Monday, April 6, 2009

Za Kale vs Maisha ya sasa.....MTAA WA SABA


Kuna wakati huwa natamani kuandika "Paradox of our music"
Yaani nieleze kuwa
Siku hizi kuna waimbaji wengi lakini wanamuziki / wasanii wachache,
Kuna studio nyingi lakini muziki mchache, kele nyingi,
Kuna vifaa vya kisasa lakini ubora wa muziki unazidi kuporomoka,
Kuna matukio mengi ya kueleza na kuimba / kutetea lakini fikra ni fupi na zimejaa kwenye mapenzi,
na mengine mengi.
Haya yote ni kwa kuwa ninapolinganisha kazi za zamani na sasa napata mashaka kama wasanii wengi wa sasa walikuwa na watu wanaowafuatilia tangu enzi hizo kabla "hawajajiingiza" kwenye muziki. NA HAPA NASEMA WENGI NA SI WOTE.
Kuna mambo yasiyobadilika kwenye muziki na kuna yanayobadilika. Muziki wa zamani ulikuwa wa kuiwakilisha zaidi jamii, lakini sasa ni hisia binafsi za wasanii. Zamani waliimba kuhusu mambo ambayo wao na pengine jamii iliyowasababishia kutunga nyimbo hizo iliamini ama kufanya ama yalifanyika hata kama hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa uwepo wake. Miziki ya zamani iliimba upendo zaidi ya mapenzi na sasa wanaimba mapenzi zaidi ya upendo. Wengi hawatafakari njia sahihi ya kuielimisha jamii na ndio maana hata unaposikiliza baadhi ya nyimbo zao ambazo zinapaswa kuelimisha (mfano kuhusu UKIMWI) unaishia kupata burudani kuliko mafunzo maana wameegemea zaidi kuburudisha. Na ndio maana licha ya kuimba kuhusu mapenzi, ndoa na mahusiano vinazidi kuyumba na kudumu kwa muda mfupi zaidi.
Anyway, Wiki hii katika kipengele chetu cha ZILIPENDWA tunaye Mbaraka Mwinshehe ambaye anakuja na kibao chake MTAA WA SABA. Aliimba kile kilichokuwa kikiaminika (hasa kwa nyakati zile) kuhusu imani ambazo zilitawala jamii yetu kwa wakati ule. Nyakati ambazo waliamini kuwa mikosi yaletwa na makazi ama majirani na kisha akarejea kwenye suluhisho lililompa amani moyoni kuwa kuhamia mtaa wa saba kulimpa amani, hakuna mabundi juu ya bati wala kulialia, kazi inazidi kumnyookea na hata mahusiano yake na majirani yakaenda sawia.
Kaaazi kwelikweli!!!! Ni mambo ya nyakati na yanarejesha hisia na kumbukumbu nyingi za wakti ambao wengi wanakumbuka mengi
Unakumbuka nini umsikiapo M'baraka katika wimbo huu?
Jukumbushe

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

1 comment:

Yasinta Ngonyani said...

Aise! nimefurahi sana umenifanya nimkumbuke mama huu ulikuwa ni wimbo wake Ahasante sana. Kweli nyimbo za zamani ni nzuri na zina mafunzo. kazi kwelikweliii:-)