Wednesday, February 4, 2009

Dah!! Waandishi wetu jamani.......

Kwanza Michael Steele si Naibu Gavana wa sasa wa hapa Maryland. Alimaliza kipindi chake mwaka 2006 ambapo aligombea u-Seneta wa MD na akakosa. Na pili Bush hakugombea uenyekiti wa Republican na utaratibu wa hapa si kama uliozoeleka nyumbani ambako Rais anakuwa mwenyekiti wa CCM.
Dah!!. Hata kama ni UDAKU. Picha na blog ya Prof Matondo

Ninaposikiliza habari za nyumbani Tanzania (shukrani kwa Da Subi na Dullonet) na hata kusikiliza kipindi ambacho ningetegemea kupata habari "zilizochimbwa" kama kipindi cha HARAKATI toka REDIO YA TAIFA naishia kupata habari za taarifa. Hii inasikitisha saana. Hakuna habari ya maana zaidi ya kueleza yaliyoelezwa.
Nakumbuka katika salamu zake kwa Blogger
Prof Matondo , blogger mwingine Dr Faustine alisema "Waandishi wetu wa habari Tanzania wanajitahidi lakini stori nyingi ni 'narrative" na hazina "facts" na depth", hivyo kuzua maswali mengi kuliko majibu." Na huo ndio ukweli na sina la kuongeza katika ukweli wake. Waandishi wa nyumbani wengi wao ni wavivu wa fikra na hawatafuti ukweli wa kile wanachoripoti. Hakuna kufuatilia na wala kuwekeza katika habari fulani zenye umuhimu kwa wengi. Ni suala la kufuata wengi wanapenda nini na kuwapa wapendacho hata kama si kwa manufaa yao. Vyombo vya habari kufuata upepo na kwa bahati mbaya wa wale ambao hawatafuti kweli ya nini kinatokea.
Yaani kuanzia taarifa ya habari mpaka vipindi vya ripoti utasikia "akiongea na waandishi wa habari,,,," ama "katika taarifa yake..." ama akizungumza kwa niaba ya kiongozi huo..." ama aina nyingine ya habari ya taarifa ambayo haijachunguzwa na yeyote. Hakuna habari zaidi ya MAELEZO na mikutano iitwayo na viongozi. Hakuna wataalamu wa kutosha kuendesha mahojiano ambao wana elimu na wanajua undani wa waulizacho. Hakuna wachambuzi wa masuala mbalimbali na hilo linapelekea kuripoti bila kuhoji. Habari za michezo ndio zasikitisha zaidi maana wanamaliza karibu kipindi kizima kusimulia mpira uliioneshwa kwenye Tv na bila kukupa habari zozote za kitaalamu na hata takwimu juu ya kilichotokea ama kinachoweza kutokea kutokana na matokeo ya mechi ama mpambano huo.
Inasikitisha saana na pengine ndio maana blogs na forums zinakua kwa kasi kwa kuwa zinafumbua mengi yenye uhitaji kuliko redio na magazeti yetu. Lakini kama tunalipa kodi inayoendesha Redio kama TBC kwanini wananchi wasipatiwe watu wenye taaluma ya kuvumbua tatizo na kupendekeza suluhisho?
Sijui

7 comments:

Simon Kitururu said...

Kazi ipo!:-(

Koero Mkundi said...

mfumo wetu wa elimu ndio umepelekea yote hayo.
Tulifanywa wajinga na akili zetu zimefifishwa ili tutawaliwe kiulaini.
Hivi sasa dalili za kuerevuka zimeanza kudhihiri na ndio maana tunashuhudia migogoro na migomo katika sekta za elimu, hii yote ni kutokana na vijana kushitukia dili la wanasiasa wetu.
Tunahitaji mapinduzi makubwa katika mfumo wetu wa elimu la sivyo hatutaishia kuwashangaa waandishi wetu wa habari tu.

MARKUS MPANGALA said...

dUH! umenikumbusha kitu, najaribu kuandaa kuwahoji waandishi wa habari katika mfumo wa makala itakuwa hivi WAANDISHI WA NI MAIMUNA? nashindwa kuelewa habari kama hiyo iliyopo hapo, nachanganyikiwa kuwa habari hizo wanapata wapi ambazo zinakosa kuchimba. Yapo mengi sana na kuna mmoja ya wanahabari alisema waandishi wanaandika hadi takataka katika vyombo vya habari. Ngoja namini dada Koero atanisaidia hoja bila kukosa. Hatufikiri,hathoji,hatujisumbui na tunakula kilichopaswa kuliwa!

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Je, kuna adhabu yo yote ambayo mwandishi anaweza kupewa kwa kuandika habari ambazo si za kweli? Kusema kweli kwa hali ilivyo sasa kwa Tanzania ni vurugu mechi kwani mtu huwezi kujua upi ni udaku na zipi ni habari za kweli zilifanyiwa uchambuzi wa kina. Ni uhuru uliopindukia kimo sijui. Zamani kulikuwa na gazeti la Rai chini ya Jenerali Ulimwengu. Lilijibidisha sana kuandika makala nzuri zilizofanyiwa uchambuzi wa kutosha. Sijui sasa gazeti hilo lina hadhi gani tangu akina Jenerali Uliwengu waondoke huko. Kwa walioko Tanzania, ni gazeti gani ambalo linaandika habari kwa kina kabisa ambalo mtu unaweza kusoma ukaridhika? Kama alivyosema dada Koero, kuna mambo ya msingi kabisa katika mfumo wetu wa elimu na maisha kwa ujumla katika jamii ambao unahitaji kufanyiwa kazi kwani ukosefu wa umakinifu unaoonyeshwa katika haya magazeti upo karibu katika kila sekta. Tufanyeje?

Faustine said...

Tatizo la waandishi wa Bongo linachangiwa na elimu duni isiyowawezesha kupambanua mambo. Pili, waandishi wanalazimika kuandika kutokana na matakwa ya weye vyombo vya habari lakini vile vile kuna nidhamu ya uoga ya kuogopa kuandika ukweli hata pale kunapokuwa na ushahidi wa kutosha.
Nadhani kuna haja ya kuboresha elimu ya waandishi wa habari, journalism ijengwe kuwa profession inayoheshimika badala kuwa ni taaluma ya makanjanja.
Aidha kuna haja ya kuwa na uhuru wa waandishi wa habari, waandishi wafanye kazi zao bila ya kuingiliwa na wamuliki.
Ni hayo tu kwa leo.
Mdau
Faustine
http://drfaustine.blogspot.com/

Simon Kitururu said...

Ukiweza tafuta movie iitwayo Shattered Glass imuongeleayo Mwaandishi Stephen Glass ambaye alikuwa anatunga hadithi na kuziripoti kama facts. Kwa kifupi kidogo kuhusu hadithi hii cheki:
http://en.wikipedia.org/wiki/Stephen_Glass_(reporter)

Anonymous said...

Mubelwa, ukitaka movie aliyoitaja Simon nifahamishe.