Thursday, December 11, 2008

Nimemsoma Jenerali Ulimwengu, na nakubaliana naye

Jenerali Ulimwengu. Picha toka Bongo Celebrity
Ukiniuliza kwanini napenda Roots Reggae ntaendelea kusema yale ambayo nimekuwa nikisema muda wote kuwa INANIWAKILISHA MIMI NA JAMII YANGU KUU. Ninalomaanisha hapa ni kuwa ni kati ya aina chache za muziki ambazo zinagusa maisha halisi ya mtu wa chini, kumfunza na kumtambulisha juu ya ugumu aliopo na kisha kumpa njia sahihi za kumkomboa (na mara nyingi ni kupigana bila kupigana kwa kuuondoa utumwa wa kiakili uathirio wengi) Ukimsikiliza Lucky Dube kwenye wimbo wake Guns and Roses upatikanao kwenye albamu yake ya Taxman anaanza kwa kujishangaa kuwa "I don' t know whyI keep believing that one day, they' ll bring us together. When they' ve shown in more ways than one that all they care about is the dollar..." Ni haya haya ajishangaayo Lucky ambayo nami pia nawashangaa viongozi wetu ambao wanajitahidi kutushawishi sisi kuwaamini wao na kisha kuamini kuwa nchi bepari (ambazo zina nia ya kuendelea kuwa viranja wa dunia) ziko mstari wa mbele kutusaidia kuwa na uchumi wenye nguvu kama wao. Mmhhhh. Yawezekana akili zangu ni kama dawa ya kikohozi (shake well before use) lakini katika hili siamini kama nitaamini maishani mwangu. Jenerali Ulimwengu ni kati ya wanahabari ninaowaheshimu saana na sio tu kwa uwezo wake wa kujengea hoja kile aaminicho, bali pia kuja na jumuisho lenye suluhisho kwa hoja na mtazamo alionao juu ya tatizo. Haya ameyafanya kwenye Radio, Television na hata kwenye makala zake magazetini kama ambavyo ameandika kuhusu suala zima la elimu. Sijabahatika wala sihitaji kujua itikadi yake, lakini najua ameeleza vema namna elimu ilivyo na makundi yake na kisha akaendelea kwa kile nilichoanza nacho kuwa tutake tusitake, elimu ya kikoloni haitatujenga na kama nisemavyo akaja na sheria zake 10 kuhusu elimu. Tunaweza kujisomea na kukubaliana naye ama kupingana naye maana tuna haki ya kukubali kutokubali na hilo ni jambo la kujivunia. Lakini haijalishi waliangalia hili toka pembe gani, CHANGAMOTO YETU hapa ni sisi kutafuta namna iliyo bora, iendanayo na mahitaji na mazingira yetu ili kuweza kuinyanyua jamii kwa elimu itufaayo na si kufuata mikia ya wale ambao mara zote wanataka kuwa juu yetu. Huo ni UTUMWA WA KIAKILIA ambao Bob Marley alituonya kwenye Redemption Song aliposema "emancipate yourselves from mental slavery, none but ourselves can free our mind" Twahitaji kuamka, kupambazuka na kusimamia kile kilicho chema kwetu na jamii yetu. Nimemsoma Jenerali Ulimwengu na nakubaliana naye na leo nasubiri kuona ana RAI gani kwetu. Huu ni mtazamo wangu wa namna nionavyo tatizo, na yawezekana NAMNA NIONAVYO TATIZO NDILO TATIZO

4 comments:

Simon Kitururu said...

Nilianza kupenda Roots Reggae tokea hata sijui niliokuwa nawasikiliza kama akina Jimmy Cliff, Bob na wengine wanamaanisha nini. Ingawa reggea ya kwanza niliyoipenda ilikuwa ni ya Eddy Grant enzi hizo. Ni muziki wenye ujumbe na mpaka saa nyingine ujumbe ni mkali na unasuta kuliko mahubiri ya wahubiri kama Moses Kulola waliofanikiwa kipindi fulani kuniokoa.

Generali Ulimwengu ninamuheshimu na kuna wakati ninamuonea wivu kwa uwezo wake wakufikishia umati ujumbe aufikirio. Kuna wanahabari vichwa lakini ni kama mwalimu ambaye wanafunzi wote wanajua anajua somo ingawa hatuelewi akifundisha.

Nakubaliana naye sana tu GENERALi mimi pia.

Mzee wa Changamoto said...

Simon mimi sikuonei wivu, bali najivunia saana kwa namna ulivyomaliza maoni yako kwa sentensi ambayo sina hakika kama wengi wataiona kwa namna niionavyo mimi. Kwamba "NI KAMA MWALIMU AMBAYE WANAFUNZI WOTE WANAJUA ANAJUA SOMO, INGAWA HATUELEWI AKIFUNDISHA". Thanx alot Brother na kwa hakika jamaa ni mtu mwenye fikra za mbali na ambaye mara zote kwenye vipindi ama makala zake najitahidi kuwaza ni nini kiendeleacho MAWAZONI mwake.
Ni Jenerali katika fani, na katika uelimishaji pia.

Anonymous said...

Hiki kijiwe sikuwa nakijua. Safi sana

MARKUS MPANGALA said...

JENERALI ULIMWENGU? yaani hapo hutnitoi kabisa, siyo siri hata mimi huwa namuonea wivu jamani maana anachokisema na kukiandika unatakiwa kudurusu. hakika huyu ndiye mwalimu ambaye wanafunzi wake nadhani hatuelewei labda ipo siku tutalewa tu. Mm mkuu mimi kwa KWAITO huniambii kitu ila Roots Reggae ni habari nyingine kuna wakti unaweza kuangusha kilio sababu ya ujumbe kukuchoma. unakumbuka tamasha moja la Bob mjini London alishangazwa na watu walivyofurahia wimbo wake wakati alidhani jinsi unavyohuzunisha wao watahuzunika? mmm akabaki hawa jamaa vipi ingawa wananizmia lakini huu ujumbe vipi?
Mkuu tusije tukataka kuuza kiti kaka yule GAVANA wa Illinois kwa Obama.
kwaheri