Wednesday, October 8, 2008

Filamu ya Richmond yaja: Naanza kuhisi vitakavyonikera

Denis Sweya (Dino) kushoto na Deo wa Dollwood
Picha toka www.fullshangwe.blogspot.com

Katika gazeti tando la Kaka Bukuku la Full Shangwe, kuna habari juu ya makamilisho ya filamu ya Richmond ambayo kwa mujibu wa Mtunzi wa filamu hiyo na muigizaji wa filamu Dennis Sweya (Dino), itazungumzia masuala ya unyanyasaji, dhuluma na rushwa iliyokithiri. Bofya http://fullshangwe.blogspot.com/
Ni kwa mujibu wa Dino huyohuyo, kuwa filamu hiyo itakayozinduliwa mwezi ujao imepigwa picha zake katika mikoa ya Arusha na Dar-Es Salaam. Hapa napenda kumpongeza msanii Dino kwa hatua aliyofikia ya kuweza kuandika filamu, kuitafutia washiriki ama waigizaji, kampuni ya kupiga picha hizo, uhariri na maandalizi yote yanayotakiwa mpaka kuja kuiingiza sokoni. Ni hatua moja mbele kuelekea mafanikio ya kisanii, lakini kuna mambo ambayo nahisi yataniketa katika filamu hii.
1: Najaribu kuoanisha maudhui yaliyotajwa na jina la filamu hiyo kuona kama itakuwa ikimtetea na kubainisha matatizo yamkumbayo mTanzania halisi ama itakuwa ni katika kutafuta jina litakaloweza kuuza kulingana na kashfa iliyokuwa na ambayo inafifia katika taifa letu. Hili naliona kama "kukurupuka" kwa kuwa siamini kama mtu anayetaka kuzungumzia unyanyasaji, dhuluma na rushwa iliyokithiri nchini Tanzania atatumia jina hilo. Kama hakutakuwa na ufafanuzi wa haja wa namna lilivyotumika Richmond kueleza unyanyaswaji, dhuluma na rushwa iliyokithiri katika nchi ambayo sidhani kama kuna mtaa wenye jina hilo, basi hii filamu itanikera
2:
Kama kuna kitu kinachoitwa unyanyasaji, dhuluma na rushwa iliyokithiri, basi kunahitaji uchunguzi na ufuatiliaji uliotukuka kuweza kuweka yote baya. Tukumbuke kuwa Filamu ni sehemu ya kuonesha matatizo na pia suluhisho kwa jamii inayohusika. Kama filamu hii haitaeleza matatizo yaliyochunguzwa na kuonesha namna ya kutatua basi itanikera.
3: Nilishaandika juu ya uvivu wa wasanii katika kutumia sanaa ambayo sio tu wanaimudu, lakini pia wamepata nafasi ya kuweza kuitumia kuiwakilisha jamii. Lakini wanaendelea kung'ang'ania maeneo ambayo kila mmoja anatambua mazuri na mabaya yake. Naamini wapo (na namaanisha wengi) wanaofahamu unyanyasaji, dhuluma na rushwa zilizopo Arusha na Dar kuliko zitakazooneshwa katika filamu hiyo. Kuna wengi walio vijijini (kuanzia Nanjilinji mpaka Rubafu) ambao wanadhulumiwa, kunyanyaswa na kutopata huduma zozote bila kutoa rushwa. Kama filamu hii haitagusa matatizo waliyonayo kinamama vijijini ambapo wanapoteza maisha kwa kukosa pesa ya kutoa rushwa, wanapigwa bila ya kuwa na mtetezi na wanakodhulumiwa pamoja na watoto wao na pia watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, filamu hii itanikera.
Huu ni mtazamo wangu na changamoto kwa wote wajiandaao kutengeneza filamu kuonesha matatizo ya waTanzania. Msipoenda vijijini ambako ndipo yalipo mtakuwa mnaonesha tunachokifahamu na itaonesha kuwa mnasaka pesa kuliko kujitahidi kutatua yale mnayoeleza kuwa ndio nia yenu kuu.

Kama jina la blog lilivyo (NAMNA UONAVYO TATIZO NDILO TATIZO) yawezekana nionavyo mimi ndilo tatizo japo naamini tatizo ni namna uonavyo nionavyo.
Blessings
See you "next Ijayo"

2 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

poa mzee, nimekutembelea na nimeipenda blog. keep it up, mambo mazito yanakuja. Thanx

Mzee wa Changamoto said...

Blessings K. Heshima kwako na kule kijiweni kwetu endeleza libeneke kama kawa.
Karibu