Wednesday, January 7, 2009

Dikteta ni nani? Na kwanini twamhitaji?

Photo Credits: Synergy
Ninapoangalia namna "tunavyokaririshwa" maana za nani ni nani, na kwanini ni yeye na kwa manufaa ya nani na nani awe rafiki na nani awe adui yake nasikitika sana. Tumepangiwa kila kitu kwa tafsiri ya wenzetu ambayo kwa hakika ni kwa manufaa yao.
Mandela alikuwa "mkorofi" ( na dikteta fulani hivi) kwa kudai uhuru ambao baada ya kutambulika sasa anaonekana ni shujaa japo hajabadili alichofanya, Saddam alikuwa shujaa aliposhirikiana na wao kisha akawa dikteta alipopingana nao. Gadafi aliyekuwa dikteta na kuonekana kama asiyewajali wananchi wake sasa kawa shujaa na "kiongozi safi" kwa kuwaruhusu "wakuu" kuingia na kukagua silaha zake japo hakuna alichobadili kwa wananchi.
Luciano aliwahi kuimba kuwa "they're trying to control our minds, and treating us like swine. They telling us who to love or hate as if they're great"
Najua akitokea mtu akalazimisha baadhi ya mambo ya maana kutendeka nyumbani basi ataitwa dikteta (na kwa bahati mbaya nasi tutashabikia hata kama si tafsiri yetu).
Najiuliza akitokea "kiongozi" akalazimisha kusimamishwa kwa mikataba yote ya madini ili ipitiwe upya hataonekana dikteta?
Je atakayelazimisha viongozi wakuu waliosababisha mabilioni ya hasara serikalini wachunguzwe licha ya katiba waliyoshindwa kuitii kutosema hivyo hataonekana dikteta?
Je atakayelazimisha wabunge kujenga ofisi na kutumia muda mwingi majimboni mwao kama walivyoahidi wakati wa kampeni hataonekana dikteta?
Atakayelazimisha utendaji wa mikoa kulingana na rasilimali zake kuwanufaisha wananchi wake na kisha nchi nzima huyo hataonekana dikteta?
Najua kuwa atakayewafikisha viongozi wakuu mahabusu ataitwa dikteta kwa kuwa amekwenda kinyume cha katiba, lakini sijui kwa nini katiba imlinde yule ambaye ameivunja kujilimbikizia mali na kuitia serikali hasara kubwa?
Kama huyu atakayetenda haya niliyosema hapo juu, atakayevunja mikataba ya ujenzi wa miundombinu yenye utata, atakayehakikisha ahadi za wananchi zinatekelezwa na waahidi hasa wabunge, atakayeshurutisha matumizi mazuri ya rasilimali za wananchi kwa manufaa ya sehemu husika, atakayeshinikiza malipo kwa wafanyakazi ambayo mpaka sasa haijajulikana kwanini hawajalipwa ilhali waheshimiwa wanapata pesa zao bila malimbikizo, atakayehakikisha kuwa mkulima wa anapata senti zake zote alizoikopesha serikali na ambazo anatumia pesa nyingi kufuatilia kuliko atakazolipwa, atakayesimamisha ziara za nje na ndani za viongozi (zisizo za lazima) na atakayeamua Tanzania iwe ya manufaa kwa wa Tanzania kwa kutumia kila kilichopo Tanzania ataitwa DIKTETA, basi namuombea awepo. Aje atufanyie hayo na nadhani tunamhitaji na anaweza kuwa suluhisho la awali kwa yaliyopo. Maana sasa imekuwa kama alivyosema Kaka Evarist kuwa HAKI IMEKUWA FADHILA na twahitaji atakayeangalia haki na kama haki .
Nionavyo ni kwamba mfumo unaotumika kumpata mtu atayewania uongozi unapita katika ngazi na misaada ambayo mpaka aje kupatikana mgombea anakuwa kashirikisha "wataalamu" wa ufujaji ambao akichukua madaraka hataweza kusema lolote juu yao.
Sasa hivi, hata nchi yangu Tanzania iongozwe na Masia na Mtume, iwapo MFUMO UTAKAOTUMIKA NI HUU ULIOPO, bado upande pekee wa maendeleo tutakaoelekea ni wa MAENDELEO HASI.
Tatizo la Tanzania si watu walio madarakani, bali ni MFUMO unaowaweka pale, unaowaongoza katika kuongoza na unaowawajibisha.

Pengine nionavyo mimi ndilo tatizo, lakini kuna ukweli kuwa tafsiri nyingine zinatufanya tuwachukie wale ambao wanaweza kutuletea mabadiliko ya kweli na badala yake tunaendeleza "kubebana na kufichana" ambako kunaendelea kutuweka tulipo.
Ni Mtazamo wangu tu na naendelea kutunza haki ya kukosea na kukosolewa.

5 comments:

MARKUS MPANGALA said...

kaka mfano wangu uleule: hasa kuhusu hili la Septemba 11, 2001 pale WTC. kwanini jengo namba 7 lilianguka saa 6 baada ya mengine kutunguliwa na ndege? kwanini lianguke wakati halikutunguliwa na ndege? kwanini Larry Silvestein alisaini mkataba wa miaka 99 wa ulinzi na kampuni ya Marvin Bush siku sita tu kabla ya tukio? kama kishindo, mbona zile posta kuu upande wa kulia na kushoto kuna jengo lingine la ghorofa hayakuanguka likaanguka jengo hilo tu? hapa nimejaza utafiti nangojea kumwaga tena hadharani kwa mtindo wa makala gazetini kama nilivyofanya mwaka 2007.
Kuna mambo yanashangaza sana, yaani watu wanakaa wanapanga wanachoona kinafaa kwaajili yao halafu tunakaririshwa ndivyo ilivyo? kwanini tuambiwe ile ndege iliangukia kule Sharksveille P.A baada ya mapambano ya rubani,abiria na watekaji? nani alithibitisha hilo? Je Rick Gibney anasema kuhusu kikosi cha jeshi cha Dakota kaskazini? Je kweli ndege ya abiria inaweza kugonga jengo la Pentagon? Ilikuwaje wakati ndege inayotajwa ya Boeing 757 igonge jengo hilo wakati inahitaji urefu wa futi 155 kwenda juu ili ikae katika usawa wake? Kwanini kulikuwa na mabaki ya ndege za Douglas A-3 Skyworrior? zilikwenda kufanya nini pale Pentagon? Jengo lina urefu wa futi 85 huku Dougls A-3Skyworrior inahitaji futi 76 tu kuishambulia Pentagon?. mmmmm NAWAZA TU JAMANI au niseme kwani Mkurugenzi wa Fiduciary co. International Bi. Ann Tatlock alialikwa kwenda OMAHA, Nebraska katika makao ya jeshi ya USSTRATCOM(Offut Air Force Base)(Us Strategic Command) huku ndege ikigonga ofisi zake katika jengo la kusini? kwanini wanajeshi walimlinda kila wakati hata alipotakiwa kutoa maoni yake mbele ya vyombo vya habari? kwanini alisema anashukuru kupewa taarifa kwani wafanyakazi wake 650 walikuwa nje ya jengo siku hiyo? Je alikuwa wapi tajiri Warren Buffut wakati alitakiwa kuwa pamoja na Ann Tatlock?
dUU nimechanganyikiwa au? aaa ha ha ha hapana jamani ila kuna mambo yanafanyika duniani yanashangaza sana, kwanini kikao cha ISI na CIA kiliamua Mohammed Atta apewe pesa kwaajili ya shambulizi lile? kwanini walitaka kumtoa katika ukurugenzi mkuu wa ISI(shirika la kijasusi la Pakistan) Mohammad Ahmed? mm basi mkuu nimechoka.

SADDAM HUSSEIN walimtumia kupambana na Iran kisa tu Iran iliwatimua wamarekani baada ya kupinduliwa utawala wa mfalme Shah, wakasema anafaa lakini walipoona amepunguza uwekezaji wao katika visima vya mafuta na kuwapa Urusi wakasema adui, heeeee. Wakasema lazima Palestina ufanyike uchaguzi wa kidemokrasia, wananchi wakaichagua HAMAS, duu jamaa wanademokrasia wanakataa matokeo yenyewe eboo? wakasema wewe Mugabe unajifanya mjanja utaona, sasa wanatulazimisha kusema Mugabe dikteta, aaaaa niwekee kisu shingoni chinja sikubali! duuu niache kwanza kichwa kinauma mkuu

Mzee wa Changamoto said...

Umemaliza mkuu. Asante sana. Nadhani hapa cha kujifunza ni kuangalia upande wa asemaye fulani ni fulani kisha kuangalia yeye ni nani. Ni ajabu tunapowategemea wenye uchu wa utawala watujenge tuwe kama wao. Na kwa kutumia mbinu zao za "kugawa na kutawala" tunatawalika bila kujijua.
Inasikitisha saana sasa tunapoanza kutafsiriwa nani ni nai na nini ni kipi ili tu tuamini wasemayo.
Mmhhhhh!! Mbaya sana.
Nami naacha maana umesema Markus

Simon Kitururu said...

Kazi kwelikweli!:-(

Anonymous said...

wakuu mna challenge za kweli si kitoto ila tatizo mi mwezenu upeo wangu mdogo yaani nipo kama bendera nafuata upepo,hapa nashukuru umeniweka wazi mambo mengi asanteni kwa hilo.
hivi ndiyo waafrica wengi tulivyo:
tuna midomo lakini hatusemi,tuna macho lakini hatuoni,tuna masikio lakini hatusikii,
THE BEUTYFULY ONE ARE NOT YET BORN

Mzee wa Changamoto said...

Karibu sana Salu. Karibu CHANGAMOTONI. Tunashukuru kuwa nawe na twaamini utaweza kutembelea majamvi mbalimbali ambayo yameandikwa kwenye "bog scroll" hapo barazani ama kwa kuungana na bloggers waliopo kwenye maoni humu.
Baraka kwako