Thursday, March 26, 2009

Ni kweli kuwa kuna bahati mbaya?

Mwishoni mwa mwezi Januari niliwahi kuuliza HIVI KWELI KUNA BAHATI? NA KAMA IPO SI NI LAZIMA IANDALIWE? (Bofya hapa kuisoma). Nikapata majibu na mitazamo mingi. Lakini ni kama vile niliangukia upande mmoja wa kile kiitwacho bahati na sasa nigeukie kwingine ambako hata Kaka Kamala kwenye maoni ya mada hiyo aliuliza. Alisema na hapa namnukuu kuwa "bahati mbaya, bahati nzuri. kama hakuna bahti, je kuna mkosi? sijui lakini tafsiri yako ndo ina mata zaidi ya bahati". Nikapata somo. Wiki iliyopita katika maoni juu ya wimbo wa Luciano uitwao Amen, Kaka Matondo akaonika kuwa "Daima huwa nawaza: ni kwa nini "wacheza rafu" ndiyo hufanikiwa zaidi katika maisha kuliko wafuatao kanuni za mchezo?" Likawa swali zuri kuwa ni kweli kuwa kuna bahati mbaya ama watu huwa hatuishi muda mrefu kuona mwisho wake? Niliwahi kuuliza maswali haya nilipotoa maoni kwa Kaka Kaluse juu ya kufikiri kuhusu tatizo badala ya suluhu kuwa
Ni mfumko wa bei unaoleta sera bora za kudhibiti, ni kifo cha fulani kinachotupa nafasi ya kumfikiria mwingine ambaye anaweza kuwa na changamoto mpya na za kisasa na sahihi zaidi ziendanazo na mahitaji.
Ni makosa ya fulani yanayoboresha sekta nzima.
Umeshajiuliza ni wangapi walikufa katika kupigania uhuru unao-enjoy sasa? Kwao yale yalikuwa matatizo lakini lengo lilikuwa kuwa na dunia tuliyonayo sasa kwa namna ilivyo.
Umeshajiuliza ni wangapi walikufa kwa matatizo yaliyokuwepo kwenye ndege za mwanzo? Ni uboreshaji uliotokea wakati ule ambao unatufanya tusafiri kwa haraka na (pengine) salama kuliko wao. Lile lilikuwa ni tatizo kwao japo ni faraja kwetu.
Unajua ni wangapi wamekufa wakihangaika kuufanya umeme uwe salama na kompyuta zifanye kazi nzuri mpaka ukaweza kusoma "mtazamo" wangu juu ya hili? Ndugu zao waliliona hili kama tatizo ambalo liliwachukulia wapendwa wao japo lengo lilikuwa ni kupatamawasiliano tuliyonayo sasa.

Pengine kila lionekanalo kuwa tatizo lina suluhisho wakati wake ukifika. Naamini kina Wright waliovumbua ndege walikumbana na "matatizo" ambayo leo hii wakiweza kufufuka wangeshangaa namna ambavyo yamedhibitiwa, lakini labda wasingeyagundua tusingepata wa kufikria walichofikiria.
Sijui kama ni mtazamo wako ama la, lakini kuna misukosuko ambayo pengine si yote lazima iitwe matatizo na kama tukifikiria suluhisho zaidi ya tatizo tunaweza kufikia mwisho wake ama kupata ufumbuzi wake mapema zaidi.
Lakini vyovyote iwavyo, liwe ni TATIZO AMA BAHATI MBAYA, naamini tunaweza ku-set akili zetu kuwa tutaweza kuyashinda. Maisha yetu ndivyo yalivyowekwa, kupambana na mengi ili tukue. Ni vema kuwa na mtazamo chanya wa kushinda kila TATIZO ama BAHATI MBAYA ijayo kwetu.


Blessings

3 comments:

Koero Mkundi said...

Huu mtazamo nimeupenda.......

"Umeshajiuliza ni wangapi walikufa katika kupigania uhuru unao-enjoy sasa? Kwao yale yalikuwa matatizo lakini lengo lilikuwa kuwa na dunia tuliyonayo sasa kwa namna ilivyo.

Umeshajiuliza ni wangapi walikufa kwa matatizo yaliyokuwepo kwenye ndege za mwanzo? Ni uboreshaji uliotokea wakati ule ambao unatufanya tusafiri kwa haraka na (pengine) salama kuliko wao. Lile lilikuwa ni tatizo kwao japo ni faraja kwetu.
Unajua ni wangapi wamekufa wakihangaika kuufanya umeme uwe salama na kompyuta zifanye kazi nzuri mpaka ukaweza kusoma "mtazamo" wangu juu ya hili? Ndugu zao waliliona hili kama tatizo ambalo liliwachukulia wapendwa wao japo lengo lilikuwa ni kupatamawasiliano tuliyonayo sasa."

Anonymous said...

Ni kweli. Katika tatizo ndimo mna suluhisho pia. Ndiyo maana tunasema kwamba kulitambua tatizo ni hatua muhimu katika utatuzi wake (ati, asiyejua na hajui kwamba hajui atasaidiwaje?). Kwa mantiki hii hakuna tatizo kuu kumshinda binadamu - pengine tu wakati wake wa kufumbuliwa haujafika. Naamini kwamba kinga na tiba ya UKIMWI, kansa na magonjwa mengine yanayotuchachafya leo itapatikana. Watu wa cryogenics wanaamini kwamba siku moja binadamu atakishinda kifo na wataweza "kufufuliwa" tena. Yote haya yatawezekana kutokana na watu wengine kujitoa mhanga. Na wengi wa mashujaa hawa hawako katika vitabu vya Kihistoria na majumba ya makumbusho. Ni watu tu wa kawaida kama mimi na wewe!

Digna Abrahamu said...

Habari za hapa.

Nimepita hapa kibarazani kwako kujitambulisha kuwa nimefungua kijibaraza changu kitakachokuwa kikijihusisha zaidi na masuala ya vijana.
Nimekuwa ni msomaji wa blog yako kwa muda mrefu, na sasa nimeamua na mimi nijitose uwanjani ili kuongeza mchango katika kuielimisha jamii.
Niko tayari kuelimishwa na kukosolewa pale nitakapoonekana natoka nje ya mstari.
Natarajia ushirikiano wako.

Digna