Monday, April 20, 2009

Za Kale vs Maisha ya sasa.... CHATU MKALI

Maalim Gurumo
Mwaka 2003 nilibahatika kuzungumza na mkongwe wa Muziki nchini Tanzania Muhidin Maalim Gurumo. Katika kuhojiana kwetu nilimuuliza kuhusu maudhui ya muziki wa sasa na namna ambavyo unajenga chuki baina ya wanamuziki. Alichoniambia ni kuwa wasanii wa sasa hawafikirii namna nzuri ya kuwasilisha ujumbe wao kwa walengwa. Aliniambia kuwa "madongo" hayakuanza leo. Alinipa mifano ya nyimbo ambazo zilikuwa zikifikisha ujumbe kwa wahusika na wakati huohuo kuendelea kuburudisha wasiojua kinachoendelea. Akanipa mfano mingi ya majibizano yaliyotokea miaka iliyopita na mwisho akazungumzia walivyopigwa "dongo" walipoikacha DDC MNlimani Park Orchestra na kuhamia OSS. Basi kule Mlimani wakashuka na Mv Mapenzi II (mtakumbuka kuna sehemu wanasema bahari imepatwa na dhoruba na nahodha na wengine wamejitosa baharini, ila wengine wenye ujasiri wanaiendesha meli kuelekea bandarini). Siku hiyo ndio nilijua kuwa ule wimbo ambao nilikuwa nikiufikiria kila nikikwea vyombo vya maji ulikuwa na maana zaidi ya nilivyofikiri. Kisha akaniambia kuwa ndipo alipowaonya na kuwajibu kwa wimbo CHATU MKALI.
Nikarejea kuusikiliza nikagundua ukweli wake. Ndio maana unasikia maonyo mengi kuhusu "kutomchezea chatu". Labda ukisikiliza kwa maana hii utaweza kugundua ujumbe ulivyowafikia wana Sikinde lakini pia kutuonya kuhusu CHATU MKALI. Wewe ulikuwa ukielewaje?
Msikilize hapa na burudika huku ukielimika

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Naona umebadili picha umependeza. Za safi kwa sisi watu wa kale. Nimeupenda wimbo huu

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Gurumo ni mmoja kati ya wanamuziki bora kabisa. Nina VCD yao ya AJALI wakati ule Marehemu Moshi TX Williams akiwa hai na huwa sichoki kuiangalia. Sauti yake nzuri na kwa kumwangalia tu unaweza kuiona busara. Asante kwa wimbo huu.

Mzee wa Changamoto said...

Asanteni kwa kuburudika pamoja nasi.
Amani kwenu