Monday, August 25, 2008

Mwaka tangu onesho la mwisho la Lucky Dube. Ujumbe wake utaishi milele



Usiku wa tarehe kama ya leo mwaka mmoja uliopita nilibahatika kuhudhuria onesho moja la muziki ambalo kama lilivyo tukio jingine lolote, liliingia katika rekodi yake maishani mwangu. Mosi, lilikuwa kati ya maonesho mengi ya "live" niliyohudhuria. Pili, lilikuwa kati ya maonesho machache ambayo ningeweza kuendelea kuangalia hata kama angesema anaanza upya tena kwa nyimbo zilezile na Tatu kwa bahati mbaya saana likawa ni onesho la mwisho kumshuhudia nyota wa muziki wa Reggae kutoka Afrika Lucky Philip Dube akituonesha kile ambacho amejaliwa kukitumia kwa miaka mingi kueleza hisia zake na za wengi katika suala zima la Haki za wanawake na watoto, Siasa, Mapenzi, Ubaguzi, Mfumo wa maisha upumbazao wengi, Imani na hata maovu mengi yaliyopo na yanayoendelea kuwepo ulimwenguni.
Nikiufikiria usiku huo bado nakuwa na fresh image ya kazi njema aliyoifanya katika kuwaunganisha watu wa mataifa, lugha, rangi, asili na imani tofauti kwa kutumia muziki wa Reggae. Akilishambulia jukwa sambamba na kinamama watatu aliokuwa nao, Lucky alionesha utaalamu katika upangiliaji wa muziki, ushambuliaji wa jukwaa, ushirikishaji wa hadhira na mwisho uwasilishaji wa ujumbe uliokuwepo ktk nyimbo zake. Alituimbisha nyimbo zake zilizorudiwa vema na wahudhuriaji hasa ule wa Ding Ding Licky Licky Bong ambao una kile alichokiita "Rasta Kwasa".
Lucky atakumbukwa kwa mawazo yake ktk mambo mengi kama Haki za watoto [ Little Heroes, Children in the street,Love Me (the way i am), You know (where to find me), Think About The Children, na nyingine] na pia katika masuala ya maisha ya kawaida na hali waishio wengi waliosahaulika katika jamii za chini. Pia aliimba kuhusu maovu yanayoendelea katika jamii. Katika wimbo wake wa Crime and Corruption uliopo kwenye albamu yake ya The Way It Is, Lucky aliimba juu ya maovu yanayoendelea katika jamii ambayo kwa bahati mbaya ndiyo yaliyomkuta kama alivyoyaimba. Aliuliza kama viongozi wameshawahi kuhofia kuporwa gari tena mchana kweupe, ama kama wameshawahi kuhofia kuondoka nyumbani kisha wakarejea wakiwa kwenye jeneza huku kichwa kikiwa na risasi (akimaanisha kuuawa). Na ndicho kilichomtokea. Na ndio maana leo hii naandika haya nikimkumbuka moja kati ya nyota walioeleza mawazo yao kwa lugha laini, hadithi ama taarifa kamili na kwa midundo iendanayo na maudhui.
Mengi juu yake yatakuja katika kuadhimisha mwaka mmoja wa mauti yake hapo Oktoba.
Sikiliza wimbo CRIME AND CORRUPTION ambacho ni kwa wale wote wenye mamlaka lakini wanatumia mamlaka hayo kujilinda na kujitenga na jamii na ndio maana hawana hisia halisi za maovu yatokeayo jamiini.

No comments: