Saturday, December 13, 2008

Welcome back Lukwangule. Welcome to the World too

Kama kawaida nilikuwa napitia blog za "wakubwa" wangu katika fani na nikakutana na "mrejeo" wa Kaka Beda Msimbe wa Lukwangule Entertainment ambao kwa mujibu wake mwenyewe ni kutoka kwenye safari ya vijijini ambayo amekiri kuwa hataisahau. Namnukuu mwenyewe hapa alivyoandika kwake kuwa "Nilikuwa mkoani Morogoro, maeneo mbalimbali ni journey ambayo sitaisahau hasa nilipokutana na vituko kutoka kwa waendesha maeneo ambao huenda hawajui hata sera nini na implication zake. Ni journey ambayo I will never forget.
Rais anapopewa takwimu za mwaka 1996 halafu akazishtukia...rais anapopewa taarifa ya matumizi ya fedha halafu anahoji uhalali wake...watendaji wanapojaribu kuziba soni zao kisha wanagutukiwa, wataalamu wa uchumi wanapobabaisha na takwimu zao halafu anawashtukia. Wananchi wanapomwambia rais waziwazi kwamba watendaji wake ni wazushi. Rais anaposhangazwa na kauli za watendaji ambazo walistahili kuzifanya zamani halafu wanasingizia mambo ambayo hayana kichwa wala mguu. Rais anaposhangazwa na uuzaji holela wa ardhi za watu kiasi cha kukosa akiba na duhh....!"
Nimemkaribisha Lukwangule kwa kuwa tumekosa habari zake kwa muda wote aliokuwa safarini na pia namkaribisha kwenye "ulimwengu wa kukosa majibu" ya maswali muhimu na halali ambayo kila mwananchi mwenye kuguswa na hali ya maisha ya tabaka la chini anajiuliza. Lakini sasa yeye kajionea maana ameonesha kusikitishwa nayo na yamemgusa kiasi cha kusema hatosahau. Nani ambaye asingeguswa kuona kuna "watawala" (wajiitao viongozi) ambao hawajui majukumu yao? Ama ambaye asingeshangazwa kuona kiongozi akitoa hizo taarifa za miaka 12 iliyopita (nadhani zitakuwa ni bora kuliko za sasa ndio maana akaamua kuzitoa kuficha uozo uliopo sasa) ama wananchi wanapoendelea (na narudia wanapoendelea maana walishawazomea na kuwashitaki kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowasa) kusema kuwa wamechoshwa na watendaji wao? Tuliwahi kuuliza hapa kwenye changamoto siku niliyoandika kama
ningepata nafasi ya kuongea na Rais wangu na maswali ya 2-5 (naomba kuyarejesha hapa) yalikuwa
Ningemuuliza kama ana IMANI NA VIONGOZI wake wasaidizi na kama ndio basi kwa asilimia ngapi. Na kama hana anakabiliana vipi na hilo?

Ningemuuliza ameweza KUTEMBELEA MIKOA MINGAPI (ukilinganisha na ile aliyotembelea wakati wa kampeni) na ameweza kutambua matatizo makubwa mangapi ambayo hakuyajua kabla?

Ningemuuliza anapata na kuhakiki vipi taarifa za utendaji wa mikoani.
Nadhani pia siku ya Uhuru niliandika kuwa nahisi Rais wetu hapati taarifa rasmi za utendaji na maendeleo huko vijijini maana siamini kuwa angeweza kuwa na tabasamu "nene" kiasi kile kama angejua uhalisi wa kile kiendeleacho vijijini ambacho kingeweza kuzuilika (maana najua anatambua kuwa hali ya vijijini si kama ya mjini).
Naamini ni hawa viongozi wanaomfanya Rais aonekane kama hajali wananchi wake na wanachi wanaingiwa na hasira na kufanya yasiyotarajiwa wala kustahili kama yaliyotokea kule Mbeya. Sina hakika kama arais aliagiza uchunguzi juu ya sababu za yeye kutaka kupigwa mawe na wananchi (ila si atawaagiza haohao walio chanzo cha tatizo?)
Inashangaza kuona ukoloni wa kutawaliwa na wenzetu umekwisha na sasa ukandamizaji unaendeshwa na ndugu zetu, kama alivyoimba Innocent Galinoma kuwa "only this time, the downpressor happens to be my brother.....". Naomba nirejeshe kibao chake kuzungumzia hali halisi ya "utawala" wa Afrika ambao mpaka leo hauwezi kutueleza nini kinaendelea kwenye uchumi wetu m'bovu ilhali walio nje wananufaika na rasilimali zetu, hawawezi kutueleza kwanini kuna vita baina yetu tena kwa silaha toka nje ambako wana viwanda vya silaha na hawana vita, hawana jibu la kwanini kuna mvua na njaa inatawala, wala hawawezi kujibu kuhusu elimu na mustakabali wa maisha ya mtoto wa sasa wa Afrika. Pia si wengi wanaweza kujieleza uwaulizapo kwanini hakuna haki na usawa. Lakini wengi twajua kuwa RUSHWA na UBINAFSI vimetawala na kuviondoa hivi ni CHANGAMOTO YETU sote kama tunataka kusonga mbele. Nasio alisema "we gonna rise up, we gonna wise up, we gonna wake up, we gonna shake up" na akaendelea kusema " and people rise and say Liberation is today, and people rise and say, POLITICIANS MUST PAY"
Ni MTAZAMO WANGU kwa namna nionavyo tatizo na yawezekana NAMNA NIONAVYO TATIZO NDIO TATIZO.
Msikilize Inno Galinoma akiizungumzia Afrika na kuwauliza waAfrika tuendako. Naweza kusema huu wimbo ni "must listen" maana ni kuhusu Afrika kutoka kwa mwafrika kwa manufaa ya Afrika na waAfrika

No comments: