Saturday, December 20, 2008

Ni kweli sote tu-wabinafsi?

Nimejiuliza swali hili mara nyingi na sasa naona ni wakati mwema wa kusaka maono ya wadau. Natambua sababu mbili za mtu kujishughulisha, moja ni Kusaka kipato chake na pili ni kujitolea kwa jamii. Lakini yote haya huanza kwa ridhisho binafsi la mtendaji. Na sijaona chochote nilichowahi kufanya ambacho hakininufaishi mimi kwa namna yoyote ile. Labda wewe waweza fikiria kama kuna chochote ulichowahi kufanya maishani ambacho hakikunufaishi kwa namna yoyote ile? Na kama vyote hutunufaisha (hata kama ni self satisfactions), ina maana sote tu-wabinafsi (tukijijali sisi kwanza)?
Changamoto yetu sote

6 comments:

Subi Nukta said...

Labda itokee sababu isiyopingika, kwa mtizamo wangu nadhani ni kweli kabisa ya kuwa binadamu wote tu wabinafsi.
Ubinafsi unapokuwa haumwumizi mwanadamu mwingine, basi unakuwa ubinafsi usio na usumbufu. Nafikir tatizo linaibuka pale ubinafsi unapovuka mipaka na kuwa kero kwa watu wengine, yaani pale mara zote unapotaka faida binafsi katika shughuli/jambo fulani izidi faida ya mwi/wengine.

Simon Kitururu said...

Naamini mtu anaweza kuwa mbinafsi hata kwa kujiua.

Ni vigumu sana kufanya kitu kisicho kunufaisha wewe binafsi hata kama ni kunufaika kwa kusaidia wengine, ingawa labda kunatofauti ya ubinafsi kutokana na jinsi ubinafsi utafsiriwavyo.

Ukichunguza nini mtu anapata binafsi hata kwa kujitolea, unaweza kugundua hata satisfaction ya milionea haishindani ya sista wa kikatoliki ajulikanaye kwa kujitolea na kwa kutokuwa na kitu lakini mwenye kupata satisfaction ya kujisikia yuko karibu na Mungu na hana wasiwasi wa kufa njaa au kudaiwa ada ya kusaidia ndugu aende shule ya vidudu.

Fadhy Mtanga said...

Ahsante da Subi na kaka Simon, mmegusa vema.
Nami naamini kila akifanyacho binadam ni kwa maslahi binafsi kwa namna moja ama nyingine.
Hebu chukulia mfano huu, mtu anatoa pesa kuchangia shule ambayo hatoisoma yeye wala wanae. Unaweza ukadhani hana ubinafsi, hapa namaanisha kufanya jambo kwa maslahi yako. Lakini ukifikiria kwa makini, unagundua kuwa pengine anaandaa mazingira ya kukubalika. Hapo hajajijali binafsi.
Lakini kama asemavyo da Subi, ubinafsi si tatizo, tatizo huja pale unapovuka mipaka na kuwaumiza watu wengine. Kama hivi vitendo vyo ubinafsi na matumizi mabaya ya madaraka.
Ni hayo tu kaka!
Alamsiki.

Mzee wa Changamoto said...

Asanteni sana wadau. Nami nafurahia na kuungana nanyi katika hili. Kuwa kila mtu ni m'binafsi kwa namna moja ama nyingine, japo kiwango cha ubinafsi ndiyo shida. Ni kama wasemavyo kila binadamu ana bacteria fulani sema wawapo zaidi ya wahitajiwao basi wanaleta magonjwa na madhara (kama nimekosea, mtabibu Subi na anisaidie). Kwa hiyo naamini kwa swali langu naweza sema sote tu wabinafsi (wa asili) ila ulafi ndio waweza ongeza dhahama kwa wengine. Au sio? Lol

Anonymous said...

Nakubaliana na wadau hapo juu. Sisi kama wanyama (japo tunajifanya siyo), tunayo hulka ya kujilinda na kujinufaisha kwanza sisi na watoto wetu. Na mnyama anayeweza kujinufaisha zaidi yeye na vizalia vyake ama kwa kuwala wenzake (huku yeye akijichunga asiliwe) au kwa kujishabihisha zaidi na mazingira kuliko wanyama wengine basi anakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kudumu na kuendelea kuishi. Hulka hii naamini ndiyo chimbuko la ubinafsi. Kama alivyosema dada Subi, binadamu (ambaye eti ni Homo Sapiens na yuko kileleni kabisa mwa msimbo wa maumbile) anashangaza hasa anapopuuza ule ubinadamu wake na kuwa mbinafsi kiasi cha kuangamiza binadamu wenzake. Mfano mara nyingi huwa najiuliza: hawa mafisadi ni binadamu au ni wanyama??? Wana roho gani hawa? Wanajisikiaje wanapoiba mabilioni ya pesa na huku wanaowaibia wanaishi chini ya dola moja kwa siku? Hawana hata senti za kununua dozi ya Malaria? Mzee wa vijisenti, kwa mfano, ni mbunge wangu na watu jimboni mwake ni masikini kabisa kabisa - hakuna maji, shule ziko hoi n.k. Mbona asichukue dola angalau milioni moja (kumbuka hivi ni vijisenti tu kwake) na kuchimba visima vya maji katika kila kijiji (kisima kimoja si zaidi ya shilingi laki moja na nusu - dola 150 tu!!!)? Ngoja nikome hapa kwani tayari moyo unanienda mbio...

Subi Nukta said...

Mzee wa Changamoto, umesema sawa kuwa kwa kawaida mwili wa binadamu unao bakteria wa aina tofauti kulingana na sehemu ya mwili kwa madhumuni ya kulinda mwili usishambuliwe na bacteria haribifu, kitaalamu hufahamika kama 'normal flora'; na, ni kweli ulivyosema kwamba pale 'normal flora' wanapozidi kiasi kinachohitajika, hubadilika na kuwa wabaribifu na kusababisha magonjwa. Mfano huo ulioutoa unaendana na maudhui ya mada.

Masangu,
Pole sana kwa moyo kwenda mbio lakini hiyo ni hali ya kawaida kabisa kumkumba binadamu yeyote mwenye hisia. Mwili husisimka kutokana na hisia zinazokuja kwa kuona ama kusikia ama kunusa ama kuhisi, kwa hivi, vitendo vya kifedhuli vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wetu vinaamsha hisia za hasira na chuki miongoni mwa raia ambao wanahisi na kuamini kuwa wanadhulumiwa pasina kupewa nafasi ya kuhoji na kupewa majibu ya kweli. Inaudhi zaidi pale tunapokuwa tumejaliwa kuwa katika nchi moja, tunawapa dhamana ya uongozi baadhi yetu ili tuweze kufaidi rasilimali na baraka za nchi yetu, na wachache hao wakatudhulumu haki iliyopaswa kuwa yetu sote. Kwa mantiki hii, binadamu yeyote ana kipimo cha uvumilivu, na tumejionea kikomo cha uvumilivu kinapofikiwa, ni kwa kiasi gani yamekuwepo madhara yanayotokana na uchungu uliolimbikizwa kwa vitendo hivyo vya kidhalimu.
Hata na hivyo, tuendelee kuomba muafaka mwema kwa mustakabali wa maisha yetu na vizazi vinavyofuata.

Ninafurahi kusoma maoni mchanganyiko toka kwa wadau mbalimbali yenye kufunza na kumwezesha mtu afikiri na kupata mtizamo wa wanajamii husika.