Tuesday, December 2, 2008

Kuelekea miaka 3 ya Awamu ya 4

Ningepata nafasi ya kuongea na Rais wangu. Kama ningepata nafasi ya kuongea na RAIS wa nchi yangu niipendayo (Tanzania) basi ningemuomba kuwa na mazungumzo ya aina ya tofauti kidogo. Mazungumzo huku tukitembea (maana nasikia mkiongea huku mnatembea inakuwa ngumu kupata hasira za haraka) na pia naamini kungekuwa na nafasi ya kuelezana ukweli zaidi. Ningeomba kuwa sisi wawili tu na ningeweza kumuuliza machache nitamaniyo.
1: Ningemuuliza kuhusu MIAKA MITATU anayotimiza akiwa madarakani na kama anadhani ametimiza asilimia 60 ya ilani yake ya uchaguzi (Si mnajua miaka mitatu kati ya mitano ni 60%?)
2: Ningemuuliza kama ana IMANI NA VIONGOZI wake wasaidizi na kama ndio basi kwa asilimia ngapi. Na kama hana anakabiliana vipi na hilo?
3: Ningemuuliza ameweza KUTEMBELEA MIKOA MINGAPI (ukilinganisha na ile aliyotembelea wakati wa kampeni) na ameweza kutambua matatizo makubwa mangapi ambayo hakuyajua kabla?
4: Ningemuuliza anapata na kuhakiki vipi taarifa za utendaji wa mikoani.
5: Ningemuuliza ni MABADILIKO gani amefanya ama kupanga kufanya baada ya kuona hali halisi ya JELA alizozitembelea na kunukuliwa akisikitishwa na hali ya huko.
6: Ningemuuliza juu ya TAKWIMU halisi za maendelea ya ELIMU (sio majengo "yanayoota" kila kata)na pia Takwimu za AFYA (sio zahabati zisizo na dawa wala wauguzi) Ningemuuliza namna anavyoamini Serikali inawajali wale waliojitoa mhanga kuitumikia kama wafanyakazi wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Walimu na wengine.
7: Ningemuuliza kama bado anaamini kuwa KILIMO NI UTI WA MGONGO WA UCHUMI WETU na kama kuna mipango yoyote ya kukiboresha.
8: Ningemuuliza juu ya MIUNDOMBINU na MAWASILIANO na kama anajua kuwa kuna mazao yanayooza mikoani kwa kukosa usafiri wa kuyaleta "sokoni" wakati kuna wanaokosa chakula upande wa pili wa nchi.
9: Ningemuuliza kuhusu RUSHWA na MATUMIZI MABAYA yanayosemwa kwa serikali na watendaji wakuu wake na kama kuna hatua zinazochukuliwa juu ya hilo.
10: Ningemuuliza juu ya ZIARA zake za nchi za nje na kama anaelimisha wananchi jinsi anavyotofautisha ziara zake kama Rais wa nchi na Rais wa Umoja wa Afrika na pengine ningeuliza kama kuna anayekaimu SHUGHULI ZAKE ZOTE za ndani ya nchi awapo katika kulitumikia Bara la Afrika.
Sina hakina na muda kama ungetosha lakini ningepata wa ziada ningeuliza kuhusu maendeleo ya Ripoti za Richmond na nyingine ambazo ninaamini "wanazifanyia kazi", ila hawajatujulisha walipofikia.
Najua angekuwa na majibu maana "anatenda kazi yake".
NB: Maongezi yetu yangekuwa ya kirafiki sana maana Rais wangu ni kiongozi, mlezi na pia rafiki kwangu. Si kama haya aliyotaka kuwa nayo Pink kama angepata nafasi ya kukutana na Rais wake. Hebu mtazame hapa chini anavyosema angependa kumuuliza Rais wake angepata nafasi kukutana naye.


3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Mubelwa mawazo/maswali mazuri sana kama kwali ungepata hiyo nafasi basi ningekuunga mkono. Kwani pia nimekuwa mara nyingi nawaza kwa nini nisiende kuongea na Rais ili jambo hili libadilishwa, au kumuuliza kama anayafurahia vipi maisha ya urais. na mengine mengi mengi

Unknown said...

Halafu naomba ukikutana naye umuulize hivi huwa anajisikiaje kwenda kuomba misaada nchi za nje ambazo zina rasilimali kidogo sana kuliko yeye na yeye nchi yake imejaa rasilimali ambazo kwa kuzitumia tu kila mtanzania angeweza kujengewa nyumba nzuri ya kuishi bure acha masuala ya elimu nk maana Algeria hilo limewezekana kwa madini kidogo waliyonayo.
Pia Muulize hivi huwa anajisikiaje wakati wananchi wanakufa kwa kukosa dawa huko vijijini na yeye na mawaziri wake wakienda kutibiwa majuu?
Na muulize hivi kama kuna Mungu na kuna siku ya kila mtu kutoa hesabu ya mambo yake, je yeye atamueleza vipi Mungu akiulizwa ahadi alizotoa kwa watanzania wakati anaomba kuwa mfalme wao?

Asante sana naamini rais wetu atakupa nafasi uongee naye.

Mzee wa Changamoto said...

Asanteni sana Yasinta na Kaka Lazarus. Ni kweli kuna mengi ya kumuuliza Mheshimiwa na naamini angeweza kujibu. Blessings