Wednesday, March 4, 2009

Labda hatuendelei kwa kuwa wa kutuendelesha hawako kwenye kiendesheo chetu

Sijakutana nao lakini pengine wapo wanaoamini kuwa mfumo wetu wa elimu unaweza kumuandaa ama kuwaandaa wengi kufikia malengo ya kufanya kile ambacho wanatamani kufanya na ama kuwa wanavyotaka kuwa. Kwa bahati mbaya mimi siamini hilo.
Natambua kuwa MFUMO WETU WA ELIMU HAUTUFANYI KUWEZA KUFANYIA KAZI VIPAJI / KARAMA ZETU na hili laweza kuwa na athari zaidi ya tuonavyo ama tudhaniavyo. Mfumo wetu wa elimu unachanganya utii wa mila, desturi, tamaduni na imani za kidini na kuwafanya wenye "neno la mwisho" kutuamulia mustakabali wetu.
Nimeshuhudia wengi wakielekea kwenye UALIMU kwa kuwa tu maksi zao hazikutosha kusonga mbele. Japo walikuwa na ndoto nyingine wanaishia kwenye ualimu. Wapo waliobambikwa kwenye u-nesi ule wa "one year course" kwa kuwa tu kulikuwa na nafasi huko na alama zake za kuendelea na masomo atakayo hazikutosha.
Labda ujiulize ungepata nafasi "ya pili" ya kukuwezesha kufanya kazi upendayo, ungebaki na hiyo uliyonayo? Unafikiri ufanisi wako ungekuwa sawa na wa sasa ulipo kwenye kazi usiyoipenda toka moyoni? Kuna athari nyingi za kufanya kitu kwa kuwa tu unahitaji pesa na hii inafanya kutokuwa na moyo wa kazi, kutokuwa na uaminifu kazini na suala la ufanisi kwa ujumla. Sijui ni wangapi wameshawahi kujiuliza kama kazi afanyayo ni chaguo lake la kwanza la kazi ulimwenguni (ama niseme kwa mazingira aliyopo) ama ni ukata tu.
Kibaya zaidi ni pale tunapogundua kuwa hata baadhi ya wanasiasa hawana ujuzi, moyo, utashi, wito wala mvuto wa siasa bali ni kwa kuwa kuna "njia nyooofu kuelekea ufisadini". Siasa imegeuka "ufisadi na ubinafsi streets". Na hawa wanasiasa hawana tofauti na wengine linapokuja suala la athari za kufanya usicho na karama ama kipaji na utashi nacho na ndio maana hawana fikra endelevu na wanawaza kujinufaisha zaidi.
Angalia wanavyolala Bungeni na kujikusanyia pesa za kutisha. Wanavyotumbua kwenye ziara ilhali kuna wahitaji majimboni mwao. Wanavyoziarika kila kukicha tena nje ya majimbo yao na kusahau wajibu wao. KIBAYA ZAIDI WANAVYOTUNGA SHERIA na kutetea ama kuchanganua nyingine zinazoathiri maisha ya mTanzania wa leo wakati wao hawana wito na nafasi hizo. Ndio maana ni mara chache saaana kukuta migongano ya mawazo ndani ya bunge juu ya kitu kinachoihusu jamii. Linalojaliwa ni SIFA YA M'BUNGE na si maendeleo kwa jimbo na wananchi waliomuweka hapo.
Sasa kama wabunge na viongozi wetu wamejiingiza huko kwa athari za mfumo wa elimu, na wako huko wakilitumikia taifa bila ufanisi kwa kuwa hawana wito, utashi wala uwezo na masuala waliyokabidhiwa. Na zaidi ya yote wanaonekana kama "kioo" ama "wawakilishi" wa huko wanakopatia hizo kura, si tuna hali mbaya? Kuna swali jingine la kwanini hatuendelei? Si ni kwa kuwa walio na dhamana hawana fikra pevu maana utendaji wao wa kazi ni sawa a Mubelwa anavyokariri hesabu ili afaulu mtihani? Mmhhhhhh!!!!!
LABDA HATUENDELEI KWA KUWA WA KUTUENDELESHA HAWAKO KWENYE KIENDELESHEO CHETU.

4 comments:

Koero Mkundi said...

Hii article imenigusa sana.
Ahsante sana kwa kuliona hili na kulisema.

Albert Kissima said...

Kwa bahati mbaya sana sisi watanzania tumeshapandikizwa dhana ya "struggle for existance" pia ile ya "survival for the fittest" na ndio maana wenyewe kwa wenyewe tunakandamizana,wengi waumie kwa manufaa ya mmoja.
Kama ulivyotangulia kusema Kaka Mubelwa,kufanya kazi usiyoipenda,yani kwa vile tu imelazimu,ni tatizo kubwa sana.Hili ni miongoni mwa matatizo makubwa kabisa yanayoikabili sekta ya elimu.Asilimia kubwa ya walimu hawakupenda kuwa walimu.Kwa maana hii hata kufundisha inakuwa si kwa moyo wala kujitolea,yani bora liende,wengi wakiwa na mawazo ya namna gani wataachana na ualimu.Ndio maana ualimu siku hizi si wito tena.
"hivi ni wanafunzi wangapi waliopata 1 za 7 au 1 za 3 na wakaamua kwenda vyuo vya ualimu?
Kaka karibu sana pale kwangu kuna mjadala unaosema "wengi hawapendi kuwa walimu,wanalazimika"

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli wengi hawaoni kama hatuendelei kwa vile wao "waubwa" wanachukuwa maendeleo yote. Hakuna maendeleo kabisa. Juzi tu wakati nipo nyyumbani nilishangaa sana wananchi walikuwa wanagawiwa mbolea. Mbolea ya kampeni.

Na kuna jambo jingine ambali watu wengi huwa wanajishusha hadhi wanyewe kwa kusema sisi waafrika"TZ" elimu yetu ni ndogo sana kuliko wenzetu wazungu. kwa nini nani amesema hili? Kwa nini hatujiamini? basi isije nikapitiliza somo

Ivo Serenthà said...

Obviously they would not have thought that the plane went down well

Hello my friend

Marlow