Tuesday, April 21, 2009

Ni wapi ulipo mstari kati ya kujivunia na kujivuna?

Mwandishi mahiri Anna Quindlen aliwahi kusema kuwa "If your success is not on your own terms, if it looks good to the world but does not feel good in your heart, it is not success at all."
Hakuna anayebisha ukweli kuwa mtu ajivunaye hukera wengi. Lakini pia sidhani kama kuna anayebisha kuwa kila chema tufanyacho twapaswa kujivunia. Tunaweka malengo ya muda mrefu, tunahangaikia malengo hayo na hatimaye kufanikisha tutakacho (hata kama si sawa na jirani, classmate, roommate e.t.c). Wengine husema "kinywa huumba" nNa maana hapa ni kuwa kuna nguvu ya matendo katika kile unenacho. Mara nyingi kunena ni hatua ya pili baada ya kufikiri na kabla ya kutenda. Kwa maana hiyo kuna nguvu ya neno katika kutambua mustakabali wako. Hivyo basi kwa kila chema tufanyacho sio tu twatakiwa kumshukuru aliyetuwezesha, bali pia kujivunia hatua tupigayo. Sasa hapa kwenye kujivunia mafanikio yetu ndiko kuliko na utata.
Ninaye rafiki yangu mpenzi, na kila ninapozungumza naye huniambia hapatikani kwa kuwa yuko "bize na kabiashara" kake. Mwanzo sikuwa nakereka maana sikujua ukubwa wa biashara, lakini inavyoonesha ni kuwa inakuwa, na licha ya matatizo na makwazo ya kiuchumi, bado anaendelea kusonga na biashara yake. Kichwani mwangu nikajiuliza, Ni kweli hataki kusema BIASHARA ili asionekane anajikweza? Lakini pia nikagundua kuwa si yeye pekee. Wengi wetu ndivyo tulivyo. Ukimwambia "nyumba yako nzuri na imependeza" anakujibu "Asante, najitahidi kukapendezesha kakibanda kangu" KIBANDA???? Na wakati mwingine unakuta ndiyo nyumba aliyokuwa akiiota na ameifanyia kazi miaka nenda rudi kuifanikisha. LAKINI BADO HATAKI KUJIVUNIA HATUA ALIYOFIKIA.
Kinachoogopwa hapa ni kulinganishwa, ni kuonekana unajiona bora na kuishi kwa hofu ya "tafsiri" ya wengine kuhusu mafanikio yako.
Kwangu mimi mafanikio ya mtu ni kulingana na alikotoka, aliko, vitendea kazi alivyokuwa navyo, alivyotumia rasilimali na muda na mambo mengine kama maamuzi aliyofanya kufikia alipo. Ni lazima kuanza kujivunia mafanikio yetu badala ya kusubiri tukifa ndio tusifiwe. Natamani rafiki yangu angeacha kuniambia "kabiashara" (kama ambavyo nimemuomba aache) na pia natamani kama wengi wa wanadamu wangeweza kutambua umuhimu na thamani wa kila wanachohangaikia kabla hawajakipoteza.
Peter tosh aliimba kuwa "you never miss your water, till your well runs dry" Tusisubiri kupoteza tulivyonavyo na kutumia historia kujivunia juhudi zetu. Tufanye sasa, ila tusidanganye kwa kujikweza ili tuonekane mashujaa maana kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajivuna badala ya kujivunia.
KWANGU MIMI HUU NDIO MSTARI KATI YA KUJIVUNIA NA KUJIVUNA
Luciano aliimba kuwa
"Satisfy yourself, dont deny yourself, be alright with yourself and you'll survive. Always love yourself, do the same to someone else, always be true to your self....." Msikilize

Jumanne njema

6 comments:

Anonymous said...

wasiojivunia vya kwao ndio wasiothamini vitu vyao halafu wanaanza kutamani vya wengine. Matokeo yake ndio wizi na ufisadi. Kweli kama ulivyosema kwenye wimbo huo kuwa jitosheleze mwenyewe utakuwa alright. Au????

Yasinta Ngonyani said...

Wengi hawajui kuwa mafanikio si ufunguo wa furaha. Furaha ni ufunguo wa mafanikio kama unapenda ulichofanya utafanikiwa na ni lazima utajivunia. Kwani ni haki yako. Mimi nawaza hivyo.

Mwanasosholojia said...

Mzee wa changamoto umenena!hiyo bi sirika ambayo waafrika wengi (au sijui niseme watanzania wengi) tunayo! kuadmit the naked truth huwa ni mgogoro!Ndi maana hata ushahidi unaonyesha kabisa mtu ni fisadi, lakini lazima tu ajitetee...mi mtu safi, si fisadi hata kidogo?sasa sijui inakaa vipi?Tunapaswa kubadilika kwa mtazamo na matendo!

Koero Mkundi said...

Ngoja nikunukuu

"Ninaye rafiki yangu mpenzi, na kila ninapozungumza naye huniambia hapatikani kwa kuwa yuko "bize na kabiashara" kake. Mwanzo sikuwa nakereka maana sikujua ukubwa wa biashara, lakini inavyoonesha ni kuwa inakuwa, na licha ya matatizo na makwazo ya kiuchumi, bado anaendelea kusonga na biashara yake. Kichwani mwangu nikajiuliza, Ni kweli hataki kusema BIASHARA ili asionekane anajikweza? Lakini pia nikagundua kuwa si yeye pekee. Wengi wetu ndivyo tulivyo"

DUH!!!!!
Hapa kama sijaelewa....
Nitakuuliza nyuma ya pazia.....

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

aisee, mimi sijui sana juu ya mafanikio na furaha, japo naamini furaha ya kweli imo ndani mwetu na mimi huitafuta hiyo kwanza

Christian Bwaya said...

Kwa nini watu hukimbilia kutafuta visingizio zaidi (iwe kwa kulaumu wengine ama kukwepa kuwajibika) kuliko kukubali makosa?

Mwanasiasa anamlaumu mwanasiasa mwenzie ama wananchi wenyewe kwamba ni wavivu wa kufikiri. Mwananchi anamlaumu mwanasiasa. Mwandishi naye anatumbikia humo humo kutupa lawama, hata siku moja hasemi na yeye anavyochangia! Mzunguko unaendelea, bila kumfaham kwa hakika ni nani hasa awajibike. Kwa nini? Tusipofika mahali pa kukubali kuwajibika sisi wenyewe mmoja mmoja tutaendelea kuyazunguka matatizo.


Yasinta, mafanikio ya kweli ndiyo furaha yenyewe. Tukifikiri mafanikio ni hela, utajiri na mambo kama hayo, ni kweli kwamba hatutaipata furaha ya kweli.

Tujiulize mafanikio ni nini hasa? Huenda mafanikio ni kule kuijua iliko hiyo furaha ya kweli ambayo nadhani ndilo lengo la kuishi kwetu!