Saturday, January 3, 2009

CHANGAMOTO YETU SANAANI

Kundi zima la Tuku lilikuwa ni mpiga ngoma, mpiga tumba + chekeche, mpiga gitaa la besi, yeye na gitaa kiongozi, mpiga marimba na marimba nyingine (kama ya kigogo hivi). Muziki wao... bofya hapo chini usikie.

Kwa muda sasa nimekuwa nikizungumzia na kuandika juu ya sanaa yetu na hususani Muziki. Na mara zote nimekuwa nikizungumzia muziki ambao utatutambulisha hata nje ya nchi. Muziki ambao hata kama mtu hatajua unatoka Tanzania lakini akiambiwa hatosita kuelewa hivyo. Ni hilo ambalo linapotea sasa. Tunapoteza dira na muelekeo kwenye muziki kwa kile kinachoonekana kama utandawazi. "Tunatayarisha" miziki kwa gharama na uwezo mdogo kuliko maelezo. SABABU? Niliwahi kuwauliza baadhi ya wasanii sababu wanazodhani zakwamisha ukuaji wa muziki wetu (wakati nikishiriki vipindi vya sanaa pale 100.5 Times Fm) na baadhi yao bila aibu wakanijibu kuwa ni Lugha (wakimaanisha Kiswahili kinatukwamisha). Nikajiuliza majina ya wasanii wa Afrika wenye heshima ya sanaa hii Ulimwenguni nikakuta wengi wao hawatumii Kiingereza. Hapa sitaacha kumtaja nguli Oliver Mtukudzi ambaye napenda kazi zake na nilishangazwa na kikosi chake anachotumia kutoa burudani hiyo. ni wachache na zana zao ni za kiasili zaidi.
Inasikitisha saana unapoona sifa na uwezo wa baadhi ya ma-producer wa muziki wa "kizazi kipya" nyumbani. Yaani ukijua kupiga kinanda na gitaa kisha ukajua matumizi ya softwares, basi ushakuwa producer. Well!! hilo pekee si tatizo, ila kutojua nani wa kumshirikisha katika muziki gani ili aweke ala gani ilete ladha gani ndio tatizo kuu hapa. Kuna wasanii wengi saana wanaofanya vema kwenye miziki ya asili na ambao kama wangeshirikishwa wangeweza kuupa muziki wetu mtazamo mpya, lakini kwa "u-mimi" uliopo katika "productions" zetu nahisi tunatafuta maendeleo kwa kujichimbia chini zaidi.
Nilijifunza mengi saana kuhusu uchanganyaji wa muziki wa asili na huu "mpya" kwa muda niliokuwa najihusisha na muziki wa ki-Afrika na ulionifanya niwe natembelea studio za Njenje pale Ilala ambapo kwa msaada wa watayarishaji Kepi, Samwel, na wengine nilijifunza mengi na kuanzia hapo niliuona upungufu wa muziki wetu kwa "jicho la ziada" na naamini hii itakuwa changamoto kwa "watayarishaji" wengi wa nyumbani kuangalia watakalo kufanya kabla hawajatamani kuwa kwenye orodha ya wamiliki wa studios. Ni mwaka mpya na changamoto mpya kwenu ni kuukuza muziki badala ya kutegemea muziki kuwakuza. Studio nyingi lakini ubora uko chini kuliko maelezo. Na bado kila siku "waimbaji" wajiitao wasanii wanasema "wamekuja kutushika na kutaka kuteka soko la kimataifa" kwa miziki isiyo na ubora.
Tukitaka na kuamua tutaweza na hii ni Changamoto Yetu sanaani

Msikilize TUKU katika moja ya nyimbo zinazompa heshima saana Ulimwenguni. Kaimba kikwao na katumia zana halisi za kikwao. Wimbo unaitwa Ndakuvara

Naomba niongeze huu Tapindwa Nei kuonesha muziki wa asili uliotulia unogavyo. Muziki mwanana, tempo ya kufikirisha, maandalizi mazuri na unaweza kuuhisi ndani mwako

4 comments:

MARKUS MPANGALA said...

Eeee changamoto kubwa hiyo! amani iwe nanyi

Fadhy Mtanga said...

Mi huwa sijui wasanii wetu wanajisikiaje wanapowaona wasanii wengine wa Kiafrika wakitamba na sanaa zao. Tena lugha zao wala si kubwa kama Kiswahili.
Nawashauri wafikiri mara nyingi juu ya mustakabali wa sanaa yetu ya Kitanzania.
Ni hayo tu!

Evarist Chahali said...

Wanastahili pongezi kwa kuuwakilisha utamaduni wetu huko ughaibuni.

Simon Kitururu said...

Kila siku huwa naombea kuwa mtazamo wa sanaa uliopo Tanzania sasa hivi uwe ni wa mpito tu!

SIpingi kuwepo kwa sanaa iliyobobea sasa hivi na itawalayo redio na TV, ila na wasiwasi tusipoangalia tutapoteza kabisa sanaa za asili.

Cha ajabu ni kwamba, nchi nyingi nilizopita mziki wa asili ndio muziki uheshimiwao. Na mpaka wafalme na wale waliofanikiwa kimaisha, kwao ni ujanja kujua muziki wa asili. Ukifuatilia kuanzia wafuatiliaji wa claasical music ulaya hata Marekani hukawii kustukia kuwa asilimia kubwa ndio wajanja wenyewe ambao maamuzi yao yakiwa mabaya dunia nzima inazinguka.

Tutafika tu lakini!