunia majeraha. Dunia inavuja damu.
Tunakwenda kanisani na misikitini kuomba mvua, kisha tukimaliza sala tunarudi majumbani kuendelea kuharibu dunia kwa kuchoma misitu, kukata miti ovyo, kuharibu vyanzo vya maji, kutoheshimu misitu, matumizi mabaya ya maji, n.k. Kinacholeta mvua sio sala. Kama sala inaleta mvua, ina maana kuwa watu wanaoishi katika maeneo ya majangwa hawajui kusali? Au sala zao ina maana kuwa hazisikiki? Kama sala inaleta mvua, basi maimamu, mashehe, mapadri, wachungaji, maaskofu waende jangwa la Kalahari au Sahara wakasaidie kuwaombea mvua wanaoishi huko. Au waende Dodoma maeneo yenye ukame wakasali. Sala kuu ni kutunza ndoa tuliyonayo na mazingira. Hifadhi ya mazingira ndio ibada yetu. Kupanda miti ni sala. Haya yote walitufundisha waliotutangulia. Badala ya kwenda kanisani na misikitini, nendeni mashambani, maporini, mitaani kwenu mkapande miti! Lindeni vyanzo vya maji. Fufueni imani zilizokuwa zimejengwa juu ya falsafa ya ekolojia.
Ninachosema ni kwamba ukiharibu mazingira yako aliyokupa muumba wako ambayo ndiyo yanakuletea mvua, usidhani kuwa ukienda kumuomba mvua, basi hiyo mvua itaanguka kwa miujiza. Sayansi ya mvua tunaijua. Bila miti, bila maji, bila upepo, bila mawingu, hakuna mvua. Mababu zetu walijua hili. Wakatufundisha kuwa mazingira yetu ni kama sehemu ya miili yetu. Ukikata mti ovyo ni kama unakata mkono au mguu wako. Ukiharibu chanzo cha maji ni sawa na kutoboa jicho lako. Ndio walitufunza mababu na mabibi zetu. Kwa Waafrika kuheshimu mazingira ni sehemu ya ibada. Kwa hiyo sisi sio tu tunatakiwa kupenda majirani zetu kama nafsi zetu bali kupenda miti, wanyama, wadudu, misitu, maji, mto, n.k.
Wazee wetu wakatuambia kuwa miti ina uhai, wakatuambia tuiheshimu. Wakatuambia kuwa miti inatuletea mvua kwa hiyo inatuletea uhai, kwa hiyo tuiheshimu. Wakaja hawa mabwana na dini zao za kuja wakasema kuwa imani hizo ni ushenzi, wakaanza kutufunza imani zisizoheshimu mazingira hata kidogo. Wao wanachotaka tuzungumzie ni maisha baada ya kifo na kutoa sadaka. Imani za kitisho. Imani za kuhubiri moto wa jehanamu huku tukitengeneza moto hapa duniani kila siku.
Moja ya kosa kubwa tunalofanya ni kudhani kuwa kwa kuwa mabibi na mababu zetu hawakuishi katika ulimwengu wenye sayansi na teknolojia ya kileo, walikuwa hawafahamu sayansi. Usicheze na wazee wetu. Katika dunia ya leo, dawa ikigundulika lazima ijaribiwe kwa wanyama wanaowekwa maabara na kuchunguzwa kwa kipindi kirefu. Wanyama hawa wanateseka. Wanapasuliwa. Wanauawa. Mababu na mabibi zetu hawakuwa na maabara kama hizi lakini walijua dawa za magonjwa mbalimbali. Walijuaje? Walijuaje dawa hii inatibu kuharisha, dawa ile inasafisha tumbo, dawa hii inatibu majeraha ya moto, dawa ile inatibu kikohozi? Babu yangu, kwa mfano, alikuwa anajua dawa ya pumu. Waliomrithisha walijuaje bila kumpasua panya kama wafanyavyo wanasayansi siku hizi?
Usicheze kabisa na mabibi na mababu zetu. Acha kuwadharau. Nikikwambia kuwa mabibi na mababu hao ni visima vya maarifa au ni sawa na vyuo vikuu usichukulie sentensi hii kwa mzaha. Jiulize, vyakula unavyokula leo hii nani kakupa? Tazama vyakula vyote vya asili na faida mwilini. Kisha tazama vyakula vya “kileo” na kemikali, homoni, na sumu zake kila aina. Mababu zetu walijuaje kuwa embe, mapera, mapapai, machungwa, mananasi, vitunguu saumu, n.k. vinaliwa? Walijuaje kuwa mchele, mahindi, maharage, giligilani, kabichi, matoke, viazi, mdalasini, ni vyakula vinavyofaa kuliwa? Walijuaje wakati hawakuwa na maabara ya kufanyia majaribio kwanza?
Wazee wetu walijifunza sana toka kwenye mazingira yao. Wakatufundisha kuwa lazima tujifunze toka kwa wanyama, nyota, anga, upepo, n.k. Unaona jinsi ambavyo makabila yanayoishi maporini huko Asia yalivyoepuka jangwa la tsunami hivi karibuni. Makabila haya na wanyama waliepuka kwa kukimbilia sehemu za milimani. Yale makabila ambayo shughuli yao kubwa ni uvuvi siku hiyo hawakwenda kuvua, walikuwa milimani. Walijuaje kuwa kuna janga linakuja? Hawakuwa na mitambo ya kisasa ya kutabiri hali ya hewa. Walijuaje?
Mazingira yetu ni mwalimu mkuu, walitufundisha waliotutangulia. Wazee wetu walituambia kuwa mito au maporomoko ya maji ni kama wimbo. Ukisikiliza wimbo huo utasikia sauti ya muumba. Unapokwenda mtoni, au kutazama maporomoko ya maji, au mawimbi baharini, sikiliza. Ukisikiliza vyema utasikia sauti hiyo.
Wakatufunza pia kuwa mawingu na anga ni kama kitabu. Wazee wetu walikuwa wakisoma mawingu kama vile mtu anasoma kitabu. Kumbe anga ni kama kitabu kimoja kikubwa. Kumbe tunaweza kutembea juu ya nchi tukitafuta vitabu huku juu ya vichwa vyetu tumezungukwa na kitabu cha siri ya dunia. Kule Afrika Magharibi kuna kabila linaitwa Wadogoni. Kabila hili limekuwa likijulikana kwa elimu waliyonayo kuhusu nyota. Wadogoni kwa miaka mingi wamekuwa wakiitaja nyota ya Sirius katika simulizi zao. Wanasayansi kinachowashangaza ni kuwa sayari hii haionekani kwa macho ya kawaida. Wadogoni waliijua sayari hii kabla wanasayansi wa magharibi hawajatengeneza vifaa vya kuona sayari na nyota za mbali. Wamisionari na wageni wengine walipokwenda kwao waliwaambia kuwa imani zao walizorithi za elimu ya nyota ni ushirikina na ushenzi.
Wengi wetu hadi leo tunawashangaa wamisionari hawa. Wakati wanawaambia Wadogoni kuwa elimu yao kuhusu nyota na mahusiano ya nyota na maisha ya binadamu hapa duniani ni ushenzi, wamisionari hao walikuwa na kitabu, yaani biblia, ambacho kinazungumzia kuzaliwa kwa mwokozi, Yesu. Kati ya watu wa kwanza duniani kujua kuwa kuna mwokozi aliyezaliwa walikuwa ni mamajusi. Mamajusi walijuaje kuwa kuna mwokozi kazaliwa? Walielekezwa na nyota ya mashariki! Kitendo cha kutoelewa Wadogoni, wamisionari hawa inaelekea pia hawakuelewa habari za mamajusi sawasawa.
Ndio maana nawaambieni mambo haya ninayosema msichukulie kuwa ni mzaha. Kama nyota ziliongoza watu kwenda alikozaliwa Yesu. Kama nyota ziliweza kutoa ujumbe kwa wale wenye elimu ya nyota kuwa kuna kiumbe wa pekee aliyezaliwa duniani, elimu ya Wadogoni juu ya nyota na mahusiano yake na maisha yetu sio elimu ya kuitupilia mbali kwa kuwa eti wao sio wakristo. Hizi ndio busara za waliotutangulia ninazozungumzia.

mtambue kwa kubofya http://www.jikomboe.com/?page_id=1247

No comments: