Ndio asili ya ULIMWENGU kuwa na yale yaonekanayo kuwa mema na mabaya. Lakini si mtazamo wa kila mmoja kuwa kuna jambo jema na jambo baya. Ninalomaanisha ni kuwa unaloona ni jema laweza kuwa baya kwa mwingine na kinyume chake kikawa sahihi. Naamini ndio maana hatuna SHUJAA WA DUNIA maana akisisitiza hili lazima litawaathiri wengine.
Kwa maana hiyo uwezekano wa jema na baya wategemea namna uonavyo na namna utakavyolikabili na hiki ndicho kigezo kikubwa cha kuwa utakavyokuwa. Natambua kuwa tuko tulivyo kutokana na historia yetu na kwa ajili ya mustakabali wetu. Kwa hiyo kuyakabili makwazo kwa mtazamo chanya ni jambo la muhimu na pengine LA LAZIMA kwa wapenda matokeo mema.
Nimemaliza kusoma makala ya Da Koero kuhusu Da'mdogo Yasintha. Na katika kusoma maoni nikagundua kuwa wengi tunakubaliana kuwa Da Yasintha angeweza kukata tamaa, angeweza kujiuza kama wengine na angeweza kufanya mambo mabaya ambayo yangehatarisha maisha yake. Lakini akaamua kuwa na mtazamo chanya wa kuyakabili maisha. Na sasa lile lililoonekana kama BAYA / KWAZO AMA BAHATI MBAYA kwake linakuwa kama CHANGAMOTO kwa maisha yake na yetu sote. KUMBE NI MTAZAMO WA JAMBO ULETAO MANUFAA / BALAA KWA JAMII.
Tukumbuke kuwa maamuzi tutendayo yanaweza kuwa na athari canya ama hasi kwa jamii yetu bila sisi kujua. Naomba nitoe mfano huu wa Dada Yasintha kueleza nionavyo mimi. Tumemsoma Da Yasinta kupitia Da Koero ambaye alianzisha blog baada ya wao kusimamishwa chuo. Sidhani kama ilikuwa kitu chema kusimamishwa chuo, lakini kilishatokea na akaamua kusonga mbele tangu hapo. Nimesoma jinsi Masudi Kipanya anavyoibua vipaji baada ya kufukuzwa / kusimamishwa Clouds Fm. Tumesoma namna watu wengi wanavyojenga heshima na kuisaidia jamii pale ambapo kunaonekana kuwa na tatizo na hapo kupata mawazo na fikra mpya za kuisaidia jamii. UJASIRI NA UVUMILIVU ALIOUONESHA DA YASINTA NI USHUHUDA TOSHA KUWA TUNAWEZA KUKABILIANA NA MENGI TUKIJIPANGA VEMA. Ni wangapi wenye kutengeneza / kulipwa pesa nyingi zaidi yake wasioweza kujenga nyumba ya hadhi aliyonayo? Lakini alijipanga na kutimiza mipango hiyo ambayo chanzo chake ni mateso / matatizo aliyokumbana nayo aliposhindwa kwenda shule mpaka alipopata kazi ya ndani iliyomfanya akimbie.
Ni lazima tukatae kuwa kuna "mwisho" wa mafanikio yetu. Ni lazima tukubali kukabiliana na mabadiliko yatujiayo na tuyakabili tukiwa na mtazamo chanya wa kufanya vema. Narejea niliyosema Jumapili kuwa "kila mwisho wa bonde ni mwanzo wa mlima" na mateso anayopitia mwanadamu mara zote huwa na suluhisho, linalotakiwa ni kuvumilia na kufikia mwisho wake. Miaka yote Yasinta aliyohangaika akiwaona wakinadada wakitengeneza pesa kwa kujiuza angeweza kuamua kukurupukia maradhi na kupata pesa ya haraka, lakini alivumilia.
Nakumbuka nilisoma pia historia ya kundi moja la Reggae liitwalo Israel Vibration. Hawa ni vijana ambao wamefanikiwa kiasi katika Reggae ulimwenguni lakini walikutana na kuanza kupanga ndoto zao hizo walipokuwa wakihudhuria kliniki ya polio. Unaweza kuona namna ambavyo twaweza kubadili tatizo kuwa ushuhuda kwa wengi.
Naamini kulikuwa na mpango katika maisha ya Yasinta kama ambavyo kuna mpango katika maisha ya kila mmoja wetu iwapo tu tutaamua kuwa na mtazamo chanya wa kile tuaminicho kuwa ni tatizo.
Ukiamua kuchukua matusi utukanwayo ukayatafsiri vema na kwa upole, utagundua kitu kuhusu wewe ambacho kinawafanya wengine wakuhusishe na matusi ama kashfa hizo. Na hata kama si kuhusika moja kwa moja, pengine kuonekana na wahusika kwakuweka kwenye mazingira hayo. La muhimu ni kutafsiri na kutafakari vema yale yote yatujiayo na kisha kuyapambanua kwa busara maana ni mchanganyiko wa MEMA na "MABAYA" utuleteayo matokeo yote maishani.
Live in the positive, cause i know good will conqure evil
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
5 comments:
Ni kweli uvumilivu katika maisha ni muhimu sana. Sote tunajua mvumulivu hula mbivu. Na pia katika maisha lazima kuwa na msimamo, pia kujiamini lakini ukisha yumba tu tayari kila kitu kitakuwa ovyo.
hakuna jambo zuri wala baya bali tafsiri yako tu. k
Hola SeniĆ³r...
Kila mtu ana kiwango tofauti ya kuvumilia na akili zake za kutafuta atakavyoishi hapa duniani. Kila mtu ana simulizi lake... awe muuza njegere au daktari...tatizo ni kuwa binadamu hatosheki!!!
Nimesoma na nimejifunza,
Ahsante sana kwa kusherehesha
Niliwahi kuandka kuwa kwa nini tufikiri kuhusu tatizo? Nitanukuu...
"Maisha haya yangekuwepo bila matatizo ni wazi yangekinaisha haraka sana. Yangekinaisha kwa sababu yasingekuwa na maana yeyote. Maana na utamu wa maisha upo katika kupambana na mazingira na kupata ufumbuzi wa jambo. Kitendo cha kupata ufumbuzi wa jambo na kusonga mbele ni kitendo chenye kushika maana halisi ya maisha. Kitendo cha kupambana na kushindwa pia ndo maisha yenyewe. Kama ingekuwa kila anachotaka mtu anakipata maisha yangepoteza maana yake.Ina maana kwamba kila mmoja kati yetu ni mtaalamu wa matatizo kwa maana kwamba anafahamu kwa vitendo. Lakini kwa bahati mbaya siyo wote kati yetu ambao tunaweza au kujua namna ya kuyatatua matatizo yetu, lakini mbaya zaidi namna ya kufanya matatizo yasituharibie maisha yetu. Kwa kuwa matatizo ni sehemu muhimu katika maisha yetu ni wazi hatuwezi kuyakwepa. Kwa kuwa hatuwezi kuyakwepa inabidi tujue namna ya kuyakubali bila kutuumiza, ujuzi ambao wengi wetu hatunao"
mwisho wa kunukuu.
kama umesoma habari ya Yasinta pale kwenye kibaraza cha dada Koero utagundua kuwa mafanikio ya Yasinta hayakuja kwenye kisahani cha dhahabu, hapana, bali alijua namana boya ya kupambana na vikwazo bila kuvunjika moyo huku akizingatia malengo aliyojiwekea.
kam Mabint wote wanajiuza kw kisingizio cha ukosefu wa ajira na mitaji wangesoma habari ile ingewasaidia namna nzuri ya kufikiri na hatimaye wangebadilika na kujitafutian riziki kwa njia halali. kazi nzuri kaka Mubelwa.
Post a Comment