Thursday, November 6, 2008

"Not over until it's done"


"..once you got life there's a chance you'll be able to overcome. Where there's will, there's a way, IT'S NOT OVER UNTIL IT'S DONE, if you believe you will achieve, everything can just turn around" Hayo ni maneno yaliyoimbwa naye mkongwe wa Lover Rock Beres Hammond katika wimbo wake Not Over Until It's Done.
Maneno hasa ndio ambayo hunipa moyo pale ninapokuwa na ndoto ama mipango na kisha kuhisi kuwa ninakumbana na vikwazo mbalimbali katika kuyatekeleza. Na ndipo nikumbukapo kuwa It's not over until it's done. Na ukimsikiliza zaidi kwenye wimbo huo anaendelea kusema kuwa "while you are wondering what suit to wear, the family's worry is what a meal to share" na hiyo hunipa mwanga kuwa pamoja na matatizo tuliyonayo, lakini wengine wana zaidi. Kwa hiyo badala ya kulalamika basi tuendelea kukamilisha mikakati ya kufanikisha ndoto zetu. Na kwa juhudi, maarifa, utii na imani kutakuwa na njia sahihi ya kutufikisha kule tutakako kwenda. Lakini juu ya yote kuwe na Baraka zake akupaye uhai.
Nimesema haya kutokana na ushindi wa Rais Mteule wa Marekani Mhe Barack Obama.
Hajatoka kwenye familia ya kitajiri, hakuwa katika familia yenye jina kubwa (kama kina Martin Luther ama Malcom X), hakulelewa malezi ya wazazi wote kumfanya awe na mtu wa kuiga majukumu ya kimalezi ya mwanaume, hakutoka katika jimbo lenye uwezeshwaji mkubwa na wala si mtu aliye ndani ya siasa kuu za nchi kwa muda mrefu. Lakini kwa miezi 21 aliyopiga kampeni, ameonesha nia halisi ya kushinda uchaguzi huu na mara zote katika harakati zake amekuwa akikumbana na "kigingi" cha kuwa yeye ni mweusi na isingekuwa rahisi kwa raia wabaguzi wa nchi hii kumpa kura. Alichofanya ni kuamini katika nia yake ya kuwa kiongozi wa nchi na yanaweza kusemwa yasemwayo lakini "it's not over until it's done". Na watu wakasema kuwa historia haiwezi kubadilika kwa mtu ambaye hajawa na uzoefu wa kuongoza hata jimbo lake akapewa dhamana ya kuongoza taifa hili lenye ukubwa wa matatizo zaidi ya wema, lakini msemo unaonekana kuwa uleule kuwa "it's not over until it's done". Wamemhusisha na Magaidi, kutumia jina lake la pili la Hussein kama njia ya kuwatisha watu, kuzungumza juu ya uwezo wake mdogo katika masuala ya kimataifa lakini alionekana kujiamini katika kile atendacho akiamini kuwa mwisho wake ni Nov 4 na kwa kuwa ilikuwa haijafika, kwake ni yaleyale "it's not over until it's done".
Obama amekuwa na mafanikio makubwa saana katika "kuiunganisha jamii" tangu akiwa Community Orgernizer huko Chicago. Ni uwezo huohuo alioutumia katika kujipanga na kueleza vema mtazamo, msimamo, imani, changamoto na matarajio yake na namna anavyojipanga kukabiliana na hayo yote katika kipindi cha utawala akipewa dhamana. Alionesha kujipanga vema katika ku-organize kampeni na kuvunja rekodi ya kukusanya kiasi kikubwa saana cha pesa kwa ajili ya kampeni kitu kilichowafanya wapinzani wake waanze kutaka kufanya uchunguzi kama watu hao hutoa pesa zao wenyewe na kwa hiari. Lakini hakusita kuonesha kuwa ana lengo na kwa kuwa muda ulikuwa haujafika, "it's not over until it's done"
Ni Jumanne ya wiki hii, tuliposhuhudia kile kilichowaliza wengi. Kuona ambacho miaka mitano iliyopita hakikuwa hata mawazoni mwa watu. Kile ambacho wengi hatukutegemea kutokea katika kizazi chetu. Tukaona kwa ushindi wa wingi wa kura na kura za kimajimbo tena kwa historia ya wapiga kura wengi tangu mwaka 1908, Barak Obama akachaguliwa kuwa Rais wa 44 wa Marekani, Rais wa kwanza mwenye asil ya Afrika na kwa hilo akadhihirisha kuwa "anything can just turn around"
CHANGAMOTO YETU ni kujifunza kutoka katika njia aliyoionesha badala ya kutegemea kuleta mabadiliko Barani na nchini mwetu. Kuamini katika kuvunja mipaka iwekwayo na "maadui" na kuamini katika kile sahihi kilichopo ndani ya mioyo yetu. Namaanisha kuwa wengi hawaoni mafisadi wakiweza kusafishwa nchini Tanzania, hawaoni kama rushwa yaweza kuondolewa nchini Tanzania, hawaoni viongozi wazembe wakiwajibishwa nchini Tanzania, hawaoni mtu akigusa na kuinua maisha ya wahitaji wengi wa vijijini nchini Tanzania na wala hawaoni mageuzi ya kweli kuelekea matumaini kwa waTanzania wengi, lakini nionalo mimi ni kuwa "IT'S NOT OVER UNTIL IT'S DONE"

BLESSINGS

1 comment:

Simon Kitururu said...

Kweli tupu usemacho Mkuu!