Tuesday, March 24, 2009

Mimi na yeye sote tuko sahihi. Na sote hatuko sahihi

Umeshawahi kuwaza kwa sauti?
Nakumbuka hili lililonisibu wakati fulani wa harakati za kusaka maisha. Nilikwenda kwa daktari wa meno kwa kuwa nilihitaji huduma ya kile nilichoamini kuwa ni kung'oa jino lililokuwa likinisumbua saaana. Na wakati huo nilikuwa sijawa na bima ya afya (kwa wale mjuao gharama za afya hapa mnaweza kuanza kuhisi ..). Baada ya vipimo vya awali nilivyolipia mamia kadhaa ya dola, Daktari akaniita na kunikalisha chini kisha kunipa uchambuzi wa nini kimefanyika na nini kinahitaji kufanyika kabla ya kung'oa jino lisumbualo na kisha kukinga mengine.
Well! Ulionekana mpango mzuri saana na nilielekea kuuafiki maana ulisikika (sounded) kama wenye kunifanya niwe na "kinywa chenye afya". Kwa hiyo akaanza na nini cha kufanya, kwanini natakiwa kufanya na ni yapi yatanikuta nisipofanya. Kisha akaanza kuzungumzia ni lini vyote vinaweza kufanyika (na hapo alikuwa na kitabu cah miadi mbele yake). Mwisho akaja kwenye gharama. Kuwa mambo haya yoote ambayo ni MUHIMU NA LAZIMA kuyafanya yangenigharimu takribani dola 4,000.
Kwanza jino likapona (ama niseme likafa ganzi) kwa gharama ambazo sikuwahi kuzifikiria, kisha tukazungumza namna ya kuweza kukabiliana na gharama hizo ambazo tayari nilishaona ni kubwa. Baadae nikaamua kuwa nisingeweza kuzimudu kwa wakati huo hivyo ntakwenda kununua dawa ya kutuliza maumivu nitumie wakati nakusanya pesa na natafuta bima.
Kichwani nikawa na maswali mengi kuwa
1: Kwanini huyu mtu haoni namna ninavyoteseka? Ni kweli kuwa nilikuwa naumia na nilikuwa na nia ya kuwa muaminifu kumlipa kama angeweza kunisaidia kunitoa jino hilo. 2: Kwanini ama kipi kimfanye yeye aniamini? Ni wangapi wamekwenda pale wakiwa na matatizo kama yangu na pengine zaidi ya yangu na labda wengine walishindwa kutimiza ahadi zao? 3: Kwanini huyu Daktari atangulize pesa kuliko utu? 4: Kwanini nimfanye daktari anayelipa wafanyakazi na gharama za jengo na uendeshaji anihudumie bila malipo kamili papo kwa papo ilhali ana ankara za kulipa?
Maswali haya manne yakanifanya nitambue kuwa nimegota kwenye wakati usio wa kulaumiwa, Wakati ambao si mimi wala yeye anayepaswa kulaumiwa japo si mimi wala yeye aliyeridhika na nia hasa ya sisi kukutana. Kwa swali la kwanza na la tatu nilikuwa sahihi. Lakini kwa swali la pili na la nne yuko sahihi.
Nikajikuta kwenye hali ambayo ukiiangalia kwa undani ninagundua kuwa kwa upande fulani (yaani upande wa kila mmoja wetu kuhusu sisi wenyewe) mimi na yeye tuko sahihi lakini pia kwa upande mwingine (yaani upande wa kila mmoja wetu amtizamavyo ama kumfikiria mwingine) mimi na yeye hatuko sahihi.
CHANGAMOTO YETU sasa ni kutambua kuwa namna nzuri ya kutambua "mzigo" unaotaka kumtwisha yule unayetaka akutendee kitu ni kujiweka katika nafasi yake na kufikiria namna ambavyo wewe ungejihisi kama angekuwa anakuomba umuombacho wewe. Nikakumbuka nilichowahi kuuliza hapa kuwa NI KWELI SOTE TU WABINAFSI?(bonyeza hapa kusoma nilichouliza.
Najiuliza kama niko sahihi kuwa yawezekana kuwa hakuna mwenye makosa katika mambo mengi kama tu tutaamua kuangalia pande zote za uamuzi.
Wewe waonaje?
Tukutane "next ijayo."

11 comments:

Subi Nukta said...

Wewe una sababu zako. Daktari naye ana sababu zake. Sawa sawa.
Mi bado sijajua hadithi ya jino imeishaje? umeng'oa ama lilipona kabisa lenyewe? Pole kwa maumivu, na hayo uliyoenda kuyapata kwa daktari juu ya gharama, pole tena.

Mzee wa Changamoto said...

Dada Subi. Niliendelea na "matibabu" na bahati nzuri wiki kadhaa mbeleni nikabadili kazi na kuwa na hii niliyonayo ambayo ilinipa bima ya afya na nikafanikiwa kuling'oa kwa gharama ya takribani dola mia. Lakini kilichonifanya niikumbuke hii hadithi ni kuwa kwa kuwa nilikasirika, hata nilipopata bima sikutaka kurejea kwake, nikaenda kwa dk mwingine aliyenitibu na kutohitaji kufanya mengine yote. Sitaki kuamini kuwa yule wa kwanza alikuwa ana mpango wa kunilia pesa maana yawezekana huyu wa pili ndiye asiyejali zaidi ya kile unacholalamika. Ila leo nimekutana na huyo Dk wangu wa $4000 ndio nikakumbuka kuwa sikustahili kuwa na kinyongo naye kwani alitenda ambavyo wengi wetu tungefanya.
Na nadhani ananijali maana ni miaka kadhaa sasa tangu niwe kwake na bado ananitumia kadi zote ziendazo kwa "wateja wake wengine".
Hapa pia kuna swali. Ni kweli Dr wangu wa zamani ananijali ama anataka pesa ama alikuwa akitafuta kitu cha "kunikamua" ama huyu wa sasa ndiye hajali?
Mmmhhh. Namna uonavyo tatizo ........

Subi Nukta said...

Ikiwa umepata tiba na maumivu kwa sasa hakuna, vyema. Ama kuhusu nani mkweli na nani siye, huwezi kubaini kwa urahisi, yakubidi kuperuzi kuhusu suala lako kisha utafute maoni ya mtu mwingine kwa sababu jambo gumu mara nyingi huamuliwa kwa mashauri ya zaidi ya angalabu watu wawili. Watu wa Marekani nao hudadisi sana hadi ikawa tabia yao ni kuzunguka kwa huyu na yule wakaranda hospitali hadi hospitali mpaka wampate atakayewaambia yale wanayotaka kusikia, isije ikawa ushaambukizwa tabia hiyo nawe.
Uzuri ni kuwa jino limetibika, hiyo ndo iliyokuwa shaka yangu, mengineyo ni ya kusherehekea baada ya kupamba.

Koero Mkundi said...

kaka Mubelwa Pole sana.
Hata mimi nimefurahi kusikia kuwa jino lilipona.
Hadithi za gharama za matibabu huko ughaibuni kwa kweli zinatisha sana.
dada yangu aliwahi kwenda huko kusoma simulizi zake zilinitisha kiasi kwamba ninaogopa sana kutia mguu.
Huku kwetu hata ukiwa na elfu tano tu umepona.

Yasinta Ngonyani said...

pole sana, maana gharama za haya meno duh kazi kweli kweli

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

bora ufe lakini mia yangu huilipe na jamaa alikuwa akimdai mshikaji, hali ikazidi kuwa mbaua, akamwambia, "obanze ompe amahela gange oijo'fe" nime pesa yangu kwanza ndipo ufe.

ni ulimwengu wa kapitalizimu, pesa na maliza dunia ni muhumu kuliko wenzio, nani kabishi?

lakini ni ujinga kwani haitokaa iwe hivyo

Anonymous said...

hi.. blogwalking. by the way, happy birthday to your sister :)

Anonymous said...

Ubinadamu kweli umepungua au kuisha kabisa.Leo nimepata mkasa ulionishtua sana.
Ninauguza mgonjwa na anatumia sindano,nimetafuta mhudumu wa kumchomea sindano nyumbani'nesi'
Dawa anazotumia mgonjwa wangu ni za gharama kubwa kiasi.Leo asuibuhi nesi kaiba dawa za mgonjwa!

Mzee wa Changamoto said...

Dah!! Pole sana Kaka Fred. Unakumbuka uliyosema kwenye DUNIA IMANI IMEKWISHA? Ntawashirikisha wadau tuone wanasemaje.
Pole sana na pole kwa mgonjwa pia

Anonymous said...

Mzee wa Changamoto; nina hadithi kama ya kwako ingawa yangu ni tofauti kidogo. Nilipokuwa mgeni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA) niliwahi kwenda kwa mganga wa meno kwani gego moja lilikuwa linaniuma. Basi naona masekretari wake walisahau kuniuliza mambo ya bima. Kila kitu kiliandaliwa, mpaka nikalazwa kwenye kiti na vifaa vyote vya kuchokonolea meno na X-ray vikawa tayari tayari. Kabla sijafungua mdomo ndipo daktari akakumbuka na kuniuliza kama nilikuwa na bima. Nilimwambia kwamba nilikuwa sijui kwani ndiyo tu nilikuwa nimefika kutoka Tanzania. Basi ukawa mwisho wa kila kitu na nilitoka nimeshikilia shavu kwani jino lilikuwa linaniuma kweli kweli. Baadaye niligundua kwamba mfadhili wangu angeweza kulipa gharama zote, nilirudi kwa daktari yule yule na alinitibu vizuri sana mpaka tukaishia kuwa marafiki.Japo nilisonya sana nilipokataliwa matibabu lakini nadhani sikuwa na haki ya kufanya hivyo...

Koero Mkundi said...

Hadithi ya Katawa na Nesi mwizi wa dawa inahuzunisha lakini inachekesha kidogo,

Kuna rafiki yangu mmoja anae mdogo wake teja, sasa kaka yao akapata TB, si akawa anatumia vidonge, kwa kuwa maendeleo yake yalikuwa ni mazuri akapewa zile dawa ili akatumie nyumbani, yule teje si akaziiba na kwenda kutafuta wateja wenye maduka ya dawa, alikamatwa baada ya mwenye duka kuwastua kwa kuwa alikuwa anawafahamu!!!!