Tuesday, November 4, 2008

Kushinda si kazi. Akishashinda sasa!!!!!!

Barack Obama wa Democrat Party
John Mcain wa Republican Party
Ralph Nader.. Independent
Bob Barr wa Libertarian Party
Cynthia McKinney wa Green Party

Leo ndio leo kwenye siasa ya Marekani na ulimwenguni kwa ujumla. Ni kwa kuwa kwa namna yoyote ile ama kwa yeyote atakayechaguliwa kuongoza nchi hii, basi lazima ataweka rekodi. Ama atakuwa Barak Obama ambaye atakuwa mwenye asili ya Afrika kukwaa nafasi hiyo, ama atakuwa John Mcain ambaye atakuwa rais mwenye umri mkubwa zaidi kushika wadhifa huo, ama wasio na nafasi kama Ralph Nader atakayekuwa mgombea huru ama Cynthia McKinney na Bob Barr ambao wanatoka kwenye vyama vichanga ama vidogo hapa nchini. Lakini twajua kabisa kuwa nafasi kubwa ipo kati ya Barak Obama ama John Mcain.
John Mcain alionekana kuwa nyuma saana ya Obama lakini ni kama anakuja tena kwa kasi ya ajabu kujaza mapengo. Kwa wale wamjuao ama wafuatiliao siasa za hapa wanafahamu kuwa Mcain ameshafanya hiyo kuwa style yake. Anajiona kama "underdog" anayefanya vema saana na anazidi kudhihirisha hilo. Na kuna uwezekano wa mtu kupata kura nyingi lakini asiwe Rais nchi hii kama ambavyo ilitokea mwaka 2000. Yanaweza kutokea mwaka huu? Si swali la kuweka pembeni maana lolote laweza kutokea kwenye uchaguzi ulio na ushindani wa ajabu na wa chinichini kama huu
Tatizo ni kwamba yawezekana akawa anajifunika shuka kukiwa kumekucha lakini pia yawezekana kura za maoni haziko sahihi. Sasa kama kura zingekuwa ama zitakuwa kama zinavyoonesha kwenye maoni, basi Barack Obama ataweka historia ya kuwa mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuwa Rais. Na hilo litawezekana baada ya miezi 21 ya kampeni za hali na mali na hatimaye kuweza kupita vigingi vikubwa vya siasa kikiwepo Hillary Clinton na kama akiweza hiki cha Mcain.
Sasa Obama akishinda ndio hasa kazi itakapokuwa na kuna "marundiko" ya lawama nioyaonayo.

1: Naamini kuna wanaomuona kama nabii vile wakiamini kuwa ushindi wake wa leo unaweza kuanza kuleta mabadiliko kesho. Hilo naona ni kama "rundiko" la lawama zijazo.

2: Watu wengi wanamuunga mkono kwenye uchaguzi ili aweke historia. Yaani orodha ya waliojiandikisha inavunja rekodi kuanzia watu wazima, vijana na mpaka wasio na makazi ambao wanaamini ataweka mabadiliko. Tatizo ni kwamba wangapi wako tayari kushirikiana naye kuleta hayo mabadiliko? Kama hakuna, basi hilo analo na ni "rundiko" la pili la lawama.
3: "Rafiki" yangu alisema "ngoja Obama ashinde labda tutapata nafuu Afrika" Nikajiuliza kuwa "mnategemea akishinda ahamishie Ikulu yake Afrika nini? Mataifa ya nje nayo yanamuona kama muunganishaji na mpatanishi mwenye uwezo na ushawishi mkubwa kimaongezi, lakini hapa nyumbani kuna chuki iliyojengeka kimatabaka na ki-rangi ambayo imejidhihirisha kidooogo kwa wale wachache wenye tabia hiyo mbovu kupanga mikakati mibaya kuharibu sifa za watu weusi. Kwa hiyo ni changamoto nyingine aliyonayo kama akishinda.
4: Lakini kwa yeyote atakayeshinda, CHANGAMOTO KUBWA ni kutafuta suluhisho la Mashariki-ya-kati, Vita vinavyoendelea Iak na Afghanistan na mkanganyiko wa uchumi unaoonekana kuimung'unya dunia hivi sasa

Kwa vyovyote iwavyo, Amani, Heshima na Upendo vitawale na kisha aliye na ushawishi wa kuwaongoza wengi na apewe dhamana tuone atakapotupeleka.
Uchaguzi ni leo, lakini kama ukishinda, CHANGAMOTO iliyo mbele yako si lele mama.

No comments: