Monday, April 27, 2009

Za Kale vs Maisha ya sasa..KIFO

Wachambuzi Kaka Kaluse na Kaka Kamala wamezungumzia saana kuhusu Kifo. Wamezungumzia kuhusu majina na matukio na hata hisia zake na pia namna tunavyotakiwa kukichukulia. Mada zao juu ya hili hazikuwa rahisi kuzikubali hasa kama hukubaliani ama kuamini katika "maisha baada ya maisha". Lakini hapa sijiulizi juu ya tafsiri wala namna kijavyo, bali najiuliza kuwa endapo tungekuwa tunajua siku ya kufa kwetu, tungekuwa watu wa namna gani? Tungekuwa wema tukiamini kuwa tunamalizia siku zetu kwa wema zaidi? Tungekuwa wakatili hasa tukijua kuwa hakuna jema tunaloweza kufanya likatusaidia kuishi kuiona kesho? Tungekuwa na maandalizi mema kwa vizazi vijavyo kwa kupanga maandalizi ya kifo, msiba na gharama zote ama ingekuwaje?
Sijawahi kupata jibu la swali hili ambalo kwa namna moja ama nyingine mwimbaji Remmy Mtoro Ongala aliuliza alipokuwa "akikihoji" kifo kuhusu uwepo, uhalali na hata matendo yake kwa wanadamu. Ukimsikiliza kwa makini utasikia maandalizi anayosema anataka kuyafanya kuepusha matatizo yanayojitokeza kwa waroho wa mali za wafiwa akisema "sitakulaumu maana nitakuwa nimeacha msimamo nyuma yangu."
Swali ni kuwa tungekuwa binadamu wa namna gani leo, kama tungekuwa tukijua kuwa kifo chetu ni kesho?


** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

3 comments:

Mwanasosholojia said...

Mzee hii imekaa vizuri!Kama ulivyosema, kama tungekuwa tunajua tunakufa lini, nafikiri hata haya matendo yanayofanywa na baadhi yetu, ikiwemo ufisadi, yasingekuwepo!Dunia ingekuwa safi! Ahsante kwa zilipendwa, kweli ya kale ni dhahabu

Yasinta Ngonyani said...

Yah, ni kweli kifo hakina huruma kinakuja saa na wakati wowote ule. Ni kweli kama tungejua unakufa kesho kweli ungekuwa ufisadi.

Nachukua nafasi hii kukupa salam kutoka kwa mume wangu wa kuweka kipande hiki. Kwani ktk mwanamuziki wa Tz Remmy Mtoro Ongala ni mpenzi wake anapenda sana kusikiliza . Ahsante sana jumatatu njema

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kila mtu anajua juu ya kifo chake. hakuna asiyejua kuwa atakufa. wote tunajua ila tunakaidi na kutamani dunia.

wabuddha wanasema life is uncertain but death is certain. kusema hujui kifo chako ni kujidanganya tu.

kristo alijua uzuri na utamu wa kufa akawaacha wajinga wauchezee mwili wake ili yeye arudi zake kwenye raha.

yasinta kifo kina huruma na ndiyo maana unajua kipo chaja. by the way, mnachokiita kifo sio kufa bali ni kuuvua mwili!