Tuesday, September 30, 2008

Ni kipi tulichopoteza kwenye muziki wetu kisichorejesheka?

Komandoo Hamza Kalala. Unakumbuka solo yake akiwa Vijana, Washirika na Bantu ya mwanzo?
Hussein Jumbe alipokuwa Sikinde na Msondo si sawa na yule aliyekuwa TOT.

Miaka inavyozidi kwenda ndivyo teknolojia inavyoongezeka ama kukua na kuonekana kurahishisha utendaji kazi katika nyanja mbalimbali. Muziki kama sehemu ya maisha ya wengi, nao umeathiriwa kwa namna moja ama nyingine na mabadiliko na ukuaji wa teknolojia ambayo imeufanya uweze kuwa wa kisasa na wenye kutengenezwa kwa muda mfupi, ubora wa hali ya juu na pia gharama za chini kiasi kutokana na vyombo vya kisasa katika kuzalisha ama kutengeneza muziki huo.
Lakini hili halionekani kuwa na ukweli katika aina zote za muziki ama muziki toka sehemu zote maana kwa mtazamo wangu naona kama muziki wa Tanzania sasa unazidi kupoteza dira kwutokana na "uvivu " wa watayarishaji na wasanii wenyewe. Naliona hili katika mambo kadhaa ambayo naamini si vibaya kuyaweka bayana katika kusaka suluhisho la hii changamoto yetu inayotukabili.
Ubora wa muziki na wanamuziki unatofautiana saana ukilinganisha sasa na zamani. Hapa ni kuanzia muda wanaoweza kufanya ama kutumbuiza jukwaani bila kuchoka ama kukaukiwa sauti. Pengine ni kutokana na kutofuata maadili na kuendekeza vilevi ambavyo vinaathiri saana undani wa njia ya sauti huku wakiacha mazoezi na matokeo yake kudhoofisha sauti na uwezo wao katika kutumbuiza bila wao kujua. Pia "kupea" kwa tunzi nyingi za sasa ambazo mara nyingi zinakuwa na ujumbe mfupi, mwepesi na usiopigania hali halisi ya mtanzania wa kawaida huku wakiendekeza anasa na kutajana majina na kisha kuwekeza mkazo katika vibwagizo ambavyo kutokana na ukosefu wa zana halisi za muziki vinakosa mvuto wa hisia na matokeo yake kupoteza kila kilichokusudiwa. Kuna mifano ya wasanii ambao walipata kuvuma na bendi za zamani na wakachoropoka kupiga ule uitwao muziki wa kisasa ambao umewatoa katika ramani ya muziki. Nyota kama Komandoo Hamza Kalala aliyejenga heshima sana akiwa Vijana na hata Washirika Tanzania Stars na miaka ya mwanzo ya Bantu Group lakini alipoingia na style ya kikongokongo kusaka maslahi tunaona alivyoporomoka mpaka watu kutokumbuka albamu kama Ngozi ya Kitimoto. Hata Marehemu Eddie Sheggy, Mhina Panduka na Hussein Jumbe ni baadhi ambao wanakubalika katika nyimbo zao wakiwa na bendi zinazopiga muziki halisi kuliko walipokuwa Bantu (Sheggy), TOT (Panduka na Jumbe).
Matumizi ya zana / ala za muziki kwa sasa yanapoteza uzito wa muziki. Kutaka kupiga muziki wa ki-Tanzania kwa kutumia kinanda (keyboard) pekee kama wafanyavyo baadhi ya wasanii chipukizi (ktk mahadhi yote) kunapoteza saaana "rythim" yake. Ukisikiliza miziki ya Zouk, Bongo Fleva na mingine ya kutengenezwa kwenye vinanda unaona mapungufu mengi kwani kisicho halisi chajidhihirisha. Wanakosa na kushindwa kutumia "percussions" halisi na hata kushindwa kushirikisha "wasanii huru" katika zana mbalimbali kama Trumpet, Saxaphone, Marimba na vingine vinavyoongeza ladha ktk miziki.
Maudhui katika tunzi za sasa mengi ni kulingana na matukio ambayo kwa hakika ni ya muda mfupi. Wapo wanaoimba na kuvuma kwa kuimba kuhusu ugomvi wak na wapenziwo halafu ukifika wakati wimbo unakuwa katika kile wanachoita "kupanda na kushika chati" unakuta wapendwa hawa wamesharejeana na wanapanga kuoana. Hapo utaona hata mwenye wimbo hataki tena kuusikia maana ujumbe si halisi tena. Nafikiri kuna MATATIZO NA MAHITAJI ya miaka mingi aya mTanzania mabyo wasanii wanaweza kuyagusa na kuyaweka bayana na wimbo utaendelea kuwa na ujumbe uleule mpaka matatizo hayo yatakapokwisha. Hapo ndipo msanii anapokuwa "mpiganaji" na SAUTI YA JAMII. Si unakumbuka nyimbo kama Ndoa ya Mateso (Dar Jazz), Mama wa Kambo (Vijana Jazz), Usia kwa Watoto (Juwata Jazz) na nyingine nyingi ambazo ujumbe wake uko palepale kama ulivyokuwa wakati zinaandikwa na kwa sababu walieleza yaliyokuwa na yanayoendelea kuikumba jamii.
Msimamo katika muziki unatofautiana na licha ya kila mmoja kufuata maslahi, wapo wanaoshindwa kuonesha walipo katika kutafuta pesa. Ni ajabu kuwa wasanii wanaangalia nini wananchi wanataka ndio wajaribu kuwa wabunifu na matokeo yake ni kuwa wanakosa msimamo maana kila waendapo wanataka kuiridhisha hadhira jambo ambalo haliwezekani na ni dalili mojawapo ya kuporomoka.
Malipo katika muziki kwa sasa ni mazuri kiasi na naamini ndio maana kunakuwa na mamluki kuliko halisia.
Napenda kusema tena kuwa haya ni kwa asilimia kubwa ya wasanii na najua na naheshimu wale wachache wanaoendeleza kazi njema ya KUBURUDISHA, KUELIMISHA NA KUIKOMBOA JAMII KATIKA YALE YAWASIBUYO.
Hii ni CHANGAMOTO YANGU na ni namna ninavyoliona tatizo la muziki wa nyumbani. Pengine waliona tofauti maana kama lilivyo jina la blogu hii "namna uonavyo tatizo ndilo tatizo"

Blessings

No comments: