Sunday, October 12, 2008

Wasanii kama "chombo cha starehe" cha serikali

Mawaziri wakuu Mhe Pinda (TZ) na Mhe Odinga (KEN) wakifurahia ngoma
Mfalme Mswati na Rais Kikwete wakiburudika na mganda


Mwalimu wangu wa Fasihi alipokuwa akinifundisha maudhui katika uchambuzi wa vitabu alizungumzia uchambuzi wa namna waandishi walivyoonesha na ama kukemea tabia za wanaume kwenye tamthilia hizo kuwatumia "wanawake kama chombo cha starehe". Na katika fafanuzi zake akasema pale unaposoma na pakaonesha kuwa mwanaume amemtumia mwanamke kutimiza matakwa yake (hata kama ni kwa ujira mdogo) basi anakuwa amemtumia mwanamke kama chombo cha starehe.
Nikiweka hayo katika MAISHA ambayo kati ya wahusika ni Serikali na wasanii, naona kile alichonieleza mwalimu wangu kikitendwa na serikali badala ya wamanume kwa wasanii badala ya wanawake.
Yaani naona namna serikali inavyowatumia wasanii katika kukamilisha adhma zao huku wakiwapa nafasi ndogo katika kuondoa kero zao za kazi inayowaweka wao na wategemezi wao ulimwenguni. Namaanisha serikali kutotatua matatizo iliyo na uwezo wa kuyatatua ambayo wasanii wamekuwa wakilalamikia kwa muda mrefu na ambayo kutatuliwa kwake kutaboresha maisha ya wasanii na wategemezi wao.
Tumeona wasanii mbalimbali wakitumika katika Kampeni mbalimbali za kisiasa. Ni katika kampeni hizo ambapo wasanii hutumika kuhamasiaha kusanyiko la kumsikiiza mgombea na hata kuburudisha hadhira na kwa wakati huo huo kumuwezesha mgombea kunadi sera zake.
Tumeona pia wasanii tangu kale wakitumika katika Propaganda mbalimbali (kama Gezaulole n.k) na kwa kutumia nyimbo basi ni jamii kubwa hufikiwa na ujumbe ambao usingeweza kuifikia kama kiongozi angetoa hotuba za redioni ama jukwaani
Ni wasanii haohao (tena wengi wao wa sanaa za ngoma za asili ambao ndio wana kipato kidogo kisanii) tunaowaona kila kukicha kwenye Tovuti na Majarida Tando pamoja na kuwasikia kwenye vyombo vingine vya habari wakifanya kazi njema ya kuselebuka Uwanja wa ndege kila wanapoalikwa kwenye mapokezi ya viongozi wakuu wa nchi mbalimbali.
Pengine kubwa na lenye kuonesha "kuthamini burudani" ya wasanii wa nyumbani ni pale wanapoalikwa kwenda kuwatumbuiza waheshimiwa wabunge ambao kwa miaka nenda rudi wameshindwa kuweka sheria ambazo zingelinda haki na mapato yao.
Najua Waheshimiwa wabunge na wenye mamlaka wana-enjoy saana sanaa ioneshwayo na wasanii wetu, lakini kama wanaishia kuwalipa pesa ya onesho (kama hayo ya bungeni) ama kuwapigia makofi na pesa ya onesho la airport, ama kama ni suala la mkataba wa kupiga kampeni na ama propaganda za wasanii, basi napenda watambue kuwa "kwa mujibu wa tafsiri niliyopewa na mwalimu wangu ninayemuamini, nao wanawatumia wasanii kama chombo cha starehe".
Hivi si wakati wa kuweka sheria kali kwa wale wanaosambaza kazi za wasanii? Si wakati wa kupitia vyema hakimiliki na unyonyaji ufanywao kwa wasanii na watu wachache kujinufaisha kwa jasho la wasanii? Ni kweli kuwa viongozi serikalini hawayaoni haya ama hayana "sound" ya kisiasa? Nachukia kila ninapoona "politrix" inaingilia uhalisia wa maisha na kuweka pembeni suluhisho linaloweza kumnyanyua msanii, familia na taifa kwa ujumla.
Lakini pia lawama hizi ama haya yote yatokeayo yana mkono wa wasanii wenyewe. Kutokuwa na umoja miongoni mwao, kuendekeza njaa na majungu baina ya baadhi yao na kutokuwa na elimu na utawala wa KAZI YA SANAA kunawafanya wagawanywe na kutumika bila wao kujijua. Kutokuwa na hesabu kamili na halisi za namna ya kugharimisha muda na kazi zao kulingana na hali ya maisha ya sasa ukizingatia kuwa ndio kazi yao wategemeayo kwa maisha ya sasa na uwekezaji wa maisha yajayo.
Kama alivyosema Bob Marley kuwa "emancipate yourselves from mental slavery, non but ourselves can free our minds" nami naamini ni wasanii wenyewe wanaoweza kuungana na kuanzisha mjadala mwema wa kufuatilia malipo ya kazi na kutotumika kwa ujira mdogo.

Ni changamoto tuu

1 comment:

Unknown said...

Big up sana my brother,kwa kuwapa ukweli halisi serikali pamoja na wananchi ambao hawajui nini kinaendelea juu ya taifa letu tajiri!keep on my brother,i know God will guide you bway!SALUTE BROTHER!