Wednesday, April 15, 2009

Nisaidie kumjibu Kaka Kamala

Picha kwa hisani ya Kijiweni, Nyegerage blog
Ama kweli namna uonavyo tatizo ndilo tatizo. Katika "toleo" langu la jana niliandika kuhusu masuala ya uwezo wa ubongo wa mwanadamu kudikiri. Na katika kuandika huko nikasema "Nimekuja kutambua kuwa watu wengi waliofanikiwa walianza harakati za mafanikio yao baada ya kukumbana na matatizo fulani." Kwangu sentensi hii ilijitosheleza kwa sababu niliamini kuwa kufanikiwa ni pamoja na kutimiza yale upendayo ama kuondokana na hofu uliyonayo. Moyoni niliamini kuwa hayo ni mafanikio. Lakini Kakangu Kamala mwenye kusoma "katikati ya mistari" na kutafakari (heshima kwako kwa hili), akaniwekea maoni yaliyonifanya nijiulize mara mbili juu ya nilichoandika.
Maoni yake (ambayo yalikuwa mafupi na ya kutambulisha ama kutafakarisha) yalinifanya nirejee upya katika kile nilichoamini na kukitafsiri kama mafanikio. Katika tafakari yangu nikakumbuka msemo usemao "katika hali yoyote uliyonayo, ingeweza na inaweza kuwa mbaya zaidi ya hapo" na huu ukanifanya nitambue kuwa kila binadamu (kwa kiwango chake) yuko kwenye mafanikio. Lakini hili halikunipa jibu kamili kuhusu swali la Kaka Kamala aliyesema "najiuliza ulichokisema juu ya mafanikio ni nini? mtu aliyefanikiwa yuko je na anafananaje? na asiyefanikiwa je? kweli kuna ambaye hajafanikiwa maishani?"
Binafsi sina jibu la jumla hivyo nimeona niweke hapa barazani ili wewe usomaye utafakari, kisha unisaidie kumjibu Kaka Kamala

4 comments:

Koero Mkundi said...

Naomba nimjibu Kamala...
Mimi naona kufanikiwa ni vile mtu anavyo yatafsiri mafanikio kwa mtazamo wake na baada ya kufiki hayo mafanikio basi atakuwa amefanikiwa. nadhani sitakuwa tofauti sana na wewe mtoa mada.
Kwa mfani ule Yasinta niliyemuandika pale kibarazani kwake alijiwekea malengo ambayo kwake aliyaona ni mafanikio kwa hiyo ukimuuliza sasa hivi kuhusu kufanikiwa ni lazima atakiri kuwa kwa kiasi fulani amefanikiwa...
nadhni nimejibu....

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ndio koero labda ni kweli. nilisoma mfano mmoja kwenye kitabu cha mmarekani eckhart Tolle cha 'a new earth' (zaidi fungua eckharttolle.com) katika kitabu hicho alioa mfano wa jamaa ambaye jibu lake kwa maswali lilikuwa ni labda! hana uhakika.

jamaa mwenyewe alishinda bahatinasibu na kupewa gari. nduguze wakamuuuliza; umefanikwa sana? akajibu labda. akiendesha gari hilo alipata ajali na kulazwa hosp. ndugu wakaja na kusema gari hili ni nuksi, bora usingelishinda, akajibu labda. akiwa bado kalazwa, nyumba yake ikaungua na kuteketea kabisa. nduguze wakasema tena; bora ulipata hajali na kulazwa, vinginevyo ungefia ndani ya nyumba kwa moto. yeye akajibu, labda!

ni kitu gani kizuri na kibaya maishani mwetu? wengi hatuwezi kutafakari vyema juu ya hili. mafanikio ninini? hatujui.

basil mramba, E Lowasa na wengine, walifanikiwa sana kupata uwaziri na walienda makanisana na kwa waganga kufanya tambiko za shukrani, lakini sasa hivi wanajuttia nafasi hizo nakutamani bora wasingezipata. ungewauliza wakati wanachaguliwa wangekuwambia ndio, japo leo wanatamani wasingegombea hata ubunge wao!

unaona matajiri kama akina mengi wanalalamika na kufungua kesi za kuchafulia jina lao na heshima zao kwa sababu ya mafanikio yao ya utajiri, japo wewe usiyechafuliwa kiurahisi, maisha ni matamu sana. sasa je, heshima ya hawa inakuwa kwenye kauli yako mchafuaji au inalala wapi haswa? ndo mafanikio haya ya kutokujisafisha mwenyewe mpaka mtu asema 'am sory'? hata hivyo, masikini(kama wapo) nao wanalalamika kwa umasikini wao.

ni yupi aliyefanikiwa kati ya mwenye hofu juu ya kesho na yule anayeacha kila hali ije na iende itakavyo?

sijui sana kuhusu mafanikio

Simon Kitururu said...

Anayeishi kafanikiwa , yuko hai.
Aliye fariki kafanikiwa, kafa.

Asiyefanikiwa, kafanikiwa angalau hata kufikiria hajafanikiwa:-(

Kufanikiwa ni jumuiya ya vitu.

Kuanzia kupumua, kuamka, kufikiria , kunya mpaka kufa.

Na ukiamua unaweza ukachagua tu ni nini hujafanikiwa katika mafanikio ya siku.

Ni mtazamo tu!

Mary Damian said...

Asante sana kaka Simon! mimi mtazamo wangu mtu kufanikiwa au ukijisifu umefanikiwa katika maisha yako ni kuishi ukimuhofu Mungu ukiaminini bila yeye hakuna utakalolifanya jema usifanikiwe. Baada ya hapo mafanikio mengine ya mwili yataonekana kwa wazi!