Wednesday, January 28, 2009
Twachagua maongezi, maongezi yachagua mawazo na mawazo yatuchagulia jamii
Maongezi yanaweza kuwepo katika namna nyingi ikiwemo ile ya kuongea kwa sauti ama yale yaendeleayo kimyakimya akilini mwetu ambayo wengine wanayaita mawazo. Lakini ni mazungumzo haya ambayo huchukua jukumu kuubwa la kutambua mengi na kutambulisha mstakabali wetu. Ni haya yanayorekebisha mienendo yetu, maamuzi yetu, mawazo yetu, hisia zetu na hata matendo yetu. Ni mazungumzo haya yaendeleayo vichwani mwetu ambayo huanza bila hata ruhusa ya muwazaji, ambayo hupelekea matokeo ya aina mbalimbali. Fikiria mazungumzo yanayokuwepo ndani ya kichwa chako pale uonapo kitu upendacho (awe mtu, gari, nyumba, kazi ama chochote). Hili ndilo husababisha mtu kufuatilia ama kupuuzia kile aonacho. Kwa maana nyingine ni kwamba tuna kila uwezo wa kuchagua aina ya mazungumzo yanayoweza kuwa na ushindi ndani ya vichwa vyetu. Hili laweza kwa kuanza kuchagua watu wakuzungukao ambao kwa namna moja ama nyingine wanaathiri mazungumzo yetu ya nje kisha ya ndani. Pia waweza kuwa makini na namna maongezi ndani mwetu yanavyogawanya matukio na umuhimu wa yaliyopita, yaliyopo na yajayo. Lakini pia katika makundi hayo matatu kuna makundi mengine manne ndani mwake ambayo ni VITU, WATU WENGINE, SISI NA MAHUSIANO.
Watu wengi hujikita kwenye kuongelea vitu (kama magari, nyumba, safari, michezo nk) na watu wengine ( kama wanasiasa, watoto, waigizaji, majirani wafanyakazi wenza, watalaka nk) kuliko wanavyojizungumzia wenyewe na mahusiano yao.
Ukweli ni kwamba maongezi tuanzishayo kichwani huchagua nini tutaendelea kuwaza na hiyo hutufanya tuchague watu tunaopenda kushirikiana nao na hiyo yageuka kuwa jamii yetu.
YAKO NI IPI NA WAICHAGUA VIPI? Yangu ni pamoja na wewe unayemaliza kusoma hapa. Nimeamua kuishi na maisha ya mazungumzo chanya, mawazo chanya na hayo yatanifikisha kwenye jamii chanya. Kwa Ujumla naishi uchanya.
Msikilize Nasio anachosema katika Living In The Positive
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
3 comments:
ndio maana sipendi siasa ambazo hapo kale nilizizimikia. utajikuta ukilaimu tu badala ya kupongeza na kuangalia tatizo lako liko wapi na ulinyofoe. utambuzi ndio elimu muhimu kwani huwa unajiangalia wewe na kujiweka sawa na hivyo kamam wewe uko sawa katika utendaji wa majukumu yako, basi na wengine huwa sawa.
tunalalamika na kusingizia hata makosa yetu kwa wengine. jikague mwenyewe kwanza. I end here, ngoja niendelee kujikagua mzee tehe tehe tehe..... kwiiiiiiiiihhhh
Kaka Mubelwa.
Huu naona ni utambuzi kabisa,
Ahsante kwa mada hii nzuri.
Usione kimya, huwanapita pita humu kuokota mawili matatu kwa ajili ya kujifunza, nakosa muda wa kuweka maoni
Tuko pamoja kaka.
Tchao!!!!!
Mzee wa Changamoto, hapo umesema kweli. Kama alivyosema Kamala, mara nyingi makosa yetu tunawavisha wengine kutokana na uzembe na udhaifu wa kuukubali ukweli; na pengine tu ni kwa sababu ndivyo tunavyofikiri na watu waliotuzunguka ndivyo wanavyotufanya tufikiri. Na kwa kufanya hivyo tunajisikia nafuu - kama vile tumetua mzigo mzito uliokuwa umetuelemea. Ambacho hatutambui ni kwamba tunapofanya hivyo tunapoteza nafasi ya kujikosoa, kujirekebisha na kusonga mbele sisi wenyewe pamoja na jamii yetu. Wakoloni walilitambua jambo hili mapema - kwamba ukitaka kumtawala mtu milele na milele basi korofisha uwezo wake wa kufikiri. Vinginevyo haiwezekani hata kama ungekuwa na silaha za kutisha namna gani. Waulize Wamarekani watakwambia. Mada nzuri hii na uchanya wako uendelee kujieneza na kujitandaza katika jamii.
Post a Comment