Saturday, May 23, 2009

Ndani ya mji kutoka "shamba".

Nimerejea kutoka shamba. Na nilipoondoka na kuaga wiki mbili zilizopita, nilitakiwa mengi mema na kisha wapo walioniuliza kama nilikuwa narejea BUKOBA maana nimesema naelekea shamba. Hili lilinifanya nijiulize mara kadhaa kuwa SHAMBA NI NINI? Pengine kwa kutokuwa muwazi kuhusu "shamba" langu, yawezekana niliwaweka wengi kwenye kitendawili.
Kwangu mimi, naamini kuwa shamba ni lile ambalo unawekeza ukitaraji kuvuna. Mfano halisi ni kila miaka mitano nyumbani ambao watu huacha shughuli zao za kawaida na kuwekeza kwenye uongo wa wanasiasa, wakiwafuata, kueleza sera na ILANI zao na kisha kuwahakikishia nafasi zaidi za kutuibia na kwa wakati huo, wanaishi maisha bora kuliko wanapokuwa wakijishughulisha na kilimo. Ila na mavuno yake twayaona pia maana tunaendelea kuwa na watawala badala ya viongozi. Shamba langu halikuwa hilo, shamba langu lilikuwa SHULE. Nilikuwa nimebanwa na maandalizi ya mwisho wa muhula na niliomba ka-muda ka ziada kujiandaa na hilo. Na sasa nimemaliza msimu na nimerejea. Lakini kwenye msimu huu kulikuwa na mengi ya kuvutia. Nilibahatika kufanya mengi ndani ya darasa na ilikuwa vema sana. Niliweza kumualika mmoja wa wahandisi ambaye pia ni mmoja wa wanaanga waliofanikiwa zaidi katika historia ya NASA Dr Don Thomas (BOFYA HAPA KUMSOMA) ambaye amekwenda kwenye Space Station mara 4 na ambaye nilionana naye kazini na kisha kumualika kuja kutoa mada kwenye klabu yetu ya wanafunzi wahandisi
Nikapata nafasi ya kutembelea "shamba tarajiwa" la Maryland ambapo tulielimishwa mengi kuhusu fani na malengo ya kuifanikisha.
Kisha katika darasa hilohilo nikafanikiwa kutembelea NASA GODDARD SPACE FLIGHT CENTER (Bofya hapa kusoma zaidi kuhusu Hubble Telescope) ambayo ndio taasisi yenye wanasayansi wengi zaidi nchini Marekani na kushuhudia ufungaji wa vifaa mbalimbali ambavyo vilitumika kwenye kukarabati Hubble Telescope katika mission inayotegemewa kumalizika leo ambapo wanasayansi hao wanatarajiwa kurejea.
Nilifurahia ziara hiyo niliyoongea na wanasayansi wengi lakini nilibahatika kuona CHUJIO KUBWA ZAIDI LA HEWA DUNIANI
Chujio la hewa ndani ya chumba cha majaribio NASA
TAZAMA ZIARA YANGU HAPA. Kwa kuwa hawakuruhusu video camera, nilitumia kamera ndogo ya still. Nisamehe kwa ubora hafifu

Lakini pia hata wakulima (wanafunzi) wenzangu pamoja na Bwana shamba (mwalimu) wangu walikuwa sehemu ya furaha kwa msimu huu. Sasa nimerejea na naamini kwa muda nitakaokuwa "mjini" tutaendelea "kubambana" mara kwa mara vibarazani.

Pamoja Daima na salamu tele toka "shamba"

5 comments:

Anonymous said...

Shambani, shambani,
Shambani, shambani,
shambani,
Mazao bora shambaaani.

Jama twendeni shambani,
Wananchi tukalime, x2

Tusikae mitaani, (taaani),
Wanawake kwa Waume (waume), x2

Wanawake kwa Waume.

Ni furaha kusikia habari za shamba.
Karibu tena kilingeni!

Evarist Chahali said...

Kwa hakika hayo ndio "mashamba" kama ulivyosema Mzee.Maana hawa wenzetu "wanatoka jasho" (kiteknolojia) na baadaye wanatengeneza mazingira ya mavuno yatakayowatosheleza kwa muda mrefu.

Sie tumepata walafi ambao hata tungebarikiwa kuangushiwa teknolojia kama za NASA,basi sia ajabu wanaanga wetu wangeishia ku-starve huko kwenye outerspace baada ya ufisadi....kama wanaiba mitambo ya DNA kwa Chief Chemist,hawashindwi kuiba nyenzo muhimu kwa wanaanga!

Mzee,pamoja na hayo naomba pokea hongera kwa hayo yaliyojiri class.

Yasinta Ngonyani said...

Mie hizo picha za shamba tu ndio zilizonofurahisha. Safi sana basi karibu tena.

Mzee wa Changamoto said...

Shukrani sana kwenu nyote. Uwepo wenu ni sehemu kubwa ya kuwepo kwa kilinge hiki na pia (kwa namna moja ama nyinginne), upangiliaji wa shughuli zenu na uelimishaji huu muufanyao kupitia blogs, unatupa njia nasi tulio nyuma yenu kujua kuwa twaweza kusonga kielimu huku tukitimiza tupendayo. Yaani kujua kuwa kazi na kusoma haviwezi kuwa sababu ya kututenga na blogs tuzipendazo. Ni mgawanyo mzuri wa muda na "kufanya jambo la kwanza kwanza" (do first thing first)kutakakowezesha yote.
Baraka kwenu na karibuni tena na tena

Christian Bwaya said...

Sa'Subi umenikumbusha mbali. Ha ha ha haaaa! Miaka ile natoka shule darasa la ngapi sijui saa nane nane ama tisa hivi kama sikosei. Njaa inauma acha kabisa...nakutana na kiashirio hiko maalumu kwa kipindi cha salamu za mkulima...Du umenirudisha mbali kweli.

Kuhusu shamba hilo, Mube hongera kwa fursa hiyo. Tuna safari ndefu kufikia waliko wenzetu.

Vyuo vya Bongo kazi kukaririshana tu hakuna cha maana tunachofanya kwa watu wetu.