Monday, October 27, 2008

Kinachousibu muziki na sanaa ya asili nchini

Sisi Tambala waliporejea na kombe toka China

Kikundi cha Afrikali Ngoma Group
Hivi karibuni bloggers Michuzi Jr na Dada Sophy wameuliza swali linalorandana kuhusu muziki na ama wasanii wa miziki na kazi za asili. Sio hawa tuu, bali hawa ni wa karibuni ambao wameweza kuuliza maswali yaendanayo na hayo hapo juu. Kwa kaka Ahmad ameuliza juu ya mwenye dhamana ya kuuinua muziki wa asili nchini (BOFYA HAPA) ilhali Da Sophy yeye kauliza tunavyowaenzi wasanii wetu mahiri wa muziki wa asili kama kina Hukwe Zawose (BOFYA HAPA KUUNGANA NAYE)
Well, nilibahatika kushuhudia na kushirikiana kidogo na vikundi kadhaa vya muziki wa asili nikiwa nyumbani na vikundi kama Sisi Tambala (ambacho baadhi ya wasanii wake nimewaona Afrikali), Parapanda Arts, Simba Theatre na wengine kadhaa na nilipata ufahamu na uzoefu mzuri saana juu ya sanaa hii. Lakini ninapojiuliza kinachoisibu sanaa hii nzuri zaidi nchini naona makwazo katika sehemu kuu nne.
Kwanza SERIKALI ina dhamana ya kuendeleza utamaduni wetu (japo nimechoka kusema lakini sitokoma) na ina wajibu wa kujenga ukumbi wa kisasa kwa shughuli za sanaa ama kusimamia mkataba halali (na hapa napata shaka kidogo) utaowezesha wawekezaji kujenga ukumbi mwanana. Nakumbuka Rais Kikwete alipotembelea Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo mwanzoni mwa mwezi Machi 2006 na kuwapa changamoto ya kujenga ukumbi wa kisasa akisema kuwa ni aibu kuwa hatuna ukumbi wa kisasa. Bofya http://www.ippmedia.com/ipp/raha/2006/03/19/62374.html . Pia SERIKALI inastahili kuweka mwongozo wa usimamizi wa Chama ama chombo kitakachosimamia muziki na wanamuziki wa muziki huu kama ambavyo imefanya kwa FAT, TOC, TAA na vingine. Pia SERIKALI inastahili kusaidia katika mafunzo na uendelezaji kwa kozi na wataalamu wataowezesha wasanii na vikundi kujua namna nzuri ya kujiajiri na kuendesha shughuli zao. Kulipa Wakufunzi kama ambavyo imefanya kwa wengine kama Maximo
Pili ni WANANCHI ambao kwa namna moja ama nyingine wameingiwa na ule "utumwa wa kiakili" wa kuthamini na kusaidia kile kiachacho asili. Wananchi wanastahili kutembela vikundi na wasanii hawa kuona namna inavyowagharimu kutengeneza nyimbo na kazi zao ili waweze kuthamini kazi zao. Wananchi wengi hawahudhurii sanaa za nyumbani na inashangaza kukuta sanaa za nyumbani zinathaminiwa saana nje ya nchi ama na watu toka nje ya nchi huku watu wengi wakiendelea kushabikia mengi yabomoayo jamii kwa kuwa tu ni "maisha ama mfumo wa maisha ya kimagharibi" Nani anayewakumbuka Tatunane?Nani ameshawatembelea Simba Theatre, Wanne Star, Parapanda na wengine kuona kazi zao? Unadhani Ngoma Afrika wakija fanya onesho nyumbani watapata washabiki kama wafunikavyo Ujerumani? Uliona mapokezi kiduchu kulingana na kazi waliyofanya waliyopata Sisi Tambala waliporejea toka kwenye 7th China Folks Arts Festival ambako walipata ushindi wa Bara la Afrika na Ushindi wa jumla katika mashindano yaliyoshirikisha mataifa 22? Hadhira ya kiTanzania inastahili kuamka na kuanza kuthamini cha nyumbani kwanza.
Tatu ni VYOMBO VYA HABARI ambavyo kwa namna moja ama nyingine (vingi na si vyote) vimekuwa vikikimbilia kwenye mapato ya haraka hata kama hakumaanishi kuendeleza muziki, sanaa ama wasanii wetu. Vyombo vingi vya habari vimekuwa havitoi kipaumbele kwa sanaa na wasanii wa muziki na kazi za asili na hili limewafanya wale wanaotegemea kila kitu toka kwao kutopata habari kamili na sahihi kuhusu sanaa. Na kuna ambavyo hutoa habari zisizo sahihi kwa kuwa tu anayehabarisha hana ujuzi ama historia ama hisia na habari za sanaa. Na hii hufanya mengi mema yasitambulike kwa kuwa upeo wa mwandishi, mtangazaji na ama mtayarishaji ni mdogo katika hilo ashughulikialo.
Na mwisho ni WASANII wenyewe. Wasanii wanastahili kushirikiana kuanzisha ama kuendeleza Chama ama umoja wenye uhai na nguvu utakaowafanya watambulike na kuthaminika mbele ya jamii. Kuanzisha Tovuti (website) ama namna ya kisasa ya kuweza kuonesha kazi zao ulimwenguni na kisha kuwa na maelewano katika viwango vya maonesho. Kukiwa na kutoelewana, wapo watakaopata tenda kwa kuwa tu wako "cheap" na hiyo haimaanishi kuwa wanathaminika, ila wanapatikanika. Wasanii pia wanastahili kushikamana katika hili na kwa kufanya hivyo watakuwa na sauti kubwa katika jamii na vyombo vya habari, kisha watarejesha heshima yao, kazi yao na mwisho sanaa ya Taifa kwa ujumla.
Luciano alisema "never forget where we're coming from. Charge out your destination and let's use what we have for the uplift of the nation"
Hatujasahau asili yetu, malengo ni kwenye thamani ya sanaa hii na kwa wale waliopo kwenye sanaa kwa msaada wa wadau wengine twaweza kutumia kila tulichonacho kulinyanyua taifa katika sanaa hii.

Ni CHANGAMOTO YETU sote kuangalia tulipoanguka na kisha kurekebisha. Ndivyo nionavyo tatizo na yawezekana namna nilionavyo ndilo tatizo.

No comments: