Tuesday, January 13, 2009

Ni lini biashara hii itakapokuwa huduma?

Picha mali ya Michuzi
Mimi si mchumi na wala si mtaalamu wa uchumi na utawala, lakini naamini kuna baadhi ya vitu ambavyo ni kama biashara lakini vyaangukia katika kundi la huduma. Nakumbuka wakati nikisoma niliwahi kuelezwa sababu tatu za kazi na mojawapo ilikuwa ni kazi ziisaidiazo jamii. Japo watendao kazi hizo hulipwa, lakini bado huwezi fananisha huduma halisi na kipato chao. Na hapo ndipo ukutanapo na wauguzi, zimamoto, walimu nk ambao ukithaminisha kazi zao ni zaidi ya malipo yao.
Sasa hii BIASHARA ya mafuta bado yaonekana kama biashara zaidi ya huduma, japo ukweli ni kwamba ni mafuta yanayoendesha nchi. Ni hayo yanayopeleka nguvukazi kwenye sehemu zao za kazi na kwa kuamua kufunga (kama watuhumiwavyo wenye vituo vya mafuta) ni kusimamisha uzalishaji kwa makusudi. Na hapa ndipo serikali inapotakiwa kuingilia kati na kuhakikisha wauzaji wa mafuta wanatimiza kile wanachotakiwa kufanya. Kna mipaka katika utendaji wa kila kitu na hapa imefikia wakati ambao serikali ni lazima "ivamie" vituo hivi na kulazimisha kufanyika kwa kitu fulani hasa zinapotolewa sababu zinazokinzana taarifa za serikali. Mwanzoni mwa mwezi huu Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa akiba ya mafuta iliyopo ni kubwa ya kuweza kutosheleza mwezi mzima na kushangazwa na hatua ya wafanyabiashara hao kupandisha bei ya mafuta kwa madai kuwa ni adimu.
Sasa sijui kama leo ni siku 13 tangu aseme hivyo ni wapi penye makosa kati ya taarifa za serikali ama matendo ya wamiliki wa vituo hivyo?
Vyovyote iwavyo, serikali inapaswa kuingilia kati maana HII SI BIASHARA TU, NI HUDUMA PIA KWA MANUFAA YA JAMII

2 comments:

Koero Mkundi said...

Kaka Mubelwa, Juzi nusura nilitelekeze gari langu kwenye Petrol Station moja iliyoko maeneo ya mjini.

Hii imekua ni kero kubwa.
Serikali imeyaachia haya makampuni uhuru mkubwa wa kukaa na kupanga mikakati yao ya kuwakomoa wananchi pasipo kuchukuliwa hatua.

Mimi nadhani kuna mahali serikali imekosea, na hapa ndipo ninapokuwa na wasiwasi na wasomi wetu, ubunifu uko wapi?

Hivi wakati hii sheria ya mafuta ikitungwa, hawakuona kuwa hili linaweza kutokea?

Jamani hivi kweli imefikia mahali hata serikali inatunishiwa msuli na hawa wahujumu uchumi, hii ni aibu gani?

Yaaani tumefika mahali mpaka tunahitaji watu wa kutusaidia kufikiri?

Nilipouliza kwenye makala yangu moja pale kibarazani kwangu, kwamba msomi hasa ni mtu wa namna gani?

Nilikuwa tayari nimeshajenga shaka juu ya wasomi tulio nao.

Nangoja nione hatua zitakazochukuliwa na serikali.....

Fadhy Mtanga said...

Tatizo tulilonalo;
Wanasiasa siyo wakweli,
Husema kwa kutazama hali,
Siamini kama wanajali,
Wewe unawaamini?

Na hili nalo tunalo;
Wenye biashara matapeli,
Hututesa bei zao kali,
Wapate faida mara mbili,
Wewe wawatumaini?