Wednesday, February 11, 2009

Gari moja = matrekta 20. Uwiano mzuri, malengo mazuri, utekelezaji ........


Serikali imesema katika mwaka ujao wa fedha wanategemea kuweka mkazo zaidi katika kununua magari ambayo yanaisaidia zaidi jamii na kuongeza ufanisi katika kilimo na si yale ambayo wamekuwa wakinunua kila mwaka kwa ajili ya watendaji wake.
Katika mahojiano yake kuhusu mwaka mmoja aliokaa ofisini yaliyorushwa na kipindi cha MCHANA HUU cha redio ya taifa TBC ( yanapatikana Dullonet Feb 12, 2009), Waziri Mkuu mheshimiwa Mizengo Pinda amekiri kuwa "katika mifumo ya bajeti, tunazo pesa zinazoweza kupunguza matatizo ya kweli ya watanzania, lakini sehemu kubwa ya fedha hizo haziendi huko na badala yake zinakwenda katika maeneo ambayokwa sehemu kubwa kabisa yanatuhusu sisi watendaji na viongozi". Mhe Pinda amesema alipopitia orodha ya maombi iliyopelekwa hazina amegundua kuwa magari ya viongozi ndiyo yaliyochukua sehemu kubwa ya kipaumbele na kuyapa kisogo magari ya wagonjwa, matrekta na magari ya zimamoto hivyo akaamua kuwa hizo bilioni 50 zilizotengwa kwa ajili ya magari ya viongozi na ambayo huhitajika kununuliwa kila mwaka zitumike kwa malengo mengine japo wa miaka miwili ijayo kwa manufaa ya wakulima na wafugaji.
Amesema amegundua kuwa awapo ziarani, kila gari moja linakaribia thamani ya matrekta madogo 20 na kuamua kuwa ni bora kwa mkulima kupata matrekta kuliko ofisi yake kuendelea kugawa "mashangingi" kwa viongozi. Amesema ni mahesabu tu ambayo anataraji kukaa na viongozi wenzake serikalini na ana imani kuwa "kwa hakika tukiamua jambo hili, linawezekana".
Waziri mkuu amesema "tumedhamiria kuwa bajeti inayokuja, kama kutakuwa na ununuzi wowote wa magari, basi yatakuwa yale yanayomlenga zaidi mtanzania wa kawaida. Magari ya wagonjwa, magari ya zimamoto, magari ya kuzoa taka ngumu na taka za kawaida, vitu abavyo naona ni kero ya kila siku hapa Tanzania."

Ni kweli kuwa kuna baadhi ya miji na manispaa ambazo hazina magari ya zimamoto wala vizoa taka na vikusanya taka ngumu, na kuna uhitaji wa zana za kilimo nchini kote, hivyo kuliona hili ni hatua kubwa sana na nampongeza saana Waziri Mkuu kwa kuliona hili na nampongeza kwa "utafiti" huo ulioleta namba ya uwiano wa magari. Pia nafurahi na nasubiri kusoma bajeti ijayo kuona ni yapi kati ya yaliyosemwa hasa hili la "kuwanyima" viongozi "mashangingi" mapya. Maana mara zote viongozi wamesema na kutoa kauli nzuri, zenye mvuto na matumaini na kisha utekelezaji hauonekani.
Changamto yetu sote ni kuweka kumbukumbu za haya na ukifika wakati basi TUHOJI UTEKELEZAJI WA AHADI HIZI KWA UPENDO NA HESHIMA.

1 comment:

Subi Nukta said...

Hadi sasa hatujaanza kuwadai deni za ahadi zao. Siku harakati hizo zitakapoanza, hapatakalika hapo wanapopakalia sasa. Siku inakuja, heri yao wenye kuzijua nyakati na majira yake.