Tuesday, December 2, 2008

Ungekuwa wewe ndiye ufanyaye maamuzi!!

Kuna ule msemo niliokuwa nikiusikia saana tutazamapo Mechi ama michezo mbalimbali ambapo walisema "unaona rahisi ukiwa nje, ukiingia ndani ndo utajua ugumu wake" Kwa kuwa nilikuwa na bado ni mwanaspoti najua kuna ukweli ndani ya usemi huu. Lakini pia wala huhitaji kuwa mwanaspoti kutambua hili, kama una fikra na hisia halisi kuweza "kujibandika" kwenye nafasi fulani ukaangalia namna ambavyo ungeweza kukabiliana na mambo mbalimbali najua utapata hisia kamili za ugumu unaoweza kukutana nao.
Nasema haya kwa kuwa najaribu kuangalia, kama mimi ama wewe ungekuwa ndiye mwenye maamuzi na nguvu ya kuibadili Tanzania (ambayo kwa hakika inahitaji m'badilishaji) unadhani ungeanzia wapi? Kwenye Kampeni za hapa Marekani waliwauliza wagombea wapange mambo matatu yatakayokuwa ya kwanza kushughulikiwa waingiapo Ikulu kulingana na umuhimu wa mambo hayo. Mimi hata sijui kama ukitoa nafasi ya mambo mia kuna lenye kuzidi jingine nyumbani. Miundombinu? Maana watu wanaozewa na mazao wakati wengine wanakufa njaa. Afya? Kuna watu wanakufa kwa kukosa matibabu ya msingi tu kama dozi ya klorokwini. Mishahara ya walimu? Maana kuna walioajiriwa miezi kadhaa na hawajaonja senti ya jasho lao. Malimbikizo ya mishahara? Si serikali itabidi ikakope maana yadaiwa mengi. Mikataba ya madini? Huko sisemi. Matumizi mabaya ya serikali? Kwanza utaingia uongozini bila mlungula?!! Rushwa? Wakati undani wa mzizi wake utahitaji miongo kadhaa kuisafisha!!! Utaanza na nini? Kununua magari ya askari kuzuia uhalifu? Wakati nyumba flats zao vyoo vimeziba? Sijui ni wapi waweza kuanza ukitaka kuibadili nchi yetu maana UOZO uliopo kwenye mfumo uliojengeka wahitaji zaidi ya vipindi viwili vya uongozi kuutoa (kama kuna uwezekano wa kuutoa).
Lakini yote juu ya yote twahitaji kuisafisha Tanzania yetu. Twahitaji wananchi wapate huduma zilizo haki yao na kuacha kununua Huduma za Mteja (customer services) tena kwenye mashirika ya Umma kama Tanesco, Bandari na hata Mapato. Twahitaji kuona watu wakiwajibika na wasipofanya hivyo waonekane wakiwajibishwa. Twahitaji kuona nchi ikiwekewa mikakati thabiti ya kutokuwa tegemezi kwa misaada ya nje na hata ile inayoletwa (pale itakapohitajika) iwafikie walengwa. Twahitaji kuona uwiano (japo wa karibu) kati ya mjini na vijijini na pia kuona mipango yenye kuongeza mzunguko wa pesa mikoani ambako ndiko kwenye uzalishaji, na kwa kufanya hivyo pengine nguvu kazi itarejea huko na uzalishaji utaongezeka. Maana mijini (kama Dar) hata waongezeke watu milioni kumi zaidi, hakuna sehemu ya kuongeza uzalishaji uendanao na ongezeko hilo la idadi.
Twahitaji mengi zaidi ya hayo, na pengine twaona serikali haifanyi itakiwavyo kuokoa haya, ndio maana nikajiuliza kuwa UNGEKUWA WEWE NDIYE AFANYAYE MAAMUZI ungeanza na lipi ama ungefanya vipi?
Kuna tatizo hapa??? Labda ni namna uonavyo ndio tatizo

No comments: